Thursday 21 September 2017

BOMOA BOMOA YATIKISA JANGWANI, NYUMBA ZAVUNJWA, MABOMU YARINDIMA




NYUMBA zilizojengwa katika eneo la Bonde la Msimbazi, katika Manispaa ya Ilala, eneo la Jangwani, jijini Dar es Salaam, zimebomelewa.
Operesheni ya kuzibomoa imekuja siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutangaza kusimamisha bomoa bomoa yoyote bila idhini yake.
Jana, wakati bomoabomoa hiyo ikifanyika, wakazi wa Jangwani walionekana kuwazuia askari polisi kutekeleza kazi hiyo.
Hata hivyo, polisi walilazimika kutumia mabomu ya kishindo kuwatawanya wananchi hao, waliopinga kubomolewa nyumba zao.
Tafrani hiyo ilitokea saa 5.00 asubuhi, baada ya Maofisa wa  Halmshauri ya Manispaa ya Ilala, kufika katika eneo hilo kwa ajili ya kubomoa nyumba zote zilizojengwa Jangwani.
Wananchi walionekana kujihami kwa silaha za jadi, kama vile mapanga, mawe, marungu, fimbo, chupa, visu na nondo.
Walianzisha vurugu kubwa kwa kuwashambulia askari, ambao nao walijihami kwa kulipua mabomu hayo ya kishindo wakiwa kwenye magari yao zaidi ya sita.
Wananchi hao pia walichoma moto matairi ili kufunga barabara ya Morogoro,  huku wakiwashambulia hovyo wapita njia na kuwapora vitu.
Vurugu hizo ziliendelea kwa kuyarushia mawe magari, yakiwemo yale ya Mwendokasi, yanayofanya safari zake katika barabara hiyo.
Aidha, kituo cha mabasi ya mwendokasi kilichoko Jangwani, kilivunjwa vioo kwa mawe.
Hali katika eneo hilo ilikuwa siyo salama, kwani watu walishindwa kupita huku baadhi ya waandishi wa habari nao wakifanyiwa fujo.
Ilipofika saa 5:30, polisi walirejea katika eneo hilo na kuanza kulipua mabomu zaidi kwa kishindo.
Mitaa yote ya  eneo hilo, iligeuka uwanja wa mapambano kati ya raia wa Jangwani na polisi, kwa takribani dakika 45, hadi askari walipofanikiwa kudhibiti eneo  hilo na kuanza kuwakamata watuhumiwa.
Baada ya polisi kuwadhibiti raia, karandinga likaanza kuvunja nyumba.
Idadi kubwa ya watu hawakuwa wametoa samani zao nje, huku wengine wakikimbia kuhofia kutiwa nguvuni baada ya kushiriki vurugu dhidi ya askari.
Wakizungumza na Uhuru, baadhi ya wananchi waliokuwa wakiishi eneo hilo, walisema  wameshangazwa na hatua ya kuvunjiwa nyumba zao, kwa sababu kuna kesi inaendelea mahakamani.
“Sisi hatukupewa viwanja huko Mabwepande. Tulikuwa tunasubiri fidia zetu serikalini ili tuondoke,”alisema Yusuf Hemed.
“Tunazo familia kubwa, hatujui wapi pa kwenda. Tumepoteza mali zote. Sijui nitafanya nini mimi?” Alisikitika mwananchi mmoja, aliyejitambulisha kwa jina moja la Halima.
Polisi Mkoa wa Ilala, ilithibitisha kutokea kwa tukio hilo  na kusema,  amri ya kuvunjwa ilitolewa na Halmshauri ya Manispaa ya Ilala ili kupisha ujenzi wa Mradi wa Kusafisha Maji Taka, jijini Dar es Salaam.
Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka (DAWASA) .
Kamanda wa Polisi Ilala, Salum Hamduni, alisema polisi walilazimika kufyatua mabomu ya kishindo baada  ya raia kukaidi amri ya kuondoka kwa hiari na amani.
“Polisi tumetumia nguvu ya kawaida kuwadhibiti na hatukupiga mabomu ya machozi wala risasi.  Tulipiga mabomu ya kishindo tu,  tulifanikiwa kuwakamata baadhi ya watuhumiwa, ambao tunaendelea kuwahoji kisha tutatoa taarifa rasmi,”alisema Kamanda Hamduni.
Alisema, eneo hilo litaendelea kudhibitiwa mpaka  uvunjaji utakapokamilika na  akahakikisha hakuna mtu atakayerejea.
“Kikubwa niwatake wananchi kutii sheria na amri zinapotolewa. Kazi ya kuvunja ilikuwa inafanywa na manispaa, polisi kazi yetu ni kusimamia amani na kulinda mali zisiibwe,”alisema Kamanda huyo.

No comments:

Post a Comment