Thursday 19 November 2015

MASKANI ZA CHAMA ZATAKIWA KUJIPANGA


MTANDAO wa Maskani za CCM Zanzibar, umetakiwa kujipanga na kujiweka tayari kushiriki uchaguzi mkuu wa marudio na kuhakikisha Chama kinaendelea kushika hatamu za dola nchini.
Umehimizwa kundeleza hamasa ili Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), itakapotangaza tarehe ya uchaguzi, maskani zote zisimame imara kushiriki uchaguzi huo kikamilifu.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alitoa agizo hilo jana, alipokutana na wana-mtandao wa maskani za CCM, katika kikao chao kilichofanyika Amani, mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Alisema maskani za CCM kwa miaka mingi zimekuwa muhimili na uti wa mgongo kwa maendeleo ya siasa za Chama.
"Maskani za CCM ni uso kamili wa Chama, ndio macho, moyo na masikio ya Chama chetu katika kupata na kukusanya maoni, ushauri au mawazo shirikishi, tusizipuuze na kuziweka pembeni," alisema Shaka.
Alisema maskani hizo wakati wote huwa ni chimbuko na hazina ya hamasa, harakati za kisiasa na chachu ya kuyaendeleza mapinduzi ya Zanzibar umoja na upendo kwa Wazanzibari wote.
Katibu mkuu huyo aliwataka wana-maskani wote kujenga tabia ya kukutana, kujadiliana, kupanga mikakati na mipango itakayokisaidia Chama kupata mafanikio
"Turudishe vuguvugu la maskani za CCM, tuendeleze joto la uhamasiahaji na kueneza siasa ya Chama kwa umma, maskani zetu ziwe kioo cha Chama mahali popote," alisema.
Akitoa maoni yake katika mkutano huo, mwana-CCM kutoka maskani ya Kachorora, Selemani Ganzi, alidai kiongozi aliyeua ari na kuviza uhai wa maskani ni Rais mstaafu Dk. Amani Abeid Karume.
Ganzi alidai chini ya uongozi wa Dk. Karume, maskani zilikufa kutokana na kutoendelezwa kwa sababu tu zilianzishwa na Rais mstaafu Dk. Salmin Amour, ambaye hakumpenda wala kumheshimu.
"Dk. Karume ameua maskani zetu sasa ni rafiki wa wapinzani wetu, amewahi kutuita CCM tuna akili za samaki, leo hii anataka upinzani uingie Ikulu, huyu hatufai tunataka kadi yetu," alisema Ganzi.
Kwa upande wake, mwana-maskani, Mohsin Madoea, alisema kitendo cha kuzipuuza maskani kimekigharimu na kukidhoofisha Chama huku akisema njia pekee ya kujinusuru ni kuzifufua.
Alisema bila kuimarika mashina ya CCM na matawi, Chama hakitaweza kupata uhai wala maendeleo ya kisiasa na kwamba hivi sasa hakuna njia nyingine zaidi ya kuzirudishia hadhi na heshima yake.
Naye Hamida Ismail Jabu, kutoka maskani ya Kwa Ali Natu, aliwataka watendaji wakuu wa Chama kusimamia majukumu yao ipasavyo pamoja na kutembelea matawi, majimbo na wilaya ili kufufua hamasa na uhai wa CCM.

No comments:

Post a Comment