Tuesday 19 September 2017

STANDARD GAUGE YASHIKA KASI



SERIKALI imesema hivi karibuni, inatarajia kutia saini makubaliano ya sehemu ya pili ya ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), kutoka Morogoro mpaka Dodoma.

Imesemahatua hiyo itafanyika wiki mbili zijazo, ambapo awamu hiyo, itakuwa na urefu wa kilomita 336 na kwamba, serikali imekusudia kukamilisha mradi huo kwa wakati.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, jana, kwenye mkutano wa mwaka wa maendeleo ya miundombinu ya barabara na reli, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema kwamba, serikali imedhamiria kufanya hivyo.

Waziri huyo alisema, mradi huo wa ujenzi wa reli, utasaidia kuongeza kasi ya maendeleo katika kufikia uchumi wa viwanda na kwamba, ili kufika huko, hakuna budi kutengeneza miundombinu ya uhakika ya reli.

Katika maelezo yake, Profesa Mbarawa alieleza namna ujenzi wa reli hiyo utakavyosaidia kuimarisha uchumi wa viwanda, ambapo wafanyabiashara kutoka nje ya nchi, watatumia bandari kuu ya Dar es Saalam kutokana kasi ya usafiri huo wa reli.

Alisema serikali ya awamu ya tano, imeweka dhamira ya dhati ya kuwa na miundombinu mingi ya reli na barabara kwa kuitumia kufikia uchumi wa kati kama dira ya serikali inavyofafanua.

“Reli hii itakuwa na spidi ya kilomita 160 kwa saa kwa upande wa abiria huku kwenye usafirishaji wa mizigo ni  kilomita 120 kwa saa, ambapo reli ya Kenya inakwenda kwa spidi ya kilomita 120. Tutawazidi na hivyo kuwa nchi ya kwanza kuwa na uwezo wa reli hii barani Afrika,” alisema.

Waziri huyo aliongeza kuwa, ujenzi wa reli hiyo katika sehemu ya kwanza, unakwenda vizuri, ambapo wakandarasi wanamalizia hatua ya kutengeneza matatu kwenye maeneo husika.

Kwa upande wake,  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), Masanja Kadogosa, alisema hatua ya ujenzi wa reli hiyo katika sehemu ya kwanza, unatarajia kukamilika kwa wakati.

Alisema ujenzi wa reli hiyo utasaidia katika kufikia Tanzania ya viwanda kutokana na zaidi ya asilimia 40 hadi 50 ya gharama ya usafirishaji wa bidhaa unawagharimu sana wafanyabiashara.

“Baada ya kupata fursa hii ya ujenzi wa reli hiyo, wafanyabiashara wengi kutoka Burundi, Rwanda, Uganda watatumia reli hii kutokana na uharaka wake, ikilinganishwa na reli ya Kenya, ambayo inasafiri umbali wa kilomita 140 kwa saa,” alifafanua mkurugenzi huyo.

Mbali ya hilo, Mkurugenzi huyo alisema, kutokana na kuwepo kwa umuhimu wa haraka wa wafanyabiashara hao kutaka kupata mizigo yao, ni dhahiri watatumia reli hiyo.

“Licha ya kutumia reli yetu ikilinganishwa na ya Kenya, bado kutakuwa na fursa kubwa ya kutumia Bandari Kuu ya Dar es Saalam, kwa ajili ya kusafirishia mizigo kwenda kwenye nchi mbalimbali zinaotuzunguka hivyo tutanufaika kiuchumi,”alisema.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania(TPSF), Godfrey Simbeyi, alisema baada ya reli hiyo kukamilika, itasaidia kuvutia wawekezaji wengi nchini kwa sababu kutakuwa na uhakika wa miundombinu.

Alisema ujenzi wa reli hiyo, utaongeza juhudi za kukuza na kuboresha mazingira mazuri ya kibiashara kwa wafanyabiashara nchini, hasa watokao nchi za Rwanda, Burundi, Zambia na Uganda, ambapo kuna muungano wa kibiashara.

“Niipongeze serikali kwa kutoa fursa kwa sekta binafsi katika kuwashirikisha kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo mfano, wazalishaji saruji, nondo na vinginevyo, watanufaika kwa kiasi fulani,”alisema.

Aprili 12, mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli, aliweka jiwe la msingi katika ujenzi wa reli hiyo eneo la Pugu jijini Dar es Saalam, ambapo mradi huo unatekelezwa.

Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi ni kilomita 300, unaoanzia Dar es Salaam mpaka Morogoro, wenye thamani ya sh. trilioni 2.8

No comments:

Post a Comment