SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, jana, alimwapisha Dk. Tulia Mwansasu, kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dk. Tulia, aliapishwa kushika nafasi hiyo, baada ya kuchaguliwa kwa kura 250, sawa na asilimia 71.2, na kumwangusha mpinzani wake, Magdalena Sakaya (CUF), aliyepata kura 101.
Jumla ya kura zilizopigwa zilikuwa 351, ambapo hakuna kura iliyoharibika.
Baada ya kula kiapo, Dk. Tulia alimshukuru Rais John Magufuli kwa kumteua kuwa mbunge na kuwashukuru wabunge wote kwa kumchagua.
Alisema atafanya kazi bila ubaguzi na kumsaidia Spika Job Ndugai katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku.
“Nitafanyakazi bila upendeleo wa vyama, elimu, jinsia ama umri. Nitailinda na kuiteteta katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuisimamia serikali kuona inatekeleza majukumu yake,” alisema.
Kwa upande wake, Magdalena alimpongeza Dk. Tulia kwa kushinda nafasi hiyo na kusema, anatarajia chini ya nafasi hiyo na kumsaidia spika, bunge litakuwa imara.
Katika hali ya kushangaza, wabunge wa upinzani walianza kuleta vurugu wakati mgombea huyo alipokuwa akijibu maswali.
Muda wote walionekana wakizomea, hali iliyomfanya katika swali la mwisho, spika kumruhusu mgombea huyo kwenda kuketi.
Baadhi ya watu waliokuwa wanashuhudia bunge katika uchaguzi huo, walieleza masikitiko yao ya tabia ya wabunge kuanza kuzomea zomea hasa katika mambo ya msingi.
No comments:
Post a Comment