Sunday 10 July 2016

KAMPUNI TATU ZA MABASI ZAFUNGIWA


KIKOSI cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), wamezifungia kutoa huduza za usafiri kampuni tatu za mabasi yaendayo mikoani, ikiwemo City Boys.

Kampuni zingine zlizofungiwa ni Super Samy na OTA, ambazo zimehusika katika ajali tatu katika kipindi cha wiki moja na kusababisha vifo vya  watu 46 na majeruhi 73.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga, alisema uchunguzi wa awali kuhusu ajali hizo umebaini zilichangiwa na uzembe wa madereva pamoja na mwendokasi.

Kamanda Mpinga alisema madereva wamekuwa wakikiuka kwa makusudi sheria inayowataka kuendesha kwa mwendo usiozidi kilomita 80 kwa saa.

Alisema matukio hayo ya ajali yalitokea siku tofauti, ambapo Juni 28, mwaka huu, saa 8 usiku, wilayani Misungwi mkoani Mwanza, basi la Kampuni ya Super Samy, likitokea Shinyanga kwenda Mwanza, liliacha njia na kupinduka na kusababisha vifo vya watu watano na majeruhi 13.

Aidha, Julai Mosi, mwaka huu, saa 6 mchana, maeneo ya Veta Dakawa, katika barabara ya Dodoma/Morogoro, maroli  mawili yaligongana na kuwaka moto na kusababisha vifo vya watu watano. Pia katika eneo hilo, basi la kampuni ya OTA lilipata ajali na kusababisha vifo vya watu sita na majeruhi sita.

Kamanda Mpinga alisema pia kuwa Julai 4, mwaka huu, saa 8 mchana, maeneo ya Maweni Kintiku mkoani Singida, mabasi mawili ya kampuni ya City Boys, yaligongana na kusababisha vifo vya watu 30 na majeruhi 54, ambapo hadi sasa wamebaki majeruhi 33, wakiendelea na matibabu na kati yao, saba wapo katika hali mbaya katika Hospitali ya mkoa wa Dodoma.

Mbali na kuzifungia kampuni hizo, Kamanda Mpinga alisema madereva waliosababisha ajali hizo kwa uzembe, wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.

Akitoa tathmini ya jumla kuhusu ajali hizo, alisema zinachangiwa na baadhi ya abiria kushabikia mwendokasi na wale wanaochukia kutotoa taarifa kwa trafiki.

Kamanda Mpinga aliwataka wazazi na walezi, wahakikishe wanawalinda watoto wao wanapokuwa matembezini huku akiwataka madereva na watumiaji wa barabara kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.

No comments:

Post a Comment