Sunday 10 July 2016

SILAHA NYINGI ZINAMILIKIWA NA WATU WASIOKUWA NA SIFA-KAMANDA SIRRO

KAMANDA wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema uhakiki wa silaha kwa mikoa ya kipolisi ya Kinondoni, Temeke na Ilala kuanzia Machi Mosi, mwaka huu, ulikuwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ya baadhi ya wamiliki kutokuwa na sifa za kuendelea kuzimiliki.

Alisema katika uhakiki huo, ilibainika kwamba baadhi ya wamiliki wana umri mkubwa zaidi ya miaka 70 na kuugua magonjwa mbalimbali kama kupooza, jambo ambalo kiusalama linamfanya mmiliki huyo kutokuwa na sifa za kuendelea kuwa nayo.

Alisema changamoto nyingine ni baadhi ya wamiliki kufariki na kuacha silaha hizo kwa ndugu zao, ambao wameshindwa kuzisalimisha na kutozilipia.

Alisema waliohakiki silaha mkoa wa Kinondoni ni watu 600 na aina ya silaha hizo ni Pistol 2,619, shortgun 1,153 na Rifle 491. Jumla ya silaha zilizohakikiwa ni 4,763.

Kwa upande wa Ilala, waliohakiki silaha ni 3,017 na aina ya silaha hizo ni Pistol 2,877, shortgun 1,467 na Rifle 406. Jumla ya silaha zilizohakikiwa ni 5,215.

Kwa upande wa Ilala,  watu waliohakiki silaha ni 2,310, ambazo ni aina ya Pistol 2,310, shortgun 873 na Rifile 674, ambapo jumla ya silaha zilizohakikiwa ni 5,530.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu limempongeza mwanamke, aliyepambana na majambazi baada ya kuvamiwa dukani kwake na kufanikiwa kuwanyang'anya bunduki aina ya SMG.

Kamanda Sirro alisema jana kuwa, mwanamke huyo alivamiwa na watu hao dukani kwake maeneo ya Buguruni, Dar es Salaam na kumpora sh. 420,000.

Alisema kwa kutumia mbinu zake binafsi, aliwagonga majambazi hao kwa gari lake, ambapo walifanikiwa kukimbia na kuacha bunduki waliyokuwa nayo aina ya SMG, ikiwa na risasi 11.

Katika hatua nyingine, Kamanda Sirro alisema wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 400 wa makosa mbalimbali, ikiwemo unyang'anyi wa kutumia nguvu, kufungua baa kabla ya muda, kukutwa wakinywa pombe muda wa kazi, kucheza kamari, kubugudhi abiria, kuvunja na kuiba.

Makosa mengine ni kupatikana na bangi, uzembe na uzururaji na kutoa lugha ya matusi. Alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, katika oparesheni safisha jiji inayoendelea.

No comments:

Post a Comment