Sunday, 10 July 2016

WAFANYABIASHARA MAARUFU ARUSHA WATIWA MBARONI

KIKOSI maalum cha polisi nchini kutoka makao makuu ya polisi,  kimewatia mbaroni  wafanyabiashara wanne maarufu wa jijini hapa, wakituhumiwa kuiibia serikali mamilioni ya fedha.

Baadhi ya vigogo (majina tunayo)  ni wale wanadaiwa kuiibia serikali fedha kupitia mashine za EFD, ambapo kampuni zao zilihusika kuingiza nchini mashine hizo.

Taarifa kutoka ndani ya jeshi la polisi zilisema wafanyabiashara hao miongoni mwao wako Watanzania wawili wenye asili ya kiasia na wawili wenye kujihusisha na biashara ya ukandarasi.

Hivi karibuni Rais John Magufuli aliutangazia umma kuwa tayari vyombo vya usalama vimepata taarifa za kuwepo kwa wafanyabiashara wanaoingiza sh. milioni saba kwa kila dakika na kwamba vyombo vya usalama vilikuwa vikiwafuatilia watuhumiwa hao.

Taarifa zaidi zilidai kuwa mara baada ya watuhumiwa hao kukamatwa juzi na kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi Arusha jana na kuhojiwa kwa zaidi ya saa nane,  walisafirishwa kwa magari maalum kwenda Dar es Salaam.

Hata hivyo, taarifa za kukamatwa kwa watuhumiwa hao zinaelezwa kuwa za siri, hivyo muda ambao walisafirishwa haukuweza kujulikana, licha ya ndugu wa watuhumiwa hao kujaribu kuwanasua ndugu zao bila mafanikio.

Hakuna kiongozi yeyote wa polisi aliyekuwa tayari kuzungumzia sakata la kukamatwa kwa wafanyabiashara hao maarufu jijini Arusha na kwamba wenye mamlaka ya kuzungumzia hilo ni viongozi wa kitaifa pekee.

Kukamtwa kwa wafanyabiashara hao wakubwa jijini hapa kumezua gumzo zito kila kona ya mji kwa kuwa waliamini kwamba ni vigumu vigogo hao kutiwa mbaroni kutokana na kuwa na fedha nyingi.

Habari zaidi zilisema uchunguzi kuhusiana na sakata hilo unaendelea kufanyika karibu katika kila kona ya nchi na kwamba kuna uwezekano wahusika wengi wakakamatwa na kutakiwa kulipa fedha za kodi waliyokwepa.

No comments:

Post a Comment