Wednesday, 18 November 2015

UVCCM YATAKA WASALITI WA MAPINDUZI WANG'OLEWE




UMOJA wa Vijana wa CCM (UVCCM) umeishauri CCM kuwachukulia hatua za kinidhamu viongozi au wanachama wasaliti wa Mapinduzi ya Zanzibar, waliokihujumu Chama katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

Umesema kuendelea kubaki na wanachama hao ndani ya CCM, ni sawa na kukubali kufuga ugonjwa utakaokuja kusababisha kilio.

Ushauri huo umetolewa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, katika mkutano wake na vijana wa CCM, uliofanyika Wilaya ya Micheweni, mkoa wa Kaskazini Pemba.
Shaka alisema wapo baadhi ya viongozi wastaafu wameanza pole pole kukisaliti Chama huku baadhi yao wakishirikiana na upinzani kwa lengo la kuwasaidia washike madaraka ili  CCM ikose na kupoteza majimbo Tanzanaia Bara na Zanzibar .

"Ni heri tukabaki wanachama na viongozi  wachache wenye moyo, mshikamano, upendo, umoja na uzalendo, kuliko kuwa na kundi kubwa la  wasaliti na wenye kupanga njama na hujuma Chama, "alisema Shaka.

Alisema umefika wakati kwa Chama kupitisha fagio la chuma na kuanza kuwabaini wanachama wakorifi na mamluki,  ili kuwachukulia hatua bila kuwaonea muhali, wakiwemo na viongozi wastaafu, ambao wana ndimi mbili na wenye upekepeke kwa ajili ya kulinda maslahi yao binafsi .

Kaimu Katibu mkuu huyo alisema, UVCCM inahuzunishwa na vitendo, matamshi na mienendo ya baadhi viongzi wastaafu wa kisiasa na kiserikali, ambao hawataki hata kulitaja neno Mapinduzi katila vinywa vyao.

"Kama yuko kiongozi au mwanachama wetu ameamua kutupinga , kutusaliti au kutuhujumu na kutukwamisha, haitakuwa uchuro wowote ikiwa  atakipinga Chama akiwa nje ya CCM," alisisitiza Shaka.

Aidha, alisema kizazi kipya cha vijana wa CCM kilichotokana na vyama vya  ASP na TANU, kamwe hakitakubali kushiriki usaliti, hujuma au umamluki wa kuviza Mapinduzi na Uhuru uliosumbukiwa na wazee kwa jasho, sharubu na mateso.

Shaka alisema hakuna haja ya kuanza kutafuta wachawi nje ya chama, wakati ndani wamejazana makuhani na magwiji wa uongo, usaliti na hujuma.

"Wazee wetu walifungua milango ya uhuru na mapinduzi kwa nia njema ili kuleta usawa, haki na umoja. Milango hiyo imeingiza kila aina ya wadudu, ndege, nyoka na twiga, sasa ni wakati wa kuisafisha nyumba yetu," alisema.
 
Akizungumzia kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar, Shaka alisema uchaguzi huo umevurugwa kutokana na kupangwaa hadaa, ghiliba na ujanja ili washike madaraka ya Zanzibar.

Shaka alisema uchaguzi huo utarudiwa kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya Zanzibar na kuongeza kuwa, anaamini upinzani utaaibika na utachekwa kuanzia mitaani hadi sokoni.

No comments:

Post a Comment