NA SELINA WILSON, NZEGA
MGOMBEA ubunge wa CCM Jimbo la Nzega Mjini, Husein Bashe, amesema
yeye ni muumini wa mabadiliko ndani ya CCM na ana imani kuwa yatapatikana chini
ya uongozi wa Dk. John Magufuli.
Amesema Dk. Magufuli ni mgombea bora, wakala wa mabadiliko
anayeakisi mahitaji ya sasa yajayo na kusisitiza kwamba, atapata kura za
kishindo na kushinda uchaguzi mkuu.
Bashe alisema hayo jana akitoa salamu kwa wananchi wa Jimbo
la Nzega Mjini katika uwanja wa Maegesho ya magari katika Mgombea urais wa CCM,
Dk. John Magufuli kuhutubia umati wa wananchi kwenye mkutano wa kampeni za
uchaguzi mkuu.
Akizungumzia kuhusu kutuhumiwa kwamba atahamia Ukawa, Bashe
alisema kwamba kama mwana CCM alikuwa kwenye kundi fulani lakini baada ya chama
kukamilisha vikao vyake na kumpata mgombea bora ameendelea kubaki ndani ya
chama .
“Mimi na CCM hatukutana barabarani. Mimi ni muumini wa mabadiliko
ndani ya chama na tumempata wakala wa kutekeleza mabadiliko kwa vitendo,
“Kwenye uchjaguzi ndani ya CCM mimi na kaka yangu Bulembo tulikuwa
kambi tofauti lakini uchaguzi umekwisha tunatafuta kura za CCM kwa ajili
ya Dk. Magufuli na ninaamini katika wapiga 47,000 za jimbo lake zinaweza
kukosekana asilimia tano lakini zingine zote atapata,”alisema.
Akizungumzia ufisadi, Bashe alimuomba Dk. Magufuli kupambana na na
ufisadi kwa vitendo na kwa kuwa ameshatangaza kwamba ataanzisha mahakama ya
mafisadi na majizi ana imani atakomesha vitendo hivyo.
“Ndugu Magufuli nakuomba kwenye vita hii tumekuwa watu wa kusema bila
kutekeleza, tutakuwa tukihoji mara kwa mara kwa utakayemtua kuwa waziri wa
katiba na sheria,
Tutahoji juu ya muswada wa kuanzisha mahakama hiyo uje mapema ili
watu washughulikiwe. Taifa leti ni tajiri kuna wezi wapo bandarini na pale
upaangalie,” alisema.
Bashe pia aliwatahadharisha wanasiasa wanatafuta kura kwa udini na
aliwataka watekeleze ahadi zao.
“Kuna kanisa la Moravian hapa Nzega kuna mtu alitoa cheki
feki ya kuchangia kanisa tunahitaji aje atoe fedha alizoahidi,” alisema bila
kutaja jina la mhusika.
Katika hatua nyingine, Bashe alimuomba Dk. Magufuli
akishachaguliwa kuwa Rais, amsadie kutatua kero ya maji kwa kumpati matanki
makubwa matano na kujengewa daraja katika eneo la Mto Nobola.
Pia aliomba serikali ya awamu ya tano iendelee kuawangalia wafanyabiashara
ndogondogo wakiwemo mama ntilie ambao wamekuwa wakinyanyaswa kwa
kufukuzwafukuzwa.
Alisema katika eneo la uwanja huo uliokuwa ukifanyika mkutano kuna
mama ntilie wanaouza chakula wamekuwa wakinyanyaswa na halmashauri yake hivyo,
aliaonya watendaji kwamba waache wafanye biashara zao bila matatizo.
Akizungumza katika mkutano huo Dk. Magufuli alimuhakikishia Bashe
kwamba, serikali itatekeleza mambo yote ili mradi kuwaondolea kero wananchi.
“Naomba haya ya maji, daraja, wafanyabishara ndogondogo mniachie
nitayamaliza na nitajenga barabara za lami. Mimi ndio Magufuli kwangu ni kazi
tu,” alisema.
Dk. Magufuli alimsifu Bashe kuwa ni kijana mvumilivu ambaye mwaka
2010 alishinda kura za maoni lakini hakuteuliwa na akabaki kuwa mwana CCM
hakuhama kwenda kokote na sasa imefika wakata atakuwa mbunge.
Aliwaomba wananchi wa Nzega waichague CCM kwa kuwa imejipanga
kuelata mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kwa kuwawezesha wananchi wa hali ya
chini ili wabadilishe maisha yao.
“Mimi nimeshagombea urais na Oktoba 25, mwaka huu, nikishashinda
watu wanaonyanyasa wafanyabiashara ndogondogo watafute pa kwenda,
sitakubali kwa kuwa hizi kero ndogo ndio zinawafanya wasijikwamue
kiuchumi,”alisema.
Dk. Magufuli alisema kama eneo la stendi, halmashauri
itafute eneo lingine lipimwe kwa ajili ya kujengwa stendi na eneo la uwanja huo
litumike kwa ajili ya mama lishe na wengine.
Dk. Kingwangala
Kwa upande wake Mgombea ubunge wa CCM jimbo la Nzega Vijijini, Dk.
Hamisi Kingwangala, ameliponda kundi la vyama vya siasa linalounda Ukawa,
kwamba wamepoteza mwelekeo kwa kuwachukua wahandisi na wakandarasi wa ufisadi.
Amesema kwa miaka 20 ajenda yao kukubwa ilikuwa ni kupambana na
ufisadi, lakini kwa sasa ajenda yao ni kushika dola wameamua kuwatumia mafisadi
wakiamini kwamba watawafikisha kwenye lengo lao la kuingia ikulu.
Dk. Kingwangala alisema hayo jana alipozungumza na wananchi wa
Nzega katika mkutano wa kampeni za uchaguzi uliofanyika katika uwanja wa Barafu
mjini hapa.
Alisema mwaka huu CCM imemleta Mgombea urais muadilifu,
mwaminifu, mchapakazi na msomi aliyebobea, Dk. John Magufuli na kusababisha
wapinzani kukosa hoja na kuanza kuhangaika mafisadi waliohama CCM.
“CCM imemsimamisha mgomnbea bora wenzetu waliamua kuwachukua
wahandisi na makandarasi wa ufisadi. Nawaomba wana Nzega tuwe makini tuchague
kiongozi kwa kutulia,”alisema.
Dk. Kingwangala alisema ajenda ya upinzani haijawahi kuwa
maendeleo hata siku moja tangu walipoanzisha vyama vyao hivyo Watanzania
wanapaswa kuwa makini katika uchaguzi wa mwaka huu.
“Lengo lao ni kutaka kushika dola na sasa wameamua kupitia njia
yoyote hata iweze ya shetani ili mradi wafike Ikulu. Msikubali mchagueni Dk.
Magufuli hana tabia ya uongo ni muadilifu na mtekelezaji,”alisema.
Alisema ndani ya CCM wapo mafisadi wachache ambao baada ya Dk.
Magufuli kuteuli wamekuwa na hofu kubwa na kasi yake ya utendaji na sasa
wanatafuta pa kwenda, hivyo wananchi wamchague ili asafishe serikali na chama
na kujenga nidhamu.
Bulembo
Katika hatua nyingine akizungumza katika mikutano ya kampeni za
uchaguzi Nzega na Tabora Mjini wakati akimnadi Dk. Magufuli, Mjumbe wa
Kamati Kuu, Abdallah Bulembo, alimtaka Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye,
arejeshe asilimia 80 ya mshahara wa waziri mkuu na walinzi.
Alisema kwa miaka 10 amekuwa waziri mkuu anasema serikali ya CCM
kwa miaka 54 haijafanya kitu, lakini mpaka sasa anaishi kwa mashahara wa waziri
mkuu ambao hakuufanyia kazi yoyote.
“Tumemvumilia sasa tumechoka, tutamchapa. Tunamtaka arudishe
walinzi ili kuthibisha kwamba hastahili kwa kuwa miaka yote 10 alikuwa analipwa
bure bila kufanya kazi,” alisema.
Bulembo alisema Sumaye ametimkia ukawa baada ya kuona hana siafa
za kiongozi ndani ya CCM, aligombea ujumbe wa NEC, ‘akapigwa’ na Dk. Mary
Nagu.
Alisema hakuna kiongozi aliyetoka CCM kwenda upinzani kama hana
makandomakando na kukosa sifa za kuwa kiongozi ndani ya Chama.
Bulembo alisema pia anamshangaa Freeman Mbowe ambaye ameanza
kulalamika kwamba wataibiwa kura wakati wao na Mgombea wao Edward Lowassa
wanapita angani Dk. Magufuli anapita chini.
“Wapiga kura wako angani au chini anakopita Dk. Magufuli,” alihoji
Bulembo huku ajijibiwa na umati wa wananchi wa Tabora Mjini waliofurika uwanja
wa Allya Hassan Mwinyi.
Alisema CCM imeshafanya kampeni kwenye mikoa 23, Dk Magufuli
ameshakwenda mikoa 12 na Mgombea mwenza Samia Suluhu Hassan, ameshapita mikoa
11.
Bulembo ambaye ndiye kiongozi wa msafara wa kampeni wa Dk.
Magufuli alisema mpaka sasa Dk Magufuli ameshafanya mikutano mikubwa ya hadhara
98 na mikutano isiyo rasimi 300.
Kwa upande wa Samia ameshafanya mikutano rasmi 65 na mikutano
isiyo rasmi 200. Alisema kwa kuwa wapiga kura wapo chini Oktoba 25 kwenye
uchaguzi mkuu lazima wachapwe tu na CCM itashinda.
No comments:
Post a Comment