Thursday, 19 November 2015

MAJALIWA WAZIRI MKUU MPYA



WAZIRI Mkuu mteule, Kassim Majaliwa, amesema alijikuta akibubujikwa machozi wakati Spika wa Bunge, Job Ndugai, akitangaza jina lake kuwa ameteuliwa na Rais, Dk. John Magufuli, kushika wadhifa huo.

Amesema hakuwa na taarifa kuhusiana na uteuzi huo na kwamba, wakati Spika Ndugai akifungua bahasha yenye jina kutoka kwa Dk. Magufuli, alikuwa akiangalia luninga pamoja na wapigakura wake waliokuja kumshuhudia akiapishwa bungeni juzi.

“Nililia na ilikuwa ni hisia za kibinadamu pale nilipoona kupitia televisheni nikitangazwa kuwa rais ameniteua kuwa waziri mkuu,” alisema Majaliwa wakati akizungumza na waandishi wa habari nje ya viwanja vya Bunge.

Alisema kama ilivyo kwa wabunge wengi, wakati kipindi cha Bunge kikiendelea, alikuwa ameketi akikamilisha mipango ya kuwasafirisha wapigakura wake waliofika kushuhudia akiapa, ambao wakati huo walikuwa wakiangalia luninga kuona kinachoendelea.

“Kundi la kwanza liliondoka jana, walibaki wachache ambao nilishakamilisha mipango ya kuwasafirisha kurejea nyumbani leo (jana) saa tano. Walikusanyika kuangalia Bunge kupitia luninga, nami nikajumuika nao na ndipo tulishuhudia spika alivyokuwa na zile bahasha, sikujua kama ndani kuna jina langu, sikuamini niliposikia natajwa.

“Nilipata mshituko mkubwa na nilijikuta natokwa machozi, lakini namshukuru Dk. Magufuli kwa kuniamini na kunipa nafasi hii kubwa. Sifahamu ametumia vigezo gani, lakini naahidi sitamuangusha,” aliongeza.

Wkati akitangazwa, Majaliwa alikuwa nyumbani kwake akifungasha mizigo ili kuhama kwenye nyumba ya serikali na kuhamishia makazi yake katika nyumba ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) .

Majaliwa, ambaye uteuzi wake haukutarajiwa na wengi, alisema hakuwa na maandalizi yoyote kwa kuwa hakufahamu kama atateuliwa kushika wadhifa huo, ambapo ameahidi kufanya kazi kwa nguvu baada ya kuapishwa na kuahidi ushirikiano kwa wabunge wote.

Uteuzi wa Majaliwa umethibitishwa na Bunge kwa kupata kura 258, ikiwa ni asilimia 73.5 ya kura zote.

MAMBO YALIVYOKUWA

Jana asubuhi wabunge waliingia ukumbini huku wakiwa na shauku kubwa ya kufahamu jina la Waziri Mkuu, na hilo limetokana na usiri mkubwa uliotawala kwa muda mrefu kuhusiana na mteule huyo wa Dk. Magufuli.

Tofauti na miaka yote, utaratibu wa uwasilishaji wa bahasha yenye jina la Waziri Mkuu, uliongeza hamasa ya wabunge na Watanzania kutokana na kuwa na tofauti kubwa.

Saa 3.31 asubuhi, mpambe wa rais alionekana akiingia kwenye viwanja vya Bunge huku akiwa na bahasha mkononi, wakati ambao tayari Spika wa Bunge, Job Ndugai alikuwa amemuagiza Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, kufuata bahasha hiyo nje ya ukumbi.

Hata hivyo, wakati wabunge wakiendelea kusubiri, Dk. Kashililah hakurudi  na bahasha hiyo, Badala yake, alirejea mikono mitupu na kutoa taarifa kuwa Dk. Magufuli amemwagiza mpambe wake kuikabidhi bungeni mwenyewe.

“Nimepokea taarifa kutoka kwa Katibu wa Bunge kuwa mambo yameshaiva na rais amemuagiza mpambe wake ailete kwangu moja kwa moja, hivyo mlinzi huyo ataileta kwangu akiongozwa na askari wa Bunge,” alisema Spika Ndugai.

Baada ya hapo aliruhusu mpambe huyo kuingia ndani ya ukumbi, ambapo alisindikizwa huku akiwa ameishika bahasha hiyo mkononi. Hatua hiyo iliamsha shangwe kubwa ndani ya ukumbi wa Bunge.

Spika Ndugai alipopokea bahasha hiyo, aliinyanya juu kuonyesha kuwa imekuja kwa siri huku ikiwa imegonjwa muhuri wa moto.

Akisaidiwa kufungua bahasha hiyo na Dk. Kashililah, Ndugai alisema:

“Nimefungua bahasha ya kwanza, ndani yake kuna bahasha nyingine, nafungua tena bahasha ya pili na bahasha ya tatu ndiyo iliyobeba karatasi yenye jina la Waziri Mkuu.”

Ndugai alisema barua hiyo imeandikwa na rais kwa mkono wake mwenyewe na si kuchapwa kwa kompyuta kama ilivyozoeleka.

Alilisoma jina hilo, ambapo wabunge walisimama huku wale wa CCM wakionekana kumtafuta Majaliwa mahali alipokaa ili wampongeze, lakini hakuwemo ndani ya ukumbi huo.

Spika baada ya kukamilisha kazi hiyo, aliahirisha bunge kwa muda wa saa moja ili kumpa nafasi Katibu wa Bunge kwenda kuandaa wasifu wake. Majaliwa alionekana akiingia kwenye viwanja vya Bunge na baadaye ndani ya ukumbi, muda mfupi baadaye.

WABUNGE WAUNGA MKONO

Wakiunga mkono hoja ya kujadili jina la waziri mkuu, mbunge wa Isimani, William Lukuvi alisema Majaliwa anazo sifa za kushika nafasi hiyo kwa kuwa ni muadilifu.


Lukuvi alisema uteuzi uliofanywa na Rais Magufuli ni uteuzi makini na sahihi hasa kwa wakati huu wenye changamoto nyingi.

‘’Katika kipindi chote kilichopita, hakuna mbunge ambaye atasema aliwahi kugombana na Mjaliwa kwani ni mpole na mtu msikivu,’’ alisema.

Kwa upande wake, Jenister Mhagama (Peramiho), alisema Majaliwa hana kashfa yoyote wala makundi, hivyo anafaa kushika nafasi hiyo nyeti.

Alisema kutokana na kasi aliyonayo Rais Mgufuri, inafaa kuwa na waziri mkuu ambaye ni kijana na atakayeendana na kasi yake.

Naye Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, alisema anamfahamu Majaliwa tangu alipokuwa mkuu wa wilaya mwaka 1996.


Alisema ni mtu msikivu na mnyenyekevu na kwamba hata baada ya kuteuliwa kuwa naibu waziri, bado aliendelea kuwa hivyo.


Kange Lugola, akichangia hoja hiyo alisema, Mungu amesikia kilio cha Watanzania kwa kuwapatia waziri mkuu, ambaye ni mtenda kazi.

“Tumepata Rais Tingatinga na sasa tumepata waziri mkuu, ambaye ni jembe, sasa nchi itakwenda kwa kasi inayostahili,’’ alisema Lugola.

SALAMU ZA MAJALIWA

Akitoa salamu za shukrani baada ya Bunge kumthibitisha, Majaliwa aliahidi kutembelea majimbo yote ili kuangalia changamoto na namna ya kuzipatia ufumbuzi.

Alisema atafanyakazi hiyo bila kuangalia tofauti ya vyama vya wabunge, ambapo atatanguliza maslahi ya Watanzania mbele.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa tasnia ya habari, ataendelea kufanya kazi na vyombo vya habari nchini kote.

Majaliwa alisema kwa muda mrefu katika kazi zake, ameshirikiana kwa karibu na vyombo vya habari, kuona kuwa wananchi wanapata taarifa zilizo sahihi na yale yanayofanywa na serikali kutangazwa.

NJE YA BUNGE

Wakizungumza nje ya bunge, wabunge wengi waliunga mkono uteuzi huo na kusema kuwa ni kijana asiyekuwa na makundi na hivyo ataimudu kazi yake.

Mbunge wa Lulindi (CCM), Jerome Bwanausi, alisema anamfahamu vizuri Majaliwa tangu akiwa mwalimu, baadaye mkuu wa wilaya na hata alipokuwa naibu waziri.

“Ni mtu makini, huwa hakurupuki, tunategemea kasi katika kutekeleza majukumu ya serikali na kuondoa kero za wananchi,” alisema.

Zaynab Vullu, mbunge wa Viti Maalumu CCM, alisema alimfahau Majaliwa akiwa DC katika Wilaya ya Rufiji, ambako alikuwa kimbilio la wananchi.

“Hata alivyofanya kazi TAMISEMI, Majaliwa alisikiliza sana hoja za wananchi na safari hii walimu wamepata mkombozi,” alisema.

Kwa upande wake, mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia, alisema amefurahi naibu wake kuaminiwa kushika wadhifa huo.

Alimtaja Majaliwa, ambaye alikuwa Naibu wake TAMISEMI, kuwa ni mwaminifu, mwadilifu, mchapakazi na si mtu wa makundi.

“Watanzania wategemee mabadiliko ya kimaendeleo, sina shaka naye,” alisema Hawa.

Naye Khadija Hassan Aboud, alielezea kufurahishwa kwake na uteuzi huo na kusema kuwa, kwa jinsi Majaliwa alivyo mchapakazi, anaimani ataendana na kasi ya Dk. John Magufuli. Alimtaja kuwa ni msikivu na mwajibikaji mzuri.

Mbunge wa jimbo la Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF), alisema Majaliwa ni mchapakazi na hana makundi, hivyo rais hajakosea kumteua katika nafasi hiyo.

Alisema anamfahamu Majaliwa tangu alipokuwa mkuu wa wilaya ya Urambo, ambapo aliweza kufanyakazi bila ya ubaguzi kwa sababu yeye alikuwa upande wa upinzani na alimpa ushirikiano.

“Rais hajafanya makosa, amepata kiongozi mzuri, hana makundi, anaheshimu kila mtu na hana kashfa na kama rais angekosea na kutuletea mtu mwenye kashfa, tungeanza nae hapahapa,” alisema.

Alisema licha ya kutoka upande wa upinzani, hana matatizo kwa mtu anayetekeleza majukumu yake ipasavyo na atashirikiana naye katika kufanyakazi na kutimiza malengo ya kuliletea taifa maendeleo.

LUSINDE

Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, alisema rais amemteua kiongozi sahihi ambaye atamudu kutumikia vema nafasi hiyo.

Alisema Majaliwa ni kiongozi makini, mtulivu na anayetoa maamuzi kwa wakati, hivyo wamepata jembe lingine na kuomba wananchi wamuunge mkono.

JAFO

Suleiman Jafo, ambaye ni mbunge wa Kisarawe, alisema taifa lilikuwa linahitaji mtu ambaye hana makandokando ya ufisadi kama Majaliwa, hivyo alimpongeza rais kwa uteuzi huo.

Alisema Rais Magufuli ameingia Ikulu bila ya wapambe, hivyo wananchi watarajie utendaji wenye tija kutoka kwa viongozi makini watakaoweza kwenda sambamba na kasi yake.

Jafo alisema amefurahia uteuzi wa Majaliwa katika nafasi ya waziri mkuu kwa sababu anafahamu utendaji wake na ni mtu wa watu, ambaye mara zote huwa makini kusikiliza hoja za watu na kuzitolea maamuzi bila ya ubaguzi.

MARTHA MLATA

Alisema Rais Magufuli ameonyesha dhamira yake ya dhati ya kutaka kulikwamua taifa kutokana na uteuzi wa Majaliwa katika nafasi ya waziri mkuu.

Martha, ambaye ni mbunge wa viti maalumu, alisema Majaliwa hana makundi, hivyo atamsaidia rais katika utekelezaji wa kaulimbiu yake ya ‘Hapa kazi tu’.

GEORGE SIMBACHAWENE

Alisema  hakushangaa aliposikia rais amemteua Majaliwa katika nafasi ya uwaziri mkuu, kwa sababu ni mtu makini na historia yake kiutendaji ipo wazi, ni mchapakazi na ataendana na kasi ya Dk. Magufuli.

MAGRETH SITTA

Aliipongeza serikali kwa ujasiri na amefurahia uteuzi wa Majaliwa kwa sababu ana uwezo mkubwa kiutendaji, hivyo atasaidia taifa kuboresha maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu.

PROFESA LIPUMBA

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema uteuzi huo wa Majaliwa, ni wa kushtukiza kwa kuwa si miongoni mwa waliokuwa wakifikiriwa, hivyo ni wazi Rais Magufuli amedhihirisha kuwa hana ubia katika kazi zake.

Profesa Lipumba alisema Rais Magufuli ameonyesha kuwa anahitaji watu wa kufanya nao kazi na kwa kuwa waziri mkuu ndiye mtendaji wa serikali, ni muhimu kujenga uwezo wa kuridhibiti bunge na kuhimili utendaji.

HAMAD RASHID

Kwa upande wake, aliyekuwa mbunge wa Wawi,Hamad Rashid, alisema taifa lilikuwa linahitaji waziri mkuu mwadilifu, mchapakazi, anayekubalika na wananchi, hivyo Rais Magufuli ametekeleza kwa vitendo mahitaji ya taifa.

Alisema Majaliwa ni mtu wa watu na kiongozi anayetumika na wananchi kutokana na ushirikiano alionao kwa wabunge na kutokuwa mtu wa makundi katika bunge wala jamii, hivyo anastahili nafasi hiyo.

“Si mtu wa makando kando, hivyo tumepata waziri mkuu na rais wanaotosha kupambana na ufisadi. Kazi kubwa iliyopo sasa ni kupata baraza la mawaziri lenye kulingana na heshima za viongozi hao ili dhana ya ‘Hapa kazi tu’ iweze kutekelezwa kwa uadilifu,”alisema.

RUANGWA YALIPUKA KWA FURAHA

Mara baada ya mbunge wao kutangazwa kuwa ameteuliwa nafasi ya uwaziri mkuu, wakazi wa jimbo hilo walianza kushangilia na kumuomba asiwasahau kwa sababu bado wanahitaji mchango wake.

Walisema  wana imani na kiongozi huyo na kumuomba aendelee kushirikiana nao katika kuboresha maendeleo ya jimbo hilo.

Mbali na wananchi, wanafamilia nao walisema wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumuwezesha ndugu yao kuteuliwa kushika wadhifa huo.

Mdogo wa Majaliwa, anayeitwa Hamis Majaliwa, alisema amefurahishwa sana na kaka yake kuteuliwa katika nafasi hiyo na anamuombea kwa Mwenyezi Mungu aweze kumuongoza katika utekelezaji wa majukumu yake.

Hamis, alisema wao kama familia, wamefurahishwa na uteuzi huo na kwamba wanaomba wananchi wampe ushirikiano ili aweze kufanikisha malengo yake.

Pia, aliwashukuru wakazi wa jimbo hilo ambao ndiyo walioanza kumchagua kwa kura katika nafasi ya ubunge.

Alisema Majaliwa ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto watatu ya Mzee Hamis Majaliwa na Binasa Issa, ambao wote walikuwa wakulima na tayari wamefariki.

WASIFU WA MAJALIWA

Alizaliwa Desemba 12, mwaka 1960, katika Kijiji cha Nanndagala kwenye Tarafa ya Nnacho, wilayani Ruangwa, Lindi.

Alisoma Shule ya Msingi Nnacho mwaka 1970 hadi 1976, ambapo mwaka 1977, alichaguliwa kujiunga na masomo ya Sekondari ya Kigonsera na kuhitimu 1980.

Alijiunga na masomo ya ualimu kwenye Chuo cha Ualimu Mtwara mwaka 1991 na kuhitimu mwaka 1993.

Mwaka 1994, alijunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuhitimu mwaka 1998.

Alijiendeleza kimasomo katika Chuo Kikuu cha Stockhom nchini Sweden mwaka 1998.

Mbali na msuala ya kitaaluma, Majaliwa aliwahi kuwa Katibu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) mkoa wa Singida na kushika nafasi ya kuwa Mjumbe wa Baraza la CWT Taifa.

Kwenye nyadhifa za utumishi serikalini, aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya za Urambo mkoani Tabora na Rufiji mkoani Pwani.

Mwaka 2010, alijitosa kuwania ubunge katika Jimbo la Ruangwa na kuibuka mshindi, ambapo aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, anayeshughulikia masuala ya elimu. Majaliwa ana mke mmoja na watoto wanne.

No comments:

Post a Comment