Thursday, 3 September 2015

DK. MAGUFULI ASHAURIWA KUMUIGA MWALIMU NYERERE


NA WILLIAM SHECHAMBO
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, ameshauriwa kufuata mfumo wa
uongozi uliotumiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere  wa
kutomwogopa mtu, kikundi cha watu au taasisi, kwa ajili ya kulinda
maslahi ya chama na taifa kwa ujumla.
Aidha, Dk. Magufuli ametajwa kuwa kiongozi makini mwenye mapenzi na
nchi yake na kwamba bila shaka atashinda uchaguzi mkuu wa Oktoba 25,
mwaka huu na kuiongoza Tanzania kwenye maendeleo ya uchumi wa viwanda
kama zilivyo ahadi zake kwenye kampeni.
Rajab Zonzo, ambaye ni miongoni mwa waanzilishi wa TANU na TANU Youth
League, alisema hayo jana, alipokuwa akihojiwa na mwandishi  wa habari
hii, jijini Dar es Salaam.
Alisema chama kimelamba dume kwa kumpa Dk. Magufuli jukumu la
kuipeperusha bendera ya urais.
Zonzo alisema Dk. Magufuli ni kiongozi makini, mwenye msimamo tangu
alipoanza kumsikia kwenye duru za siasa hapa nchini.
Alisema iwapo Dk. Magufuli ataendelea na msimamo huo, akiwa Ikulu
atumie mtindo wa Mwalimu Nyerere kwenye uongozi, ili aipeleka Tanzania
kwenye maendeleo.
Zonzo alisema siasa za sasa duniani zimeingiliwa na mdudu anayeweza
kufananishwa na kirusi, ambapo mtu mmoja anaweza kutumika kusambaza
mdudu huyo, kisha kusababisha maafa makubwa kwa jamii na taifa kwa
jumla.
Alisema mtu ambaye hatamsifu Rais Jakaya Kikwete, ana wivu usio na
maana, kwakuwa kiongozi huyo amefanya kazi kubwa kuifikisha nchi hapa
ilipo pamoja na kukivusha chama kwenye wakati mgumu.
Mwasisi huyo alisema utaratibu wa kumteua rais mtarajiwa wa awamu ya
tano na mwenyekiti wa chama, ulikuwa umeandamwa na jinamizi lililokuwa
likiwatumia baadhi ya watu ambao kwa sasa hawako ndani ya CCM baada ya
kushindwa vita ile.
“Kilichotokea Dodoma na kumpata Magufuli ilikuwa ni vita kati ya
binadamu na jinamizi, japo halikuonekana kwakuwa lilikuwa likiwatumia
watu waliokuwa wakiaminiwa na chama kuwa ni wanachama na makada makini
ambao wasingethubutu kukihujumu chama.
“Tumekuwa mashuhuda kuwa walijitokeza wazi baada ya kushindwa, lakini
sifa zote zinastahili kuelekezwa kwa Kikwete, uongozi wake makini ndio
umesababisha chama kuvuka jaribu lile,” alisema Zonzo.
Aliongeza kuwa ni laana kutumia hotuba za Mwalimu (Nyerere),
kujitafutia umaarufu na kuungwa mkono kwenye safari ya kudanganya
Watanzania, ambayo mwisho wake ni mbaya kwa mhusika na kizazi chake.
Kauli hiyo imetokana na kitendo cha Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa
kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, kutumia kipande cha hotuba ya
Mwalimu Nyerere na kudai kuwa ameifuata baada ya kukosa mabadiliko
ndani ya CCM.
Alisema Watanzania wanapaswa kutuliza akili, kuamua kwa busara na
kutokufuata mkumbo, kwa kuwa katika kizazi hiki, kuna watu wanadiriki
kutumia imani za kishirikina kutaka kukubalika na idadi kubwa ya watu
bila kujali uchafu wa mhusika na athari zake kwa taifa.
Alisema Tanzania ni nchi nzuri ambayo mataifa makubwa bado
wanaitamani,  licha ya kumalizika kwa ukoloni, hivyo wanatumia kila
njia kurudi na kuchukua vilivyosalia.

No comments:

Post a Comment