Sunday 10 July 2016

KITWANGA ATOA YA MOYONI

MBUNGE wa Misungwi, Charles Kitwanga, amerudi jimboni na kutoa ya moyoni akivitaka vyombo vya habari viache’ longolongo’ kumhusisha na sakata la Lugumi, wakati kuna Mawaziri wa Mambo ya Ndani ya nchi waliomtangulia.

Amesema japokuwa yeye ni mmoja wa waanzilishi wa kampuni ya Infosys nchini hapa, lakini kampuni hiyo haihusiani na Lugumi katika suala lolote, haijafanya kazi na polisi au Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na yeye hajui mambo ya Lugumi.

Kitwanga ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kabla ya uteuzi wake kutenguliwa na Rais Dk. John Magufuli na nafasi yake kushikwa na Mwigulu Nchemba, alisema hayo jana nyumbani kwake wakati akizungumza na waandishi wa habari.

“Nimerudi jimboni kwa ajili ya kufanya kazi za jimbo, ndicho hicho nilichochaguliwa na wananchi wa Misungwi kufanya,” alisema Kitwanga na kudai kuwa sasa atakaa jimboni kwa muda mrefu kuliko awali, ambapo alikuwa na majukumu mengi ya kitaifa.

“Watu mlikuwa mnazungumza mambo mengi ambayo sikuyaelewa,angalieni  lini nilikuwa Wizara ya Mambo ya Ndani, mimi ni Waziri wa ngapi katika wizara hiyo toka 2011, mkifanya utafiti mtaelewa mnapotosha Watanzania, waulizeni mawaziri wa nyuma tuache longolongo,” alieleza.

Alifafanua “ Infosysni ni ajenti wa Dell ambayo ni Kampuni ya Marekani ni kubwa duniani na namba moja ya kuuza PC, Lugumi aliingia mkataba na Biometric ya USA ambao walinunua vifaa vya Dell, Dell wakawambia anayetufungia vifaa hivyo ni Infosys,”alisema.

Alidai kazi ya Infosys ilikuwa ni kuhakikisha vifaa vya Dell vimefika salama vifungwe, Polisi ndiyo ilikuwa na mkataba na Lugumi kupitia Biometric, hivyo kumhusisha yeye na sakata la Lugumi wakati Infosys haikufanya kazi na Lugumi ni kumchafua.

Alizidi kutoboa kwamba hadi Agosti mwaka 2010, alikuwa na asilimia 33 ya hisa kwenye Kampuni ya Infosys, lakini kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huo, alimwuuzia hisa hizo Lubanga Kitwanga.

“Fanyeni utafiti wa kina na kuandika ukweli juu ya sakata hilo, vinginevyo mtaendelea kupotosha Watanzania, kampuni yoyote inayofanya kazi halali imesajiliwa, angalieni BRELA mtapata Lugumi ni ya nani,” alisisitiza Kitwanga na kudai akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani hakuwahi kuona nyaraka yoyote ya Lugumi mezani kwake.

Akizungumzia kutenguliwa kwa uteuzi wake baada ya kuingia bungeni na kujibu swali akiwa amelewa, Kitwanga alisema anampongeza sana Rais John Magufuli kwa uadilifu, umakini na uchapa kazi wake hodari, hivyo kamwe hawezi kuhoji alichoamua rais.

Akijibu swali kwa nini alienda Israel baada ya kutenguliwa, alisema yote hayo ni longolongo za kumchafua. “Sina uhakika kuna aliyeangalia pasipoti yangu akaona nilienda wapi na nilitoka wapi, chunguzeni kwanza.”

Akizungumza na wananchi wa mji wa Misungwi jana baada ya kuzungumza na waandishi, Kitwanga alisema dhambi kubwa atakayochukiwa na ‘mchwa’ wa wilaya hiyo ni kusimamia kila fedha ili ziwafikie wananchi wake na kuwaletea maendeleo.

Alishangiliwa na wananchi lukuki waliofika kumlaki kwenye uwanja wa stendi ya mabasi aliposema:  “Nyanza yetu lazima irudi, waliokula hela za Nyanza, wakiwemo vigogo waliomo wilayani Misungwi, wajiandae, mahakama ya mafisadi iko mbioni,”

Waziri huyo wa zamani alisema serikali ya awamu ya tano itaendelea kuboresha huduma za afya, miundombinu ya barabara, maji, kuinua wajasiriamali, wakiwemo vijana na wanawake.

Mbunge huyo alitoa magodoro 150 kwa ajili ya hospitali ya wilaya na zahanati mbalimbali za kata, 'Composer' moja, vyerhehani 10, moja na mashine ya kuchomea vyuma kwa vikundi mbalimbali vya wanawake na vijana wajasiriamali wa wilayani humo, vyote vikiwa na thamani ya sh ml 9.1.

No comments:

Post a Comment