Wednesday, 16 September 2015
'WAGOMBEA WA UPINZANI WATAANDIKA HISTORIA MPYA'
Na Mwantanga Ame, Pemba
MWENYEKITI wa Kamati ya Kampeni za CCM Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema wagombea wa upinzani wajiandae kuingia katika vitabu vya rekodi ya historia ya maajabu ya dunia kwani, watashindwa vibaya na wagombea wa CCM.
Balozi Iddi, ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alisema hayo jana wakati akihutubia wanachama na wapenzi wa CCM, baada ya kufungua maskani ya Balozi Seif Ali Iddi, katika kijiji cha Chakweni, mkoa wa Kusini Pemba.
Alisema ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao hauna wasiwasi na waliojitokeza kushindana na Chama, wajiandae kuingia katika historia ya maajabu ya dunia ya kushindwa Zanzibar na Tanzania nzima.
Alisema inashangaza kuona baadhi ya viongozi wa vyama hivyo wanaendelea kusimamisha wagombea wa urais, ambao tayari wana rekodi ya kushindwa katika uchaguzi uliopita, jambo ambalo ni ndoto kwa mwaka huu kutokea miujiza ya kuishinda CCM.
Alisema hiyo ni kutokana na historia yake, ambapo tayari mgombea wa CUF, alishashiriki katika uchaguzi tangu mwaka 2005, lakini ameshindwa.
Alisema hata katika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu, mgombea huyo hawezi kufanya miujiza yoyote ya kuishinda CCM kwa vile ameshakuwa dhaifu kama kilivyo chama chake.
Balozi Seif alisema hiyo ni kutokana na vyama hivyo kushindwa kuwa na wagombea imara wa kushindana na CCM kwani, tayari hivi sasa vimesimamisha wagombea wa mkopo kutoka vyama vingine, ambao sera zao zimeanza kuonekana hazina mvuto kwa wanaowaunga mkono kiasi ambacho imesababisha baadhi yao kuvihama vyama hivyo.
Balozi Seif alisema hashangai kuona hivi sasa kuna wanachama wa CCM, Kisiwani Pemba, wameamua kukihama chama hicho na kujiunga na CCM, kwa vile tayari wamebaini vyama vya upinzani vinawadanganya.
Alisema wamebaini hivyo baada ya kuona kuwa huduma za maji, barabara, umeme na ustawi wa jamii, zimekuwa zikiletwa na CCM.
Kutokana na hali hiyo, Balozi Seif alisema vyama vilivyoingia katika ushindani huo, vinapaswa kujiandaa kushuhudia vifo vyao, kwani vingi vitakufa baada ya uchaguzi mkuu ujao.
Alisema wakati umefika kwa wananchi wa Pemba kuwaunga mkono wagombea wa CCM kwa nafasi zote kwa kuwapa kura kwani wana dhamira ya kuwasaidia.
Balozi Seif aliwaahidi vijana hao kuwa atawapatia mashine na boti huku Mke wa Makamu wa Pili wa Rais, Mama Asha Suleiman Iddi, akiahidi kuwaimarishia maskani yao kwa kuizeka kwa mabati badala ya makuti.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment