Thursday, 3 September 2015
MASSABURI AWAZIMA CHADEMA UBUNGO
NA MARIAM MZIWANDA
MGOMBEA Ubunge jimbo la Ubungo kwa tiketi ya CCM, Didas Massaburi,
amewataka CHADEMA kuacha kuweweseka kwa kuwa mparaganyiko uliopo ndani
ya chama hicho hauwezi kuwazuia wanasiasa makini kuhama na kurudi CCM.
Alisema hana muda wa kuchochea maandamano, lakini ataendelea kuwapokea
waliochoka kudhulumiwa haki zao na kurubuniwa kwa siasa za uchochezi
ndani ya CHADEMA.
Massaburi aliyasema hayo jana, jijini Dar es Salaam, alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari na kupokea wanachama wapya kutoka
CHADEMA na CUF.
Alisema zaidi ya wanachama 200 wamerudisha kadi kutoka CHADEMA na CUF
na anaendelea kuwaomba wanachama wengine kujitokeza kwa wingi pale
wanapovutiwa na sera zenye mwelekeo.
“Namuunga mkono Dk. Willibrod Slaa kwa nguvu zote ni mwanasiasa makini
anayejitambua, lakini sina muda wa kuandaa au kuchochea maandamano
nchi nzima wamuunge mkono ila nina muda wa kuendelea kupokea wanachama
wapya ndani ya CCM na haya ndio matokeo ya dhuluma wanazozifanya
CHADEMA, watu wamewachoka,” alisema.
Aliongeza kuwa laana ya ukabila na kukumbatia makapi inawaathiri
CHADEMA na kugeukana kwakuwa wanachama waliorudisha kadi waliletwa
kwake na mmoja wa diwani wa CHADEMA.
“Diwani huyo alinifuata na kusema wapo wanachama wamechoka unyanyasaji
wanamuunga mkono Dk, Slaa naomba wapokee, wanarudi CCM, nikamwambia
ahsante walete na kweli toka jana ninawapokea mamia kwa mamia, hivyo
sishituki na kujitetea kwake kwa viongozi wake na kudai kuwa nimeandaa
maandamano,”alisema.
Masaburi alisema CCM ni imara na Ubungo itarudi kwa chama hicho na
kuendelea kupambana na mafisadi kila kona.
Kwa upande wa wanachama waliorudisha kadi hizo, aliyekuwa mgombea wa
viti maalumu CHADEMA, Halima Mshamu, alisema chama hicho kwa sasa
kimepoteza mwelekeo na katu hawawezi kuendelea kuvumilia wale
walioshindwa kuthamini mchango wa Dk. Slaa.
“Wananchi wasidanganywe na Lowassa, hana cha kuwasaidia, CCM imemuacha
kwasababu ya tuhuma nyingi wampuuze,”alisema.
Kwa upande wake, mwanachama wa CUF, Mbwana Abdallah, alisema
amehangaika na chama hicho kwa muda mrefu na kushinikizwa katika
migomo mikoa mbalimbali, ikiwemo Lindi, lakini kwa sasa kutokana na
ushawishi alionao eneo la Manzese atahakikisha anatoa elimu kwa kila
mmoja kuachana na UKAWA.
Alisema UKAWA imewadhalilisha vya kutosha Lowassa ni nembo ya ufisadi
na viongozi wao hawana njia ya kumsafisha ni aibu kubwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment