RAIS Dk. John Magufuli, ameagiza eneo lote
linalozunguka machimbo ya Tanzanite, lizungushiwe ukuta huku yeye akiingia
rasmi kupigana vita na wezi wa madini hayo.
Agizo hilo alilitoa jana, kabla ya kuzindua
barabara ya KIA hadi Mererani, yenye urefu wa km 26, wilayani Simanjiro mkoani
Manyara.
Rais Magufuli alisema, Tanzanite ina eneo la
kilomita za mraba 81.99 na kuna ‘block’ ambazo zimegawanywa kutoka block A hadi
D, sawa na umbalo wa km 13.
"Zilizobaki ni block moja hadi nne, ambazo
uzalishaji wake ni mdogo. Tanzanite hii, hakuna sababu ya kumung'unya maneno,
zinaibiwa sana, ni shamba la bibi, nafikiri la mabibi waliokufa miaka mingi.
Watu wanachukua kuliko hata shamba la bibi," alisema.
Alisema kuwa,ili kuzuia wizi huo, ameamua eneo hilo
kuanzia block A mpaka D, ambalo lina mali nyingi za Tanzanite, lizungushiwe
ukuta.
“Naagiza Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kupitia
Suma JKT na wengine, kuanza kujenga ukuta eneo lote na kazi hii ifanyike
haraka," alisema.
Pia, alisema watakapokuwa wanajenga ukuta, wanatakiwa
kuweka eneo lote uzio wa umeme, kamera na mlango mmoja na vifaa maalumu vya
kuzuia wizi.
"Nataka niwaambie, hata kama utameza Tanzanite,
kile kifaa kitaonyesha tu, hata kama utaivaa kwenye kiatu itaonekana ili
Tanzanite inayochimbwa hapo serikali ipate haki yake, mchimbaji naye akapate
fedha yake," alisisitiza.
Alisema sababu ya kuweka ukuta ni kuhakikisha mali
hiyo haiibiwi hovyo na kwamba, haiwezekani mtu achimbe, halafu ikauzwe nje ya
nchi.
SOKO KUHAMIA SIMANJIRO
Vilevile, Rais Magufuli aliagiza soko la Tanzanite
lihamie Simanjiro badala ya Arusha, ili wanunuzi wanaotoka nchi za nje waifuate
eneo hilo.
"Kwa sababu njia ya kufika Simanjiro ni
nyepesi, barabara ni lami, wakija huku wananchi wa hapa watafanya biashara na
Simanjiro itaendelea," alisema Rais Magufuli.
Aliongeza kuwa, Tanzania ni nchi tajiri kwa sababu
ilipendelewa na Mungu, ikapewa madini ya Tanzanite, ambayo hayapo mahali
pengine popote duniani.
"Lakini tujiulize haya madini yanatusaidia
sisi? Mungu ametupa madini, sisi tunapata shida. Hatuna barabara, hospitali,
maji, shule, lakini Tanzanite tunayo, inatumikaje?" Alihoji huku
akishangiliwa kwa mayowe na wananchi.
Rais Magufuli alisema, tatizo lililopo Tanzania siyo
vyama, hivyo ni vyema kujiuliza sababu ya rasilimali kuibwa.
"Tanzanite hii ingekuwa imepewa nchi nyingine,
hapa pangekuwa kama Ulaya, lakini inawezekana Mungu alifanya makosa, akaweka
Tanzanite kwa Watanzania, lakini kama hajafanya makosa, tuanze
kubadilika," alisema.
Alisema kama Tanzanite ingetumika vizuri,
wasingeshindwa kununua hata gari moja la wagonjwa ili liwasaidie wananchi wa Simanjiro.
"Sasa ninawaomba Watanzania, tusimame imara,
tumeanza vita ya kupambana na mafisadi wa uchumi wetu, ni lazima twende pamoja.
“Vita inavyotokea, mbinu za mabeberu huwa ni
kuwachonganisha wapiganaji. Mtaanza kujiuma na kusemana wenyewe ili wao
wafanikishe malengo yao," alisema.
Aliongeza: "Ndiyo maana nazungumza kuwa,
maendeleo hayana chama. Inawezekana ninyi mkaanza kugombana hapa Simanjiro,
huyu ni mbunge wa CHADEMA, huyu ni mwenyekiti wa CCM, mnachelewa, adui yetu
siyo huyo, adui yetu yupo pale amekaa mnamuangalia (mafisadi), mtang'ang'ania
ya pembeni, mnasahau ya muhimu."
Rais Magufuli alisema, baadhi ya viongozi wanaopewa
mamlaka ya kusimamia rasilimali za nchi, ndio wanakuwa mafisadi wa kuwaumiza Watanzania.
"Tunasahau tulipotoka, mahali tulipo na
tunapokwenda. Hii Tanzanite leo ipo, lakini haitakaa miaka yote, siku moja
itaisha na ikiisha tutaachiwa mashimo na kubaki masikini. Katika uongozi wangu,
nimeamua kuiongoza hii vita,"alisisitiza.
Kuhusu hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa kwa
wawekezaji, alivipongeza vyombo vya ulinzi na usalama na kuwataka wale
waliokuwa wakihusika kusaidia kutoa taarifa hizo, kuachiwa ili wakae na tume ya
kujadili madini inayoongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba
Kabudi, ili waweze kuupitia mkataba na kuurekebisha ili utiwe saini upya.
"Nina hakika watu wa Tanzanite na wawekezaji
wengine watakaa na serikali ili kuhakikisha tunatengeneza mkataba ulio na faida
kwa serikali. Hatuwezi tukawa na mikataba ya kinyonyaji, halafu wananchi
wanaendelea kusikitika na kulia, nimesema hapana ndani ya mamlaka yangu,"
alisema.
BoT YAPEWA JUKUMU
Pia, Rais Magufuli ameitaka Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), kutengeneza mkakati wa kushiriki katika ununuzi wa madini hayo.
"Kwa sababu Tanzanite huwezi kudanganya kama
ambavyo unaweza kudanganya dhahabu. Dhahabu ukichukua lichuma yenye rangi ya
njano hivi, ukiliyeyusha unaweza ukamdanganya mtu, lakini Tanzanite ni vigumu. Nataka
twende na wakati kwa faida ya Watanzania," alisema.
POLISI LINDENI TANZANITE
Pia, alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama
kuhakikisha vinalinda na kusimamia madini hayo yasivushwe.
"Anayetoka awe mtu, ambaye amelipa naye
anaenda kwa usalama kuuza hata kama anataka kwenda kuuza Ulaya," alisema.
Aliongeza kuwa, katika hatua ambazo wameanza
kuzichukua, kuna watu ambao wameanza kukimbia kutokana na kuogopa, kwa sababu
walikuwa wakifanya hovyo.
Akizungumzia barabara hiyo, alisema wakati akiwa
waziri wa ujenzi, walipokuwa wakiweka jiwe la msingi, watu walikuwa
wakizungumza kuwa, haiwezi kujengwa na kwamba ni siasa tu.
"Walisema hii ni siasa, ndiyo maana tumeweka
jiwe la msingi mwaka 2010, wakati uchaguzi umekaribia. Kwamba hii ni janja ya
CCM na hii ni siasa, haiwezi kujengwa barabara ya lami. Leo barabara ipo,"
alisema.
Aliwashuruku wananchi wa Manyara na Simanjiro kwa
kura nyingi walizompa na kuahidi kuendelea kuwatumikia kwa sababu walimchagua
bure.
"Mmenipa jukumu hili kwa ajili ya kuwasaidia
na kuwafanyia kazi. Naahidi kuwa sitawaangusha, nawahakikishia katika uongozi
wangu, sitawabagua Watanzania," alisema.
Aliishukuru Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano na watendaji wake, Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na
wakandarasi kwa kumaliza barabara hiyo yenye urefu wa km 26, ambayo imejengwa
kwa sh. bilioni 32.5.
"Pia, nawapongeza Watanzania wote ambao
wamekubali kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi yao," alisema.
Rais Magufuli alisema wamejipanga kutekeleza Ilani
ya CCM, ambayo iliahidi kutengeneza barabara na kuwaletea Watanzania maendeleo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema barabara hiyo ni kiungo muhimu cha
Wilaya ya Simanjiro na Arumeru.
Alisema kukamilika kwa barabara hiyo kumerahisisha
mawasiliano kati ya machimbo ya Tanzanite, eneo la uwekezaji la Mererani na
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
"Ujenzi wa barabara hii ni moja ya miradi ya
barabara, ambayo inasimamiwa na serikali yetu kwa asilimia 100," alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera alisema mkoa
wake una changamoto mbalimbali, ikiwemo ya ukosefu wa maji.
Alimpongeza Rais Magufuli kwa kupigania rasilimali
za Watanzania, ikiwa ni pamoja na kupambana na mafisadi.
"Kwa muda mfupi ulioingia madarakani, umefanya
mambo makubwa sana, sisi wananchi wa Manyara tunakupongeza sana," alisema.
No comments:
Post a Comment