Wednesday, 16 September 2015

CCM YAPANIA KULIREJESHA JIMBO LA MBEYA MJINI



NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA

JUMUIA ya Wazazi ya CCM mkoa wa Mbeya, imesema imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha jimbo la Mbeya Mjini, linarudi chini ya miliki ya Chama.

Hatua ya kulirudisha jimbo chini ya CCM, kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, kutalifanya jiji kupiga mbele hatua za maendeleo, tofauti na ilivyo sasa ambapo siasa za majitaka, zinazoendeshwa na CHADEMA, zikiambatana na maandamo, vurugu na uchomaji moto barabara za lami, zimekuwa kikwazo.

Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Jumuia ya Wazazi mkoani Mbeya, Fadhir Mrami, wakati akizungumza na makatibu wa jumuia hiyo, makatibu elimu kata na makatibu wa matawi kutoka kata zote za mjini Mbeya.

Jumla ya viongozi 202 walihudhuria kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, ulioko kwenye shule ya sekondari ya Sangu.

Mrami alisema tangu jimbo hili liwe chini ya mbunge Joseph Mbilinyi, kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, maendeleo yamesimama kwani wananchi wamekuwa wakiaminishwa zaidi katika kushiriki kufanya maandamano na vurugu zisizo na msingi, hali inayosababisha maendeleo kurudi nyuma zaidi.

Alisema lengo la jumuia hiyo kuwaandalia kikao hicho viongozi wake ngazi ya kata, ni kuwapa elimu ya jinsi ya kufanya kampeni zenye lengo la kukiletea ushindi Chama wilaya ya Mbeya Mjini, ndani ya kata zao, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mgombea wa CCM, Sambwee Shitambala, anashinda na kuwa mbunge wa jimbo hilo.

"Wazazi tunaahidi kuipatia CCM ushindi mkubwa Mbeya Mjini kwani tumejipanga kikamilifu kuhakikisha jimbo hili linarudi chini ya miliki ya CCM. Kinachotakiwa ni nyie viongozi wote wa jumuia ngazi ya kata, kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake kikamilifu," alisema Mrami.

Aliongeza kuwa jumuia hiyo inalaani vikali vitendo vinavyofanywa na viongozi pamoja na wanachama wa CHADEMA, kubandua na kuharibu mabango ya mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, mgombea ubunge, Shitambala na zile za wagombea udiwani.

Mrami alisema tatizo hilo linachangiwa pia na baadhi ya wafanyabiashara mjini Mbeya, kuihujumu CCM.

Alisema kwa vile tayari wamezibaini changamoto hizo mapema, watahakikisha wanazifanyia kazi haraka iwezekanavyo ili kukiwekea Chama mazingira mazuri ya ushindi.

Kwa mujibu wa Mrami, viongozi hao wa jumuia ngazi ya kata katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, wanatakiwa kuendelea na kazi ya kuwahimiza wananchi kuvitunza vizuri vitambulisho vyao vya kupigiakura ili waweze kuitumia haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi bora, watakaoshirikiana nao katika kuleta maendeleo ya kweli.

"Pia mnatakiwa kuhakikisha wazee wa jinsia zote mbili, yaani wanaume na wanawake, wanahimizwa kuwahi mapema kwenye vituo vya kupigiakura siku ya Oktoba 25, mwaka huu, ili waweze kushiriki kupigakura," alisema Mrami.

Aliwaagiza viongozi hao kuhakikisha mawakala watakaoteuliwa kusimamia zoezi la kuhesabu kura, wawe ni watu makini, wenye uelewa mkubwa ili kuepukana na hujuma zinazoweza kuletwa na wapinzani.

No comments:

Post a Comment