Thursday, 5 January 2017

ABAMBWA NA POLISI AKIFUKUA KABURI LA ALBINO

MKAZI wa Chapakazi, mkoani Mbeya, Jonas John (28), amekamatwa na polisi akiwa anafukua kaburi la marehemu Sista Osisara, aliyefariki miaka sita iliyopita, ambaye alikuwa mlemavu wa ngozi.

John, alikutwa akifukua kaburi la marehemu Osisara, aliyefariki mwaka 2010, kwa lengo la kuchukua viungo vyake vya mwili.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Dhahiri Kidavashari, alisema lilitokea jana, saa saba usiku, katika kijiji cha Mumba, kilichoko kata ya Ilembo, wilaya ya Mbeya.

Aliongeza kuwa, mtuhumiwa alikuwa na wenzake wawili, ambao walifanikiwa kukimbia.

“Marehemu Osisara, ambaye alikuwa ni mlemavu wa ngozi, alifariki dunia mwaka 2010, kwa ugonjwa wa homa, ambapo alizikwa katika makaburi yaliyoko kijiji cha Muumba,” alisema Kidavashari.

Alisema John alikutwa akiwa na majembe na koleo, ambavyo walikuwa wakitumia kufukulia kaburi hilo na kwamba, baada ya kumhoji, aliwataja washirika wenzake wawili waliofanikiwa kukimbia.

Kidavashari alisema msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa hao waliokimbia unaendelea ili kuwaunganisha na mtuhumiwa wa kwanza anayeendelea kushikiliwa na polisi.

“Jamii inatakiwa kuachana na tamaa ya kupata mali kwa kupitia njia zisizo halali kwani polisi hawataruhusu wala kufumbia macho vitendo kama hivyo. Watu wanatakiwa wajishughulishe na kazi halali kwa lengo la kujipatia kipato halali kuendesha maisha yao,” alisema Kidavashari.

Taarifa zaidi zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa, mtuhumiwa akiwa na wenzake wawili, walianza kufukua kaburi hilo usiku wa kuamkia jana.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Julius Kibona, alisema watuhumiwa hao walipoufikia mwili wa marehemu, ndugu zake wanaoishi jirani na makaburi hayo, walishtuka na kuanza kupiga mayowe ya kuomba msaada.

“Wenzake walifanikiwa kukimbia, lakini yeye alishindwa kwani alikuwa ndani ya kaburi, hivyo alikamatwa na wananchi waliojitokeza kwa wingi baada ya kusikia kelele za kuomba msaada,” alisema Kibona.

Aliongeza kuwa wananchi hao wakiwa na hasira,walimtoa John ndani ya kaburi hilo na kuanza kumshambulia kwa kipigo kikali hadi polisi walipofika na kufanikiwa kumuokoa.

No comments:

Post a Comment