Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,kupitia CCM Dk. John Magufuli akiwahutubia wakazi wa mji wa Kaliua katika Uwanja wa Kolimba |
Wakazi wa mji wa Kaliua wakimsikiliza Mgombea urais wa CCM, Dk. Magufuli alipokuwa akiwahutubia |
Mgombea Urais wa CCM Dkt Magufuli akimkabidhi Ilani ya CCM mgombea ubunge wa jimbo la Kaliua, Profesa Juma Kapuya |
Mgombea urais wa CCM, Dk Magufuli akisalimiana na mgombea ubunge wa jimbo la Urambo,.Margareth Sitta. Kulia kwake ni mbunge wa zamani wa jimbo hilo,.Samwel Sitta. |
NA SELINA WILSON, URAMBO
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John
Magufuli, amezidi kuchanja mbuga huku akiahidi utendaji kazi uliotukuka kwa
maendeleo ya haraka ya Watanzania.
Akionekana tofauti na wagombea wengine,
akiwemo Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond na anayelalamikiwa kwa
kushindwa kukata kiu ya wananchi kwa kuhutubia dakika sita hadi tatu, Edward
Lowassa, Dk. Magufuli amekuwa kivutio kikubwa kwenye mikutano yake.
Jana, alitua Urambo huku akiendelea na
utaratibu wake wa kutumia barabara, ambaapo alihutubia mkutano wa hadhara na
kuahidi kujenga kilometa sita za barabara ya lami katika mji wa Urambo.
Alisema pia ataharakisha ujenzi wa
barabara ya lami ya Kaliua/ Urambo unakamilika haraka ili kufungua fursa za
kiuchumi kwa kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao.
Dk. Magufuli alisema serikali yake ya
awamu ya tano itaendelea kuunganisha wilaya na mikoa kwa lami ili wananchi wawe
na uwezo wa kusafirisha bidhaa zao kwenda maeneo mbalimbali hadi nje ya nchi.
Alisema anatambua tatizo kubwa la
Urambo, hivyo atahakikisha wanajenga mabwawa makubwa na kuhifadhi maji na
kuyasukuma kwenda kwa wananchi.
“Tunajenga madaraja kuzuia maji,
tutatumia magreda kuchimba mabwawa na kuelekeza maji kutoka kwenye madaraja
hayo na kutengeneza miundombinu ya kuyatunza na kuyafikisha kwa
wananchi,”alisema.
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli
alisema kwamba ataziba mianya ya fedha zinazovuja na kuchotwa na wajanja
wachache wanaokwamisha maendeleo ya wananchi.
“Nitatumia jina langu la Magufuli
kuwadhibiti watu hao na kuzitumia fedha hizo kuboresha elimu na kuanzia mwakani
wanafunzi kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne hawatalipa karo,” alisema.
Alisema pamoja na kufuta karo,
serikali yake pia itaangalia suala la michango ili kuliondoa wanafunzi wasome bila kusumbuliwa kwa kuwa
anataka kujenga Taifa la wasomi.
Dk. Magufuli alisema akichaguliwa,
atakuwa Rais wa vyama vyote, makabila yote, dini zote kwa kuwa anajua mahitaji
ya Watanzani sio vyama bali ni mtu wa kuwafanyia kazi.
Kuhusu kodi alisema ataweka utaratibu
mzuri wa ukusanyaji wa kodi ambao kwa sasa unawalenga wanyonge wakiwemo
wafanyabiashara ndondogo na wafanyakazi ambao wamekuwa wakibeba mzigo mkubwa.
Alisema akiingia Ikulu, atapunguza
makato ya kodi kwa wafanyakazi kutoka asilimia 11 ili ibakie tarakimu moja na
kwa wafanyabiashara ndogondogo hatokubali wabanwe na kodi za hovyo hovyo, badala
yake wafanyabiashara wakubwa ndio walipe kodi.
Dk. Magufuli aliwaponda wanasiasa
wanaofanya kampeni kwa kuwaahidi Watanzania mambo ya uongo, jambo ambalo
alisema ni dharau kubwa ambayo dawa yake ni kuwanyima kura.
Aliwaomba wananchi wa Urambo wamchague
Magreth Sitta kwa kuwa ni mtu anayemfahamu vyema.
“Ni mchapakazi, ni mwana mama mahiri,
ni mwalimu na mimi mwalimu pia ni jasiri,
Nimesoma naye Chuo Kikuu,
ninamfahamu Magreth. Ninaomba kwa heshima kubwa mniletee huyu. Namkabidhi Ilani
ya Uchaguzi ili yote yanayotakiwa kutekelezwa ndani ya Ilani ayasimamie
huyu,”alisema.
Akizungumza katika mkutano huo,
Magreth aliwaomba wana Urambo wamchague Dk. Magufuli kwa kuwa anayatambua
matatizo ya zao la tumbaku, hivyo akiwa rais atayamaliza.
Bulembo
Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi Taifa,
Abdalla Bulembo, aliwataka wananchi wa Urambo wamchague Dk. Magufuli kwa kuwa
ni mtoto wa masikini, aliyepitia maisha ya kawaida na anazijua shida za Watanzania.
“Hatuwezi kupeleka Ikulu wapiga dili. Msichague CCM B, chagueni
viongozi mliowazoea. Msihangaike na mtu ambaye hata hawezi kushika kalamu
kuandika,”alisema.
Mpanju
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya
Kampeni, Amon Mpanju, aliwataka wananchi wa jimbo hilo wamchague Magreth kwa
kuwa ni kiongozi anayejali makundi ya watu mbalimbali wenye ulemavu.
Alisema wasikubali kupotoshwa na
wapinzani ambao mgombea wao, Edward Lowassa, amekuwa akihubiri udini kwa
kuwataka Walutheri wamchague yeye kwa kuwa ni mwenzao.
Kabla ya kwenda Urambo, Dk. Magufuli
alifanya mkutano katika jimbo la Kaliua na kumnadi mgombea ubunge wa jimbo
hilo, Profesa Juma Kapuya, akisisitiza kwamba ni mchapa kazi hodari.
Aliwaahidi wananchi wa jimbo hilo
kwamba anajua changamoto za jimbo hilo kuwa ni maji na miundombinu ya barabara
na kwamba hilo ni eneo lake, hawezi kushindwa hivyo wampe kura awatumikie.
Katika mikutano yake katika kila
jimbo, Dk. Magufuli amekuwa akipokea wanachama kutoka vyama vya upinzani, ambao
wamekuwa wakirudisha kadi za vyama vya CUF na CHADEMA, baada ya kuchoshwa
na siasa za hovyo.
Miongoni mwa wanachama hao ni viongozi
waandamizi wa CHADEMA, wakiwemo wenyeviti na makatibu wa wilaya, ambao walisema
kwamba wameamua kurudi CCM kutokana na kukerwa na mtindo wa kukataa wagombea na
kusimamisha ‘makapi’ kutoka CCM.
Akizungumza katika moja ya mikutano
hiyo, aliyekuwa Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Urambo, Obeid Obeid alisema
ameamua kutoka ili awe huru kwa kuwa CHADEMA kuna mambo mabaya yanakera ikiwemo
kuuza chama.
Obeid alisema Dk. Magufuli anatosha
kuwa Rais wa Tanzania na wagombea wa vyama vingine ni makapi, hawana sifa ya
kuongoza nchi.
Alisema Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman
Mbowe anachukua ruzuku sh. milioni 334, lakini anashindwa kuwezesha ofisi
na hivi karibuni ofisi yao walitolewa vyombo nje kutokana na kukosa kodi.
No comments:
Post a Comment