Wednesday, 25 November 2015

NDUGAI AANZA KULIFANYIAKAZI AGIZO LA MAGUFULI



NA HAPPINESS MTWEVE, DODOMA

SPIKA wa Bunge Job Ndugai, amesema ofi si yake imeandaa waraka maalum ambao utatumika kuchambua safari za nje kwa ajili ya maofi sa wake na kwamba zenye umuhimu na maslahi kwa taifa ndizo zitapewa kipaumbele.

Amesema hatua hiyo inalenga kuunga mkono jitihada na maelekezo ya Rais Dk. John Magufuli ya kupunguza matumizi ya serikali ili kuelekeza nguvu zaidi kwenye huduma za jamii na miradi ya maendeleo nchini.

Aidha, amesema kamwe hayuko tayari kuona Ofi si ya Bunge inanyooshewa kidole kutokana na matumizi mabaya ya fedha ikiwemo safari za nje za maofisa wa bunge.

Kauli hiyo ya Ndugai imekuja wakati taasisi, mamlaka na serikali zikitekeleza agizo la Dk. Magufuli la kubana matumizi huku watendaji wakipigwa ‘stop’ kusafi ri nje ya nchi, ambapo wakati wa hotuba ya kuzindua Bunge, aliitaja taasisi hiyo kama moja inayotajwa kuwa na matumizi mabaya ya fedha.

Akizungumza na UHURU katika mahojiano maalum nyumbani kwake mjini hapa jana, Ndugai alisema amejipanga kikamilifu kuhakikisha anaifuta sifa hiyo chafu kwa kutokuwa na mambo hayo.

“Tumeandaa waraka maalumu kwa ajili ya kupima kila kitu…safari tutaangalia zile zenye manufaa kwa taifa. Hatuwezi kusimamisha safari zote kwa sababu kuna mikutano ambayo ni lazima kama nchi tushiriki na si vinginevyo,” alisema Ndugai ambaye amechukua mikoba ya Anne Makinda.

Alisema kwa kuanzia wataanza na ziara za mafunzo nje ya nchi kwa Kamati za Kudumu za Bunge, ambazo zitapunguzwa kwa kiasi kikubwa ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya washiriki.

Ndugai alisema kitendo cha Ofi si ya Bunge kutajwa miongoni mwa taasisi zenye matumizi mabaya ya fedha, kinachafua taswira yake, hivyo ni lazima wajipange kikamilifu kusafi sha na kuifanya kuwa safi .

Alisema tayari wiki iliyopita alikutana na kufanya mazungumzo na watumishi wote wa Bunge, kupanga mikakati ya kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu.

“Tumeanza kujipanga kikamilifu na kamwe hatutamvumilia mtumishi ambaye ni mzembe na asiyetekeleza vyema majukumu yake ipasavyo kwa sababu zama za kuvumiliana zimekwisha…Hapa ni kazi tu,” alisema.

Akizungumzia kuhusiana na wabunge wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kufanya vuruguwakati wa hotuba ya Dk. Magufuli kuzindua Bunge la 11, Ndugai alisema hawakutumia busara.

Hata hivyo, alisema amejipanga kuhakikisha Bunge la 11 linakuwa la tofauti na lenye nidhamu na kwamba atatenda haki kwa wabunge wote, lakini atasimamia kanuni na taratibu za Bunge.

Alisema awali UKAWA walimwandikia barua na kumueleza kuwa watafanya fujo iwapo Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ataingia ndani ya ukumbi wa Bunge kwa madai kuwa Zanzibar hakuna rais.

Alisema kutokana na hatua hiyo, walikutana na viongozi wa UKAWA ambao waliwasilisha ombi lao kutaka Dk. Shein asiingie bungeni, jambo ambalo alisema hakuwa na uwezo nalo na halitekelezeki.

“Nilikubali kufanya mkutano nao baada ya kuniomba kufanya hivyo, lakini jambo walilonieleza sikuwa na uwezo nalo na halitekeleziki, hivyo sikukubaliana nao kabisa,” alisema.

Ndugai alisema kitendo kilichofanywa na wabunge hao kilimkasirisha sana kwani hakipendezi machoni kwa Watanzania ndani na nje ya nchi na kuwa baada ya Dk. Magufuli kumaliza kuhutubia aliwatumia salamu akiwataka kutorudia kufanya vitendo hivyo.

Aliongeza kuwa ni jambo la ajabu kama wabunge watakaa ndani wakipewa posho kupitia fedha za Watanzania na badala yake wanatumia posho hizo kufanya fujo badala ya kujadili mambo ya msingi.

Alisema pale bungeni, wabunge wanapaswa kujadiliana kwa hoja na kufi ka muafaka kwa mustakabali wa taifa na Watanzania waliowaamini na kuwapa dhamana ya kuwaongoza.

“Nitakuwa Spika wa ajabu sana kama nitashindwa kuchukua hatua pale ninapoona baadhi yetu wanakiuka kanuni na kuchezea fedha za Watanzania ambazo zinatumika kutulipa posho,” aliongeza Ndugai.

Aidha, aliahidi kutumia mamlakayake ya Spika kutoa adhabu kali kwa wale wote watakaosababisha vurugu ndani ya ukumbi wakati shughuli zikiendelea.

Kuhusu uendeshaji wa Bunge, Ndugai alisema amejifunza mambo mengi na ambayo yatampa muongozo kutoka kwa mwalimu wake Anne Makinda, Spika wa Bunge la 10.

Alisema kila hatua aliyopita Spika Anne na yeye alipita, hivyo anaamini kabisa alikuwa na mwalimu mzuri na atafanya vizuri kupitia elimu hiyo.

Kusuhu serikali kuhamia Dodoma ambayo ndio Makao Makuu ya Chama na serikali, alisema wanampongeza Dk. Magufuli, ambaye mpaka sasa bado anaendelea kufanyia shughuli zake katika Ikulu ya Chamwino mjini hapa.

Alisema licha ya kuwa katika hotuba yake ya uzinduzi wa bunge hakuzungumzia jambo hilo, lakini ni ajenda moja wapo ya CCM, hivyo wanamuomba abariki na kukamilisha mchakato huo sasa.

No comments:

Post a Comment