UMOJA wa Vijana wa CCM (UVCCM) umesema baadhi ya wanasiasa
waliotaka Tanzania iwe na muundo unaofanana na Umoja wa Ulaya (EU),
walikusudia kuudhoofisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kutaka uvunjike
ili taifa lisambaratike.
Pia, alisema wanasiasa hao walilenga kuligawa taifa
na kuwagawa wananchi kwa kuondoa mshikamano uliopo.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka,
alisema hayo ofisini kwake jana, alipokuwa akitoa maoni yake baada ya Uingereza
kupiga kura ya kujitoa EU.
Shaka alisema muundo wa EU ni wa jumuia ya
kimaendelo na kwamba, hauna sura ya
kuwaweka watu katika mazingira na malengo ya kubeba maisha ya watu,
maendeleo, kuimarika kwa uchumi au kupigania ustawi wa amani ya pamoja.
Alisema kwa sababu ya mfumo huo kuwa dhaifu na
legelege au usio na masharti ya kudumisha umoja na
maisha ya watu wake kijamii, kisiasa, kiuchumi na
kiutamaduni, jambo linalofanya
mwanachama yeyote kutoka wakati wowote na wakati mwingine bila hata ya sababu
ya maana na ya msingi.
"Tuliwaambia mamluki na wasaka madaraka kwa
hila kwamba, muundo wa EU una mashaka, si imara kama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Marekani
(USA), Afrika Kusini au Uingereza (UK), lakini walibisha, sasa ni wazi
wanaaibika wanaposikia haya yanayoendelea kwa baadhi ya wanachama
kujiondoa,"alisema Shaka.
Alisisitiza kuwa katika dhamira njema inayoheshimu,
kulinda, kuhifadhi na kuendeleza maisha
ya watu kwa nyakati zote, ni rahisi kuuita muundo wa EU kuwa ni legelege na usio na dhamira ya dhati
kuwaunganisha watu wake.
Hata hivyo, Kaimu Katibu Mkuu Shaka, alisema UVCCM
kila zilipotolewa hoja na wanasiasa wa upinzani, hususan chama cha CUF, kutaka
muundo wa Muungamo wa Tanzania uwe kama EU, ilisimama kidete kupinga.
Alisema CCM hawakukaa kimya bali walikuwa wakiuchambua
muungano huo na kuonyesha athari zake na kuongeza kuwa, umejikita kushirikiana
katika nyanja za kiuchumi huku ukiwa
hauna kinga na msingi madhubuti wa kudumisha utaifa na umoja.
"Tutaendelea kuwaenzi, kuwasifu na kuwathamini
waasisi wetu, ambao wamefanikiwa kuliweka taifa letu pamoja kwa zaidi ya miaka
50 sasa. Tuna muungamo imara unaojali na kulinda maisha na umoja wa kimaendeleo
kwenye demokrasia, kisiasa na kiuchumi,"alisema.
Shaka alisema watu wa taifa moja wakiishi kwa
umoja, kushirikiana na kuhurumiana, lazima itambulike kuwa, jambo hilo
lilijengwa katika misingi imara na madhubuti isiyopaswa kuvunjwa.
"Kwa mfano Northern Island, Wales au Scotland
zinaweza kujitoa EU wakati wowote, lakini nina hakika watu wake hawafikirii
wala siamini kwamba watataka siku moja wajiweke kando na muungamo wa UK. Yawezekana
wapo wachache wanaoweza kufikiria kinyume, lakini hawawezi
kufanikiwa,"alisema.
Aidha, Shaka alisema nchi mbalimbali duniani
zinautamani Muungano wa Tanzania kwa vile ni wa kipekee kwa kuwa unaweza
kufananishwa na nchi chache duniani kama vile Ujerumani, Afrika Kusini,
Uingereza, Pakistan na Marekani ambao
wameweza kuwa na muungano wa kweli kwa ajili ya watu wote.
Maoni ya Shaka yamekuja siku chache baada ya Waziri
Mkuu wa Uingereza, David Cameron, kutangaza kujiuzulu baada ya serikali yake
kushindwa katika kura ya maoni ya kuendelea au kujitoa kwenye EU.
Cameron alifikia uamuzi huo baada ya kura za maoni
kuonyesha kuwa, wananchi waliotaka Uingereza ijitoe kwenye umoja huo ni
asilimia 52 dhidi ya 48 waliopinga.
Alisema hawezi kuendelea kuongoza nchi hiyo huku
ikiwa nje ya umoja huo, ambapo kwa hisia kali, Cameron alisema anakubali
matokeo ya kujitoa kwenye umoja huo huku akisema kilichofanyika ni jambo la kidemokrasia.
No comments:
Post a Comment