Thursday, 5 January 2017

MKURUGENZI, DIWANI WAZICHAPA KAVU KAVU



KIKAO cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, kimeingia dosari baada ya kujitokeza majibizano makali baina ya Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mashaka Mbilinyi na Diwani wa Kata ya Kibaoni, Gudlucky Msowoya.

Hali hiyo ilisababisha Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Francis Ndulane, kurushiana makonde na diwani huyo.

Tukio hilo lilitokea jana, wakati wa uchangiaji hoja mbalimbali, ambapo Msowoya baada ya kupewa nafasi, alianza kumshushia shutuma mwenyekiti huyo, akidai kuwa anapindisha sheria, hivyo alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Francis Ihunyo, kuingilia kati.

Wakati akiendelea kuchangia, Mbilinyi alimtaka diwani huyo kukaa chini, lakini alikaidi amri hiyo, ndipo alipomuagiza mkurugenzi amtoe nje.

Diwani huyo aligoma kutoka nje, akisema mwenyekiti hana mamlaka ya kumtoa ukumbini, hali iliyosababisha mwenyekiti kuahirisha kikao hadi diwani huyo atakapotoka nje.

Wakati kikao kikiwa kimeahirishwa, madiwani na wageni walikwenda kupata chakula, ambapo mkurugenzi alitaka kutumia muda huo kuzungumza na diwani huyo.

Ghafla, aliposogea kwenye meza ya Msowoya ili kuzungumza naye, kwa hasira diwani huyo alimrushia mkurugenzi sahani iliyokuwa na chakula, hivyo kuzua tafrani kwa viongozi hao kuanza kurushiana makonde.

Iliwalazimu madiwani wengine kuingilia kati ili kuamulia ugomvi huo huku mkuu wa wilaya akiomba msaada wa polisi kutuliza tafrani iliyojitokeza.

Akizungumza na gazeti hili, Msowoya alisema mwenyekiti wa halmashauri hiyo aliendesha kikao kwa upendeleo, hususan kwa madiwani wenzake wa CHADEMA, kwa kuzuia hoja za msingi zinazowasilishwa na madiwani wa CCM.

Alipohojiwa kuhusu sababu ya kurusha sahani, alisema alikuwa na hasira, hivyo hakutaka kumsikiliza mkurugenzi huyo kwa sababu siku zote yupo upande wa mwenyekiti.

No comments:

Post a Comment