Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli akiwasili kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora kwenye mkutano wa kampeni za CCM |
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Nzega mjini, Hussein Bashe, akihutubia wakazi wa mji huo waliojitokeza kwa wingi kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za CCM ambapo mgombea wa Urais kupitia CCM alihutubia |
NA SELINA WILSON, TABORA
KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ameseama mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli ni muadilifu na mzalendo mwenye nia njema ya kuwatumikia Watanzania.
Amesema Dk. Magufuli ndiye atakayewaondoa wananchi wa kawaida kutoka katika manyanyaso na changamoto na kuwewawezesha kufanya shughuli zao katika mazingira bora na unafuu zaidi.
Kinana aliyasema hayo jana wakati akizungumza na maelfu ya wakazi wa mkoa huo walifurika katika Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Alisema kwamba Mkoa wa Tabora ulikuwa na changamoto ya hospitali iliyokaa miaka mwili bila kuendelezwa kutokana na changamoto za mkandarasi, lakini yeye alitatua na sasa amepatikana Dk. Magufuli ndio dawa ya matatizo kama hayo.
“Nilikuta pia kuna ujenzi wa chuo kimoja ujenzi ulisimama mkandarasi ameng’ang’ania eneo la mradi anadai fedha zake nikalitatua. Haya yote dawa yake ni Dk. Magufuli, namfahamu ni mchapa kazi,”alisema.
Alisema kuna kero kwa wachimbaji wadogo wa madini wanasumbuliwa huku kukiwa na watu waliohodhi maeneo makubwa ambayo hayajaendelezwa.
“Nimemsikia Dk. Magufuli akisema atawanyang’anya wenye mashamba makubwa waliyoyatelekeza, sasa na hawa dawa yao ni Dk. Magufuli, mchagueni ili awe Rais awafanyie kazi,”alisema .
Kinana ambaye wakati wote alikuwa akishangiliwa na umati huo wananchi aliwanadi wagombea ubunge na udiwani wa mkoa huo huku akisisitiza kwamba Dk. Magufuli ataleta mabadiliko ya kiuchumi.
Alisema kero za wanyabiashara ndogondogo, kusumbuliwa na mgambo, polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zitamalizwa na Dk. Magufuli kwa kuwa ni mtu mwenye kupenda maendeleo ya wanyonge.
Mapema, akizungumza katika mkutano huo, Mjumbe wa Kamati ya Kampeni za CCM, Samuel Sitta, alisema CCM imeteua mgombea bora anayekubalika na ndio maana mafisadi walisusa na kutimkia UKAWA.
Sitta aliwataka wananchi wasikubali kupotoshwa na Mgombea wa UKAWA, Edward Lowassa, kwa kuwa hafai kuongoza nchi, sio msafi na hana sifa za kuwa Rais wa Tanzania.
Alisema Lowassa akiwa kijana mdogo, alikuwa na fedha nyingi na mpaka sasa hakuna mwanasiasa anayemfikia kwa kuwa na fedha nyingi ambazo hazijulikani kazipataje.
DK. JOHN MAGUFULI
“Mtu amekopeshwa amekwenda chuo kikuu amemaliza masomo yake amefaulu vizuri anakuja na cheti chake kutafuta kazi unamwambia awe na uzoefu wa miaka mitatu mpaka mitano, huo uzoefu ameupata wapi…”
Kero ya vijana wanaomaliza vyuo vikuu kukosa kazi kwa kigezo cha kutokuwa na uzoefu itakuwa historia baada ya kanuni na sheria za kazi hususan serikalini na taasisi za umma.
Mgombea Urais wa CCM, Dk. Magufuli, alitoa ahadi hiyo jana wakati akihutubia umati wa wananchi katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Mjini Tabora.
Alisema hiyo ni kero kubwa na kama ni sheria ama kanuni, akiingia madarakani serikali yake itaipitia upya ili kutoa fursa za ajira kwa sababu utaratibu huo hauna tija na unawakwaza wahitimu.
“Mtu amekopeshwa amekwenda chuo kikuu amemaliza masomo yake amefaulu vizuri anakuja na cheti chake kutafuta kazi unamwambia awe na uzoefu wa miaka mitatu mpaka mitano, huo uzoefu ameupata wapi,”alisema.
Dk. Magufuli alisema hizo ni sehemu ya kero na manyanyaso kwa wananchi wenye maisha ya chini ambapo katika serikali yake anataka kuyamaliza kabisa ili kubadilisha maisha ya Watanzania.
Akizungumzia uchumi Dk. Magufuli alisema, ameomba urais ili kuunda serikali makini itakayoangalia rasilimali za Watanzania na kuzisimamia ipasavyo ili ziwanufaishe wananchi wote.
Alisema pia ataweza mazingira mazuri kwa wawekezaji hususan wanaokuja akuwekeza kwenye viwanda na wawe wanapatiwa vibali za kuanzisha viwanda bila kuzungushwa.
Dk. Magufuli alisema pia atakuwa mkali kwa wakandarasi wazembe wanaochelewesha miradi ya wananchi ikiwemo ya umeme ambayo amepata taarifa kuna ucheleweshaji.
“Mimi ndio kiboko ya makandarasi. Nilikuwa nawasimamia makandarasi wa ujenzi wa barabara sasa nikiwa rais nitawasimamia makandarasi wa umeme, maji, ujenzi na wengine na watakaochelewesha kazi watakiona,”alisema.
Akiwa katika jimbo la Bukene, alimnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo, Seleman Zedi na kuwataka wananchi wamchague kwa kuwa ni mfuatiliaji wa maendeleo ambaye ameweza kupata mradi wa barabara ya lami kilomita 149 ndani ya jimbo lake.
Dk. Magufuli aliwaonya watendaji wa serikali wanaojilimbikizia posho kwenye maadhimisho ya sherehe ikiwemo Wiki ya Maji wakati hakuna huduma hiyo na kusisitiza kwamba ataifuta.
Katika majimbo mbalimbali mkoani Tabora, Dk. Magufuli alisisitiza dhamira ya kufuta karo shule za msingi hadi sekondari kidato cha nne, kuboresha huduma za afya, maji na umeme na kuwezesha wananchi kiuchumi.
HUSSEIN BASHE
“Dk.
Magufuli pambana na ufisadi kwa vitendo na kwa kuwa umeshatangaza utaanzisha
mahakama ya mafisadi na majizi nina imani utakomesha vitendo hivyo…”
Mgombe ubunge wa Nzega Mjini kupitia CCM, Hussein Bashe, amesema
ni muumini wa mabadiliko ndani ya CCM na ana imani yatapatikana chini ya
uongozi wa Dk. John Magufuli.
Amesema Dk. Magufuli ni mgombea bora, wakala wa mabadiliko
anayeakisi mahitaji ya sasa, yajayo na kusisitiza kwamba, atapata kura za
kishindo na kushinda uchaguzi mkuu.
Bashe alisema hayo jana wakati akitoa salamu kwa wananchi
wa Nzega Mjini katika Uwanja wa Maegesho ya Magari wakati mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, akihutubia
umati wa wananchi kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu.
Akizungumzia kuhusu kutuhumiwa kwamba atahamia UKAWA, Bashe
alisema kama mwana CCM alikuwa kwenye kundi fulani, lakini baada ya Chama
kukamilisha vikao vyake na kumpata mgombea bora ameendelea kubaki ndani ya Chama.
“Mimi na CCM hatukukutana barabarani. Mimi ni muumini wa mabadiliko
ndani ya Chama na tumempata wakala wa kutekeleza mabadiliko kwa vitendo…kwenye
uchaguzi ndani ya CCM, mimi na kaka
yangu Bulembo (Abdallah) tulikuwa kambi tofauti, lakini uchaguzi
umekwisha tunatafuta kura za CCM kwa ajili ya Dk. Magufuli na nina amini
katika wapiga 47,000 za jimbo langu zinaweza kukosekana asilimia tano, lakini
zingine zote atapata,”alisema.
Akizungumzia ufisadi, Bashe alimuomba Dk. Magufuli kupambana na na
ufisadi kwa vitendo na kwa kuwa ameshatangaza ataanzisha mahakama ya mafisadi
na majizi ana imani atakomesha vitendo hivyo.
“Dk. Magufuli nakuomba kwenye vita hii tumekuwa watu wa kusema
bila kutekeleza, tutakuwa tukihoji mara kwa mara kwa utakayemtua kuwa Waziri wa
Katiba na Sheria, Tutahoji juu ya muswada wa kuanzisha mahakama hiyo uje mapema
ili watu washughulikiwe. Taifa leti ni tajiri kuna wezi wapo bandarini na pale
upaangalie,” alisema.
Pia, aliwatahadharisha wanasiasa wanaotafuta kura kwa udini na
aliwataka watekeleze ahadi zao.
“Kuna Kanisa la Moravian hapa Nzega kuna mtu alitoa cheki
feki ya kuchangia kanisa tunahitaji aje atoe fedha alizoahidi,” alisema bila
kutaja jina la mhusika.
Katika hatua nyingine, Bashe alimuomba Dk. Magufuli
akishachaguliwa kuwa Rais, amsadie kutatua kero ya maji kwa kumpati matanki
makubwa matano na kujengewa daraja katika eneo la Mto Nobola.
Pia, aliomba serikali ya awamu ya tano iendelee kuawangalia
wafanyabiashara ndogondogo wakiwemo mama ntilie ambao wamekuwa wakinyanyaswa
kwa kufukuzwafukuzwa.
Alisema katika eneo la uwanja huo uliokuwa ukifanyika mkutano kuna
mama ntilie wanaouza chakula wamekuwa wakinyanyaswa na halmashauri yake, hivyo
aliaonya watendaji kwamba waache wafanye biashara zao bila matatizo.
Akizungumza katika mkutano huo, Dk. Magufuli alimhakikishia Bashe
kwamba serikali itatekeleza mambo yote ili mradi kuwaondolea kero wananchi.
“Naomba haya ya maji, daraja, wafanyabishara ndogondogo mniachie
nitayamaliza na nitajenga barabara za lami. Mimi ndio Magufuli kwangu ni kazi
tu,” alisema.
Dk. Magufuli alimsifu Bashe kuwa ni kijana mvumilivu ambaye mwaka
2010 alishinda kura za maoni, lakini hakuteuliwa na akabaki kuwa mwana CCM ambaye
hakuhama kwenda kokote na sasa imefika wakata atakuwa mbunge.
Aliwaomba wananchi wa Nzega waichague CCM kwa kuwa imejipanga kuleta
mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kwa kuwawezesha wananchi wa hali ya chini ili
wabadilishe maisha yao.
“Nimegombea urais na Oktoba 25, mwaka huu nikishinda, watu
wanaonyanyasa wafanyabiashara ndogo ndogo watafute pa kwenda, sitakubali
kwa kuwa hizi kero ndogo ndio zinawafanya wasijikwamue kiuchumi,”alisema.
Dk. Magufuli alisema kama eneo la stendi, halmashauri
itafute eneo lingine lipimwe kwa ajili ya kujengwa stendi na eneo la uwanja huo
litumike kwa ajili ya mama lishe na wengine.
Dk. HAMIS KIGWANG’ALA
“UKAWA
wamepoteza mwelekeo kwa kuwachukua wahandisi na wakandarasi wa ufisadi...”
Kwa upande wake mgombea ubunge wa jimbo la Nzega Vijijini, Dk.
Hamisi Kigwang’ala, ameliponda kundi la vyama vya siasa linalounda UKAWA kwamba
limepoteza mwelekeo kwa kuwachukua wahandisi na wakandarasi wa ufisadi.
Alisema kwa miaka 20, ajenda yao kubwa ilikuwa ni kupambana na
ufisadi, lakini kwa sasa ajenda yao ili kushika dola wameamua kuwatumia
mafisadi wakiamini kwamba watawafikisha kwenye lengo lao la kuingia Ikulu.
Dk. Kigwang’ala alisema hayo jana alipozungumza na wananchi wa
Nzega katika mkutano wa kampeni za uchaguzi uliofanyika katika Uwanja wa Barafu
mjini hapa.
Alisema mwaka huu CCM imemleta mgombea urais muadilifu,
mwaminifu, mchapakazi na msomi aliyebobea, Dk. Magufuli na kusababisha
wapinzani kukosa hoja na kuanza kuhangaika na mafisadi waliohama CCM.
“CCM imemsimamisha mgomnbea bora, wenzetu waliamua kuwachukua
wahandisi na makandarasi wa ufisadi. Nawaomba wana Nzega tuwe makini tuchague
kiongozi kwa kutulia,”alisema.
Dk. Kigwang’ala alisema ajenda ya upinzani haijawahi kuwa
maendeleo hata siku moja, tangu walipoanzisha vyama vyao, hivyo Watanzania
wanapaswa kuwa makini katika uchaguzi wa mwaka huu.
“Lengo lao ni kutaka kushika dola na sasa wameamua kupitia njia
yoyote hata iwe ya shetani ili mradi wafike Ikulu. Msikubali mchagueni Dk.
Magufuli hana tabia ya uongo ni muadilifu na mtekelezaji,”alisema.
Alisema ndani ya CCM wapo mafisadi wachache ambao baada ya Dk.
Magufuli kuteuliwa wamekuwa na hofu kubwa na kasi yake ya utendaji na sasa
wanatafuta pa kwenda, hivyo wananchi wamchague ili asafishe serikali na chama
na kujenga nidhamu.
ABDALLAH BULEMBO
“Tumemvumilia
sasa tumechoka, tutamchapa. Tunamtaka arudishe walinzi ili kuthibisha kwamba
hastahili kwa kuwa miaka yote 10 alikuwa analipwa bure bila kufanya kazi…”
Katika hatua nyingine, akizungumza katika mikutano ya kampeni za
uchaguzi Nzega na Tabora Mjini wakati akimnadi Dk. Magufuli, Mjumbe wa
Kamati Kuu, Abdallah Bulembo, alimtaka Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye,
arejeshe asilimia 80 ya mshahara wa waziri mkuu na walinzi.
Alisema kwa miaka 10 amekuwa waziri mkuu, kisha anasema serikali
ya CCM kwa miaka 54 haijafanya kitu, lakini mpaka sasa anaishi kwa mashahara wa
waziri mkuu ambao hakuufanyia kazi yoyote.
“Tumemvumilia sasa tumechoka, tutamchapa. Tunamtaka arudishe
walinzi ili kuthibisha kwamba hastahili kwa kuwa miaka yote 10 alikuwa analipwa
bure bila kufanya kazi,” alisema.
Bulembo alisema Sumaye ametimkia UKAWA baada ya kuona hana sifa za
kiongozi ndani ya CCM, aligombea ujumbe wa NEC, ‘akapigwa’ na Dk. Mary
Nagu.
Alisema hakuna kiongozi aliyetoka CCM kwenda upinzani kama hana
makandokando na kukosa sifa za kuwa kiongozi ndani ya Chama.
Bulembo pia alimshangaa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ambaye ameanza kulalamika kwamba wataibiwa
kura wakati wao na mgombea wao, Edward Lowassa, wanapita angani Dk. Magufuli
anapita chini.
“Wapiga kura wako angani au chini anakopita Dk. Magufuli,” alihoji
Bulembo huku akijibiwa na umati wa wananchi wa Tabora Mjini waliofurika Uwanja
wa Ally Hassan Mwinyi.
Alisema CCM imeshafanya kampeni kwenye mikoa 23, Dk Magufuli
ameshakwenda mikoa 12 na Mgombea Mwenza Samia Suluhu Hassan, ameshapita mikoa
11.
Bulembo ambaye ndiye kiongozi wa msafara wa kampeni wa Dk.
Magufuli alisema mpaka sasa Dk. Magufuli alishafanya mikutano mikubwa ya
hadhara 98 na mikutano isiyo rasimi 300.
Kwa upande wa Samia ameshafanya mikutano rasmi 65 na mikutano
isiyo rasmi 200. Alisema kwa kuwa wapiga kura wapo chini, Oktoba 25 kwenye uchaguzi mkuu lazima wachapwe
tu na CCM itashinda.
No comments:
Post a Comment