SERIKALI imewataka waislamu kutunza amani nchini ili kutimiza yale yaliyoandikwa katika kitabu cha dini.
Pia, wametakiwa kusuluhisha pale wanapoona amani inatoweka ili Tanzania iendelee kuwa nchi yenye amani na utulivu kama ilivyo hivi sasa.
Akizungumza kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli, wakati wa futari iliyoandaliwa na Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Makamu wa Rais, Samia Suluhu alisema hakuna chochote kitakachofanyika kama nchi haitakuwa na amani.
“Waislamu wenzangu mnatakiwa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali za kuhubiri amani katika nchi ili kuweza kufikia malengo tuliojiwekea,” alisema Samia.
Aliongeza kuwa suala la amani ni jukumu la waislamu kuanza kuimarisha na wengine kufuata.
Hata hivyo, aliipongeza Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam, ambayo imekuwa ikilinda amani na kusisitiza amani kila wakati.
Samia alisema serikali itakuwa pamoja waislamu katika kutatua changamoto zinazowakabili kwani wana mzigo mzito mbele yao, lakini watahakikisha kwamba wanafikia malengo yote waliyojipangia hasa ya kuleta amani nchini.
Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir, alisema wana matumaini kwamba umoja ukijengwa, nchi inaweza kufikia malengo ya kukuza uchumi na kuleta amani kwa ujumla.
Hata hivyo, Mufti Zubeir aliwataka waislamu kujitokeza BAKWATA kwa ajili ya kutoa mawazo tofauti, lengo likiwa ni kujenga baraza hilo.
“Sisi ni watumwa wa watu, tunataka tuwatumikie kwa kuwaunganisha katika umoja, mshikamano na amani, leteni fikra zenu ni muhimu sana katika kujenga baraza,”alisema.
Alisema wao kama viongozi wa dini, wataendelea kuhutubia amani ili kuziba mianya ya machafuko katika nchi, huku akiwataka waislamu kuhakikisha kwamba wanaunga mkono jitihada za serikali ili kufikia malengo.
Kwa upande wake, Sheikh Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhadi Mussa, alisema mwaka huu, sikukuu ya Idi-El-Fitr kitaifa itasaliwa mkoani Dar es Salaam, kati ya tarehe sita au saba kutegemea mwandamo wa mwezi.
Alisema sala hiyo itasaliwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja na Baraza la Iddi litafanyika kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais John Magufuli.
No comments:
Post a Comment