Tuesday 24 November 2015

TRAFFIKI 80 MATATANI PWANI


NA MWANDISHI WETU

SIKU chache baada ya gazeti hili kufichua vitendo vya rushwa vinavyofanya na askari wa usalama barabarani mkoa wa Pwani, kugeuza mradi wa kujiingizia kipato badala ya kusimamia majukumu yao ya kiusalama, polisi mkoa huo imeanza panguapangua kwa askari hao.

Panguapangua hiyo imehusisha askari 80 wa kikosi cha usalama barabarani, kuondolewa na kupangiwa kazi zingine za kipolisi.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kubainika utendaji kazi wa askari hao kutoridhisha pamoja na kufikishiwa malalamiko ya muda mrefu na jamii juu ya tabia ya uombaji rushwa.

Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Polisi mkoani wa Pwani, Jaffari Ibrahim, alisema kumekuwepo na malalamiko mengi kuhusu vitendo vya rushwa na utovu wa nidhamu kwa askari hao, hivyo jeshi limeamua kuboresha ufanisi.

Alisema mabadiliko hayo yanalenga kuimarisha utendaji wa kazi na kudhibiti vitendo mbalimbali vinavyolalamikiwa na wananchi.

Alieleza kuwa wamegundua tatizo linalosababisha askari hao kukiuka sheria za kazi zao ni kutokana na kukaa kwa muda mrefu katika kitengo hicho bila kubadilishwa na kuhamishwa kitengo kingine.

Kamanda Ibrahim alielezea kuwa wapo baadhi ya askari wa usalama barabarani wanaolalamikiwa kuomba rushwa kwa kukusanya fedha kwa madereva, lakini wamekuwa wakikosa ushahidi.

Aidha, alisema kutokana na kukosa ushahidi, jeshi la polisi limekuwa likikwama kuwachukulia hatua za kuwafukuza kazi askari husika.

Kamanda huyo alisema kufuatia kukosa ushahidi,wameomba ushirikiano na jamii na madereva kutoa taarifa polisi kupitia ofisi ya kitengo cha usalama barabarani na jeshi la polisi mkoa huo bila kuogopa.

Aliwataka wananchi kutoa taarifa za madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani na kuwaasa madereva kufuata sheria za barabarani.

Hivi karibuni, gazeti hili liliripoti kushamiri kwa vitendo vya rushwa kwa baadhi ya askari hao, ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo hivyo kwa kukusanya fedha kutoka kwa madereva wa magari wanayoyazuia kwenye vizuizi mbalimbali kwenye barabara ya Kilwa.

Pia, ilibainika kuwa karatasi zinazotumikakuandikiafaini (notification), zinazotolewakwa madereva pindi wanapokiuka sheria za usalama barabarani, hazina vigezo vya uhalali na zinatolewa bila stakabadhi, hivyo kuikosesha serikali mapato.

Fedha hizo zinakusanywa kwenye vituo vya ukaguzi vya Kongowe Kanisani,Shamba la Mwandege Bakharesa, Jaribu na Mkuranga. Wakihojiwa kwa sharti la kutotajwa majina wala namba za usajili wa magari hayo, baadhi ya madereva walisema kwenye vibanda hivyo, kuna daftari wanaloandikisha namba za usajili za magari yaliyotoa fedha kiasi cha sh. 5,000.

Walidai kuwa katika kituo cha ukaguzi wa magari cha Shamba la Mwandege, bila kulipa fedha hizo gari husika haliwezi kuendelea na safari kwa madai ya kukiuka kanuni na sheria za usalama barabarani.

Gazeti hili Novemba 12 na 13, mwaka huu, lilifika kwenye kituo hicho cha ukaguzi na kukaa kwa saa nne kila siku, ambako lilishuhudia magari yote yaliyozuiliwa kwa muda huo, askari na madereva wakifanya mazungumzo nje ya magari hayo na kisha kuruhusiwa.

Kwa mujibu wa madereva na utingo wa magari hayo, ukaguzi unaofanyika kwenye kituo hicho ni kuhakikisha kama muhusika amelipa sh. 5,000 na sio usalama wa gari husika.


 

No comments:

Post a Comment