BAADA ya Rais Dk. John Magufuli, kumteua Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Kassim Mjaliwa, kushika wadhifa wa waziri mkuu, wasomi mbalimbali nchini wamesema uteuzi huo umekidhi vigezo vya kiongozi mwajibikaji.
Wamesema Majaliwa ni kiongozi asiyekurupuka katika kufanya maamuzi na anafahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, baada ya kutumikia nafasi ya Naibu Waziri wa TAMISEMI.
Wasomi hao walibainisha kuwa, licha ya uteuzi huo kuwa wa kushtukiza kwa Watanzania wengi, umelenga kumpata kiongozi atakayesimamia shughuli za serikali kwa weledi.
Wakizungumza na gazeti hili jana, baada ya Majaliwa kuthibitishwa na Bunge kushika wadhifa huo, walisema kiongozi huyo ni mchapakazi na mwenye busara katika kufikia maamuzi.
Mwanazuoni na mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benson Banna, alisema uteuzi huo umezingatia mahitaji halisi ya Watanzania.
Alibainisha kuwa licha ya uteuzi huo kuwa wa kushtukiza, wananchi hawakuhitaji waziri mkuu mwenye kupenda kujulikana, bali umaarufu wake upatikane kwa namna anavyofanyakazi za kuwatumikia wananchi.
Mhadhiri huyo wa UDSM alisema, maamuzi hayo ya Dk. Magufuli kumteua Majaliwa, yameonyesha namna ambavyo kiongozi huyo anavyofanya maamuzi pasipo kukurupuka.
“Dk. Magufuli anachukua maamuzi yake kwa kujikita kwenye kazi ya kuwatumikia wananchi, hivyo Majaliwa ni kiongozi sahihi kwa sababu ana uzoefu wa kutosha, tangu alipokuwa TAMISEMI,” alisisitiza.
Profesa Banna aliongeza kuwa, madai yanayotolewa na baadhi ya watu kuwa Majaliwa ni mpole, hayana msingi kwa kuwa hicho sio kigezo cha kumpata kiongozi bora.
Alisema Majaliwa amekuwa akichukua maamuzi yenye busara na hekima kwa maslahi ya nchi na hiyo ndiyo sifa ya kiongozi bora mwenye kufaa kuwatumikia wananchi.
PROFESA KAYUMBO
Kwa upande wake, msomi kutoka UDSM, Profesa Hosea Kayumbo, alisema uteuzi uliofanywa na Rais Dk. Magufuli, licha ya kuwa wa kustukiza, umeifanya serikali yake kuwa ya kipekee.
Alisema uteuzi wa Majaliwa kushika nafasi hiyo ya uongozi wa shughuli za serikali ni sahihi kwa sababu ni mfuatiliaji na sio mwenye kufanya maamuzi ya kukurupuka.
Profesa Kayumbo alisema uchapakazi wake ulidhihirika wakati wa ufuatiliaji wa agizo la ujenzi wa maabara kwenye shule za kata, hivyo bila shaka atatoa mchango mkubwa zaidi kwenye sekta ya elimu.
Akizungumzia utendaji kazi wa waziri mkuu huyo mteule wakati alipokuwa mkuu wa wilaya ya Urambo mkoani Tabora, alisema wananchi wa wilaya hiyo wanamkumbuka kwa kuwashurutisha watendaji wazembe.
“Wananchi wa Urambo wanamkumbuka sana kwa uchapakazi wake uliozingatia sheria na kanuni, ambao uliwachukiza watendaji wazembe,” alibainisha Profesa huyo.
Aliongeza kuwa licha ya baadhi ya watu kupanga kumkwamisha, alifanikiwa kuwadhibiti.
Alisema Dk. Magufuli amedhihirisha namna ambavyo serikali yake itakavyoendeshwa na viongozi wachapakazi, hivyo wananchi wana matumaini na serikali ya awamu ya tano.
No comments:
Post a Comment