Wednesday, 18 November 2015

MAGUFULI AWASILI DODOMA KWA GARI, JINA LA WAZIRI MKUU KUTANGAZWA KESHO BUNGENI

RAIS John Magufuli akisalimiana na Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa, alipowasili Ikulu Ndogo iliyoko Chamwino jana

RAIS Dk. John Magufuli amewasili mjini Dodoma jana, huku akiwa na siri nzito ya jina la Waziri Mkuu ambalo anatarajia kuliwasilisha bungeni kesho.

Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Bunge iliyotolewa wiki iliyopita, jina la Waziri Mkuu litawasilishwa kesho na Rais Magufuli kwa Spika Job Ndugai.

Baada ya kuwasilisha jina hilo, litasomwa mbele ya wabunge wote na kuthibitishwa, kisha watapiga kura ya kumchagua.

Baada ya kuthibitishwa kwa Waziri Mkuu, siku hiyo hiyo Naibu Spika atachaguliwa na kula kiapo cha uaminifu, na baada ya hapo wabunge watajiweka tayari kwa hotuba ya kwanza ya Rais Magufuli, itakayotolewa keshokutwa saa kumi jioni.

Baada ya Rais Magufuli kumaliza kuhutubia Bunge, litaahirishwa na Waziri Mkuu hadi tarehe itakayotajwa.

Dk. Magufuli aliwasili mkoani Dodoma akitumia usafiri wa njia ya barabara kitendo ambacho ni nadra kufanywa na viongozi wakubwa wa taifa hili.

Itakumbukwa hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu, Dk. Magufuli alitumia usafiri wa barabara kupiga kampeni nchi nzima karibu miezi miwili.

Hali hiyo, ni tofauti na watangulizi wake, ambao kwa nyakati tofauti za kampeni mwaka 2005 na 2010 walitumia usafiri wa helikopta (Chopa) kuzunguka nchi nzima.

Watanzania wengi wanaamini Waziri Mkuu ajaye atatoa picha kamili ya mwelekeo wa Rais Magufuli katika suala zima la utendaji kazi wa kila siku wa Serikali yake yenye kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi tu’.

Viongozi waliowahi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu ni pamoja na Mwalimu Julius Nyerere (1961-1962), Rashid Kawawa (1962 na 1972-1977) na Edward Sokoine (1977-1980, 1983-1984) ambao wote ni marehemu.

Wengine ni Cleopa Msuya (1980-1983, 1994-1995), Dk. Salim Ahmed Salim (1984-1985), Joseph Sinde Warioba (1985-1990), John Malecela (1990-1994), Frederick Sumaye (1995-2005), Edward Lowassa (2005-2008) na Mizengo Pinda (2008-2015).

No comments:

Post a Comment