Wednesday, 16 September 2015
MGOMBEA UBUNGE AAHIDI KUDHAMINI UKOPESHWAJI PIKIPIKI
Na Nathaniel Limu, Singida
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Singida Mjini kupitia CCM, Mwalimu Mussa Sima, ameahidi endapo wananchi watampa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao bungeni, atatumia ubunge wake kudhamini vijana wakopeshwe pikipiki ili waweze kuanzisha biashara ya kusafirisha abiria (bodaboda) kwa lengo la kujipatia kipato.
Mwalimu Sima, alitoa ahadi hiyo juzi, wakati akiomba kura kwenye mkutano wa kampeni, uliofanyika katika mtaa wa Nyanza, kata ya Kindai mjini hapa.
Alisema uamuzi wake huo unalenga kupunguza tatizo kubwa la uhaba wa ajira kwa vijana wa jimbo hilo.
“Nitashirikiana na mamlaka zinazohusika kubaini vijana makini, waadilifu na wanaojituma. Hawa nitahakikisha natumia ubunge wangu kuwadhamini kwenye maduka yanayouza pikipiki wakopeshwe, na nina uhakika ndani ya miezi sita, watakuwa wamemaliza madeni yao na pikipiki zitakuwa mali zao kihalali”,alifafanua.
Aidha, Mwalimu Sima aliwataka kina mama na vijana kujiunga na vikundi vya ujasiriamali na kuvisajili kisheria, ili kujijengea mazingira mazuri ya kufaidika na shilingi milioni 50, zitakazotolewa kwa kila kijiji nchini, zilizobainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Akifafanua, alisema kabla ya kukopeshwa fedha hizo, ofisi yake ya ubunge itahakikisha vikundi hivyo vya ujasiriamali vinapata mafunzo, ili kuwajengea uwezo wa kujiingizia kipato kwa ufanisi zaidi.
Katika hatua nyingine, mgombea huyo wa nafasi ya ubunge, alitaja baadhi ya vipaumbele vyake atakavyoanza navyo kuwa ni pamoja na kuhakikisha kila shule ya sekondari inakuwa na huduma ya mtandao wa internet.
“Lengo la kila shule ya sekondari kuwa na mtandao wa internet, ni wanafunzi kupata fursa zaidi ya kujisomea, ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao. Pia nitahakikisha jimbo letu linakuwa na shule za sekondari za kidato cha tano na sita, zitakazokidhi mahitaji ya jimbo letu,” alisema.
Kwa upande wa afya, Mwalimu Mussa alisema ataelekeza nguvu zake kutekeleza Ilani ya Uchaguzi, ambayo imebainisha ujenzi wa zahanati kwa kila kijiji na vituo vya afya kwa kila tarafa.
Awali, Meneja kampeni wa CCM katika jimbo hilo, Mosses Ikaku, aliwaomba wakazi wa kata ya Kibaoni na zinginezo za jimbo hilo, kuchagua rais, wabunge na madiwani kutoka CCM.
“Nawaomba sana ndugu zangu msidanganywe na wasanii ambao wanasubiri kipindi cha uchaguzi, ndio wanafanya usanii kwa kupanda bodaboda, eti kujua kero za Watanzania.Chagueni wagombea kutoka CCM, Chama pekee chenye ilani inayoonyesha wazi kitawaletea maendeleo ya kweli Watanzania,"alisema Ikaku.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment