NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imetiliana saini na
Kampuni ya Quality Group Limited (QGL), mkataba wa ujenzi wa mji wa kisasa katika
eneo la Hoteli ya Bwawani mjini Unguja.
Uamuzi huo wa ujenzi wa mradi mkubwa wa uwekezaji na wa
kwanza katika historia ya Zanzibar, unalenga kuinua fursa za ajira, kukuza
utalii na uchumi kwa kasi.
Mradi huo ambao utatekelezwa kwa awamu mbili, unatarajiwa
kugharimu zaidi ya sh. bilioni 500, ambapo utatoa fursa za ajira kwa Wazanzibar
zaidi ya 15,000.
Akizungumza wakati wa kutiliana saini mkataba huo,
Mwenyekiti wa Kampuni ya QGL, Yusuf Manji, alisema ameamua kufanya uwekezaji
huo mkubwa ili kusaidia juhudi za serikali kukuza uchumi na utalii visiwani
humo. Mji huo utajulikana kama Stone Town Village.
Alisema mradi huo utahusisha uboreshaji wa Hoteli ya
Bwawani, ambayo itakuwa chini ya usimamizi wa QGL, ujenzi wa nyumba za kisasa
380 na maduka makubwa ya bidhaa mbalimbali.
Pia, utahusisha sehemu ya maegesho ya magari na michezo
ya watoto, masoko kwa ajili ya shughuli za wazawa na wageni na huduma zote za
kijamii, ikiwemo hospitali ya kisasa yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 250.
Manji, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, alisema
mbali na huduma hizo, pia mradi huo utahusisha ujenzi wa barabara na uzalishaji
umeme wa kutosha kwa ajili ya kuhudumia eneo hilo na maeneo ya jirani.
“Zanzibar ni sehemu ya Tanzania na hapa ndipo baba yangu
(Mzee Mehbub Manji) alikozaliwa, hivyo nina historia napo nzuri sana. Tunafanya
uwekezaji huu mkubwa ili kukuza uchumi na utalii wetu. Hakuna sababu ya watu
kwenda Malaysia wakati Zanzibar kuna kila kitu,” alisema Manji.
Aliongeza kuwa mradi huo utaanza utekelezaji wake hivi
karibuni kwa kuwatumia wakandarasi wa nje na wazawa, ambao watahusika kwenye
hatua mbalimbali na utazingatia sheria zote ikiwemo uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji
ya Uwekezaji na Vitega Uchumi Zanzibar (ZIFA), Salum Nassoro, alisema mradi huo
ni wa kihistoria na utasaidia kuongeza kufungua fursa visiwani hapa.
Alisema mbali na kukuza uchumi na kuvutia watalii zaidi,
mradi wa Stone Town Village, utaongeza mapato ya serikali na kuitangaza zaidi Zanzibar
ulimwenguni kote.
Kuhusu Hoteli ya Bwawani, Nassoro alisema itakarabatiwa
na kuwa katika kiwango cha nyota tano na kwamba, taswira yake itaendelea
kutunzwa kwa ajili kumbukumbu ya kipekee ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh
Amri Abeid Karume.
Aliongeza kuwa mradi wa ujenzi wa Stone Town Village
utatekelezwa kwa mujibu wa sheria na hautaathiri mandhari ya Mji Mkongwe.
No comments:
Post a Comment