Wednesday 25 November 2015

SAMIA AKAZA BUTI


MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesema serikali itaendelea kuahirisha kufanyika kwa sherehe mbalimbali nchini ili fedha hizo ziweze kutumika kwa mambo ya kijamii.

Amesema kwa msimamo huo ambao Rais Dk. John Magufuli, ameuanza, amewataka wananchi kushirikiana na serikali ili kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa gharama nafuu na ufanisi mkubwa.

Kauli hiyo aliitoa jana, Dar es Salaam, wakati alipokutana na uongozi wa Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania (WFT) kuzungumzia dhamira ya serikali katika kuyatafutia ufumbuzi matatizo yanayowakabili wanawake na watoto wa kike nchini.

Alisema maamuzi hayo ni sehemu ya mpango wa kuimarisha utendaji serikalini kuanzia serikali kuu hadi serikali za mitaa ili fedha zinazopatika zimfi kie kila mwananchi.

“Hivi sasa tuna mpango wa kuimarisha utendaji serikalini kuanzia serikali kuu hadi serikali za mitaa ili kinachopatikana kidogo kimfi kie kila mwananchi,” alisisitiza Samia.

Aliongeza kuwa, atafuatilia kwa karibu utekelezaji wa ahadi ya kupatikana kwa maji safi na salama, kuboresha afya ya mama na mtoto na utoaji elimu na uhifadhi wa mazingira.

Alisema suala la maji liko kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na miradi ya kuchimba visima virefu katika mikoa ya Singida na Dodoma iko kwenye mchakato na cha msingi ni kusimamia fedha hizo zitumike kuleta maji kama ilivyokusudiwa.

“Nilipokuwa kwenye kampeni nimejionea shida ya maji na wanawake ndiyo wanaopata tabu ya kutembea mwendo mrefu kutafuta maji. Kwa hiyo, pamoja na kazi zangu za kumsaidia Rais, nitasimamia miradi yote ya maji, angalau kuhakikisha maji yanapatikana umbali wa mita 400 kutoka eneo wananchi wanakoishi au karibu zaidi,” alisema.

Kuhusu afya ya mama na mtoto alisema, Samia alisema kazi hiyo ataianza hivi karibuni kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotetea haki za wanawake ili kupunguza vifo vinavyosababishwa na mimba za utotoni.

Hata hivyo, alisisitiza kusimamia suala la kuhakikisha zahanati, vituo vya afya na hospitali nchini zinakuwa na dawa na vifaa tiba vya kutosha katika wodi za wazazi kwa ajili ya kuhudumia kina mama na wananchi.

Kwa upande wa elimu, Makamu wa Rais alisema, atasimamia ujenzi wa mabweni kwa watoto wa kike na kuhakikisha mazingira yanatunzwa.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Mtandao huo, Profesa Ruth Meena, alimpongeza Samia kwa kushika nafasi ya juu ya uongozi akiwa mwanamke wa kwanza kuweka historia nchini.

No comments:

Post a Comment