Monday 4 January 2016

WATAKAOWATOZA WANAFUNZI MICHANGO KUKIONA-MAJALIWA


WAZIRI Mkuu, Kassim Majliwa, akikabidhiwa silaha za jadi na Mzee Daniel Gama,  baada ya kuwasili kwenye kijiji cha Maposele  na kukagua ujenzi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Peramiho, jana. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, akifungungua tawi la Benki ya Posta la Songea akiwa katika ziara ya mkoa wa  Ruvuma jana. Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Uratibu, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama kadi ya akaunti yake ya Benki ya Posta Tanzania, aliyokabidhiwa  baada ya kuifungua alipokuwa akifungua tawi la Benki hiyo la Songea, jana. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Majaliwa akikagua mahindi yaliyohifadhiwa nje ya majengo ya maghala ya  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA mjini Songea, jana,  akiwa katika ziara ya siku tatu mkoani Ruvuma.
(Picha na Ofisi ya Waziri  Mkuu)
 

Na Mussa Yussuf wa Uhuru, Ruvuma

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri nchini, kuzisimamia na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye shule za msingi na sekondari ili kuwabaini na kuwachukulia hatua za kinidhamu walimu watakaowatoza wanafunzi michango ambayo serikali imeipiga marufuku.

Amesema katika kutimiza azma ya serikali ya kutoa elimu bure, fedha za kuendeshea shughuli za kitaaluma zitapelekwa moja kwa moja shuleni na ni wajibu kwa wakurugenzi hao kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Aidha, amesisitiza kuwa kila mtoto mwenye umri kuanzia miaka minne, anapaswa kuanza masomo ya awali, hivyo kila shule ya msingi inapaswa kuwa na darasa maalumu la awali ili kumjengea mwanafunzi msingi imara wa kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.

Waziri Mkuu aliyasema hayo juzi, mkoani hapa, akiwa kwenye ziara ya kukagua shughuli mbalimbali za kimaendeleo pamoja na kubaini changamoto zinazowakabili wakazi wa mkoa huo.

Alisema wakurugenzi wa halmashauri wanapaswa kuzifanyia ukaguzi wa mara kwa mara shule zilizoko kwenye maeneo yao ya utawala ili waweze kujiridhisha hatua zilizofikiwa katika utoaji elimu bure.

“Majukumu ya ukaguzi wa shule yasiachwe kwa ofisa elimu pekee, kwani hata wakurugenzi wanapaswa kuzikagua kubaini namna zinavyotoa elimu kwa sababu zipo kwenye maeneo yao,” alisisitiza Majaliwa.

Alibainisha kuwa serikali imeanza kukusanya akaunti za benki za shule zote ili kupelekea fedha za kugharamia shughuli za utoaji elimu.

Waziri Mkuu alisema fedha hizo zitapelekwa moja kwa moja kwenye shule husika badala ya kwenye halmashauri, hivyo wakurugenzi wanapaswa kujiridhisha kwa kuzifanyia ukaguzi.

Alisema walimu watakaobainika kuwatoza michango mbalimbali wanafunzi, licha ya serikali kupiga marufuku, watachukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumzia changamoto ya utoro kwa wanafunzi, Majaliwa aliagiza kuwekwa kwa mkakati wa kuhakikisha kila mwanafunzi anayeanza darasa la kwanza, asiache shule hadi atakapohitimu masomo yake.

Alisema tatizo la utoro kwa wanafunzi linaweza kukabiliwa kwa walimu na wazazi kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana nalo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Saidi Mwambungu, alisema mkoa huo umenza mkakati wa kukabiliana na utoro pamoja na mimba kwa wanafunzi.

Alisema katika jitihada hizo, mwaka jana walifanikiwa kumkamata mwalimu wa sekondari aliyekuwa akidaiwa kujihusisha kimapenzi na wanafunzi na tayari amefikishwa mahakamani.

Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayokabiliwa na tatizo la utoro pamoja na ujauzito kwa wanafunzi.

Kwa mujibu wa takwimu za mkoa huo, mwaka juzi wanafunzi 56 wa shule za sekondari na tisa kutoka shule za msingi walipewa ujauzito.

Viongozi chama cha tumbaku kikaangoni

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza kukutana na viongozi wa Chama Kikuu cha Tumbaku mkoa wa Ruvuma, ili kueleza sababu za kushindwa kukiendesha kiwanda cha tumbaku.

Kiwanda hicho, ambacho awali kilikuwa tegemeo kwa wakazi na wakulima wa mkoa huo kwa utoaji wa ajira na kununua tumbaku kwa wakulima, kwa sasa kimeshindwa kujiendesha.

Amewaagiza viongozi hao waambatane na wawakilishi wa wakulima wa zao hilo ili kubaini sababu za kusuasua kwa kiwanda hicho.

Majaliwa alitoa agizo hilo juzi, mkoani hapa, ambapo aliwataka viongozi hao kumuelezea mkakati wao wa kuhakikisha chama hicho kinaimarika.

“Nahitaji kukutana na viongozi wa  chama kikuu cha ushirika cha Tumbaku, waniambie mkakati wao wa kukiendeleza chama hicho.

“Kile kiwanda kilikuwa muhimu kwa wakazi wa mkoa huu katika utoaji ajira, hivyo lazima wafike kunielezea mpango wao wa uendelezaji,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Alisema viongozi hao pia wanapaswa kutoa ahadi thabiti ya namna watakavyoimarisha maendeleo ya zao hilo ili kuinua uchumi wa mkoa pamoja na kipato cha wakulima.

Aidha, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa wakazi wa mkoa huo kutumia rasilimali za misitu iliyoko kwa ajili ya kuendeleza ufugaji nyuki.

Alisema soko la asali limezidi kupanuka hivyo ni muhimu kutumia fursa hiyo katika kujiongezea kipato kwa wananchi.

Aliwataka maofisa ufugaji nyuki kujifunza kupitia kwenye shamba la Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, lililoko Zuzu, mkoani Dodoma.

Alisema kwa sasa mahitaji ya asali yameongezeka na wakazi wa mkoa huo wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo muhimu kiuchumi.

 ‘Acheni kupima viwanja kibiashara’

HALMASHAURI nchini zimetakiwa kuacha kupima viwanja kwa madhumuni ya kibiashara zaidi, badala yake ziweke  viwango vya bei za viwanja vilivyopimwa ili viendane na uhalisia wa kipato cha wananchi.

Pia, zimetakiwa kununua vifaa vya kutosha vya upimaji ardhi ili kuendana na kasi ya ukuaji wa miji.

Halmashauri hizo pia zimetakiwa kuacha kuazima wataalamu wa upimaji ardhi kutoka maeneo mengine, badala yake kutumia wataalamu waliopo kwenye maeneo yao.

Maagizo hayo yalitolewa na juzi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Ruvuma.

Alisema baadhi ya halmashauri zimefanya zoezi la upimaji viwanja kuwa la kibiashara zaidi, hivyo kusababisha wananchi kushindwa kumudu kuvinunua kwenye maeneo yaliyopimwa.

“Upimaji ardhi haupaswi kufanywa kama sehemu ya biashara, wananchi wana uwezo wa kujenga, lakini wanakwamishwa na viwango vikubwa vya bei vilivyowekwa,” alisema Majaliwa.

Alisema halmashauri hazipaswi kuuza maeneo yaliyopimwa kwa gharama kubwa.

Aidha, Waziri Mkuu alisema upimaji ardhi haupaswi kuishia kwenye viwanja pekee, bali hata kwenye mashamba ili wakulima waweze kupata hatimiliki zitakazowawezesha kuzitumia kama msingi wa kujiongezea mitaji.

Alisema upimaji wa maeneo ni muhimu katika kupunguza migogoro ya ardhi, hivyo kuwawezesha wananchi kufanya shughuli za uzalishaji mali bila usumbufu.

Kufuatia agizo hilo la Waziri Mkuu, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu John, tawi la Dar es Salaam, Eston Ngilangwa, alisema limetolewa katika kipindi muafaka, ambacho Watanzania wamekuwa wakikabiliwa na changamoto lukuki zinazosababishwa na migogoro ya ardhi.

Alisema mamlaka husika, hususan halmashauri, licha ya kuanza kupima viwanja, bei zake ni kubwa na kusababisha wananchi wenye vipato vya chini kishindwa kuhimili.

Aliongeza kuwa ni muhimu kwa serikali kuandaa waraka maalumu wa kuziagiza halmashauri kupanga bei kulingana na pato la wananchi wa eneo husika.

No comments:

Post a Comment