Sunday 10 July 2016
TCRA YAAKUNJUA MAKUCHA, YAZITOZA FAINI KAMPUNI SITA ZA SIMU
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imezipiga faini kampuni sita za simu na kuzitaka zilipe sh. milioni 649, kabla ya Julai 30, mwaka huu.
Hatua hiyo inatokana na kampuni hizo kukiuka masharti ya usajili wa laini za simu za mkononi.
Mbali na hatua hiyo, TCRA pia imezitaka kampuni hizo kuwasilisha orodha iliyohakikiwa ya mawakala wa kusambaza na kuuza laini za simu nchini ifikapo Julai 15, mwaka huu.
Tamko hilo lilitolewa Dar es Salaam, jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema hatua hiyo inafuatia kampuni hizo kukiuka masharti ya usajili wa namba au laini za simu za mkononi.
Kilaba alizitaja kampuni hizo kuwa ni Airtel Tanzania Limited, Benson Informatics Limited (Smart), MIC Tanzania Limited (TIGO), Viettel Tanzania Limited (Halotel), Vodacom Tanzania Limited na Zanzibar Telecon Limited (Zantel).
"Kampuni hizo zimekiuka masharti ya usajili wa laini na matumizi ya laini kama yalivyoainishwa na sheria ya mawasiliano ya kielektroniki na posta ya mwaka 2010 na kanuni ya mawasiliano ya kielektroniki na posta ya mwaka 2011," alisema.
Aliyataja maeneo yaliyogungulika kuwepo na ukiukwaji wa usajili wa laini za simu kuwa ni namba kutolewa bila mteja kutakiwa kusajiliwa, namba kusajiliwa kwa majina, vitambulisho na nyaraka za watu wengine, namba kutofungwa hadi usajili kukamilika na namba kusajiliwa usajili wa awali.
Kilaba alisema Airtel Tanzania inatakilwa kuilipa TCRA sh. millioni
182,500 kabla ya Julai 30, mwaka huu, ambapo sh. milioni 74 ni faini kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 148 bila kutumia kitambulisho halisi cha mnunuzi, sh. milioni 33,500 kwa kuruhusu laini 67, ziuzwe bila kujaza fomu za usajili, sh. milioni 32,500 kwa kuruhusu laini 65 ziwashwe kabla ya kuuzwa na sh. milioni 42, 500 kwa kuruhusu laini 85 zifanyiwe usajili wa awali na kutumika kwenye mtandao wake.
Alisema SMART inatakiwa kulipa sh. milioni 17, ambapo sh. milioni saba kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 14 bila kutumia kitambulisho halisi cha mnunuzi, sh. milioni saba kwa kuruhusu laini 14 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili na sh. milioni tatu kwa kuruhusu laini sita ziwashwe kabla ya kuuzwa.
TIGO inatakiwa kulipa sh. milioni 189, ambapo sh. milioni 93,500, kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 187 bila kutumia kitambulisho, sh. milioni 43,500, kwa kuruhusu laini 87 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili, sh. milioni 41 kwa kuruhusu laini 82 ziwashwe kabla ya kuuzwa na sh. milioni 11 kwa kuruhusu laini 22 zifanyiwe usajili wa awali na kutumika kwenye mtandao wake.
Kampuni ya Halotel inatakiwa kulipa sh. milioni 107, ambapo sh. milioni 36 kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 73, bila kutumia kitambulisho, sh. milioni 36, kwa kuruhusu laini 72 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili, sh. milioni 34, kwa kuruhusu laini 82 ziwashwe kabla ya kuuzwa.
Vodacom inatakiwa kulipa sh. milioni 96, ambapo sh. milioni 49, kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 98 bila kutumia kitambulisho, sh. milioni 24, kwa kuruhusu laini 48 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili, sh. millioni 19, kwa kuruhusu laini 38 ziwashwe kabla ya kuuzwa na sh. milioni 4.5 kwa kuruhusu laini tisa zifanyiwe usajili wa awali na kutumika wenye mtandao wake.
Aidha, Zantel inatakiwa kulipa sh. milioni 57, ambapo sh. milioni 36.5, kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 73 bila kutumia kitambulisho, sh. milioni 11.5 kwa kuruhusu laini 23 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili, sh. milioni saba kwa kuruhusu laini 14 ziwashwe kabla ya kuuzwa na sh. milioni mbili kwa kuruhusu laini nne zifanyiwe usajili wa awali na kutumika kwenye mtandao wake.
Kilaba aliwataka watoa huduma hao kuacha kuwatumia mawakala wasioruhusiwa kuuza au kusambaza laini za simu nchini na kuzima
laini zote zilizopo sokoni, ambazo zimewashwa na kuhakikisha wanawasilisha taarifa ya utekelezaji wa TCRA ndani ya siku saba, kuanzia tarehe walizopokea uamuzi huo.
Alionya kuwa mtoa huduma atakayekaidi utekelezaji huo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake, ikiwa ni pamoja na kushitakiwa kwa makosa ya jinai.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment