Thursday 19 November 2015

WAMILIKI UCHUMI SUPERMARKET WAWALIZA WAJASIRIALALI, WADAIWA KUTOWEKA NA MABILIONI YA PESA


WASAMBAZAJI wa bidhaa mbalimbali nchini waliokuwa wakitoa huduma kwenye maduka ya Kampuni ya Uchumi Supermarket ya jijini Dar es Salaam, wameziomba serikali za Tanzania na Kenya, kuingilia kati ili walipwe fedha wanazoidai kampuni hiyo.

Zaidi ya wasambazaji 300, wamejitokeza hadharani wakieleza kuwa wanaidai Uchumi zaidi ya sh. bilioni 5.4, zinazotokana na kusambaza bidhaa mbalimbali kwenye maduka ya kampuni hiyo, ambayo imetangaza kufilisika na wamiliki wake kutoweka nchini.

Wakizungumza jijini Dar es Salaam, jana, wafanyabishara hao walidai wamiliki wa Uchumi Supermarket, wametoweka na fedha hizo ambazo ni za malipo yao baada ya kusambaza bidhaa  katika Supermarket hizo.

Walisema  kitendo cha wamiliki hao kutoweka na fedha hizo ni utapeli wa kuaminika,  ambao raia hao wa Kenya wamewafanyia wanawake wa Tanzania, ambao wanafanya shughuli zao katika mazingira magumu ili kujikwamua kiuchumi.

Walisema utapeli huo umewaacha wanawake wengi wajasiriamali katika mazingira magumu kwani asilimia kubwa  walikopa  fedha nyingi za mitaji katika benki  na  Chama cha Kuweka na Kukopa cha Tanzania Saccos for Women Entrepreneurship (TASWE), hivyo kuwaachia madeni makubwa.

Akizungumza katika mkutano wa kujadili sakata hilo uliowashirikisha wanawake  wanaodai fedha hizo, Mkurugenzi wa Bodi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), anayewakilisha wanawake wafanyabiashara, Anna Matinde, alisema wanawake wengi waliokopa fedha za mtaji kwa  ajili ya kuzalisha bidhaa  ili kuzisambaza katika Supermarket za Uchumi, hivi sasa wako katika hatari ya kufirisiwa na benki pamoja na Saccos.

“Tunalaani kwa nguvu zote kitendo cha wamiliki wa Uchumi kutoweka na fedha za kinamama hawa. Tunamuomba Rais Dk. Magufuli alingilie kati suala hili, kabla  halijaelekea kubaya. Rais asikilize kilio hiki cha kinamama wa Tanzania, ambao wameporwa fedha zao za mitaji na Wakenya, ambao walikuja kwa mgongo wa kuwekeza kumbe wana nia ya kutapeli,” alisema Anna, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Bodi ya Wafanyabishara Wanawake Tanzania.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wasindikaji Wadogo wa Chakula Tanzania (TAFOPA), Suzy Laiser, alisema wamiliki wa Uchumi baada ya kufilisika, walipaswa kulipa fedha hizo, lakini walitoweka na kuwaacha wadai wakihangaika.

“Binafsi nilikuwa upande wa bucha katika Supermarket hizo, mashine zangu zimefungiwa katika maduka yao na  ninawadai fedha nyingi. Tunamuomba Rais Dk. Magufuli atuangalie kwa jicho la huruma ili turudishiwe fedha zetu, la sivyo nyumba zetu zitauzwa kwa sababu tuliziweka rehani ili kupata mitaji.

“Tuna imani kubwa na Rais wetu kwa sababu anasisitiza zaidi watu kuchapakazi. Hivyo kina mama zaidi ya 300 watakosa shughuli za kufanya baada ya kufanyiwa utapeli huo,” alisema Suzzy.

Mwenyekiti wa kamati ya kufuatilia sakata hilo, Joseph Mlai, alisema wamejaribu kulifikisha suala hilo kwa balozi wa Kenya hapa nchini, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika.

Uchumi Supermarket ilifunga biashara zake nchini baada ya kutangaza kupata mgogoro wa kibiashara mwezi uliopita, huku ikishindwa kulipa stahiki za wafanyakazi.



No comments:

Post a Comment