Thursday, 5 January 2017

CHADEMA, CUF WAZIDI KUVURUGANA

HATUA ya CHADEMA kuwasimamisha wagombea wake katika uchaguzi mdogo wa udiwani, imeanza kuchafua hali ya hewa ndani ya CUF na kutibua makubaliano kati yao.

Aidha, uongozi wa CUF umedai kuwa ukata ndani ya chama hicho umeendelea kukitafuna na kusababisha kuchelewa kufanya kampeni za uchaguzi huo mdogo.

Mbali na hilo, baadhi ya wasomi na wanasiasa wamesema kuwa, kitendo cha CUF kutangaza kususia kushiriki kwenye sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi, hakuwezi kuathiri hali ya kisiasa Zanzibar.

Akizungumza jana, Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo, alisema wameshangazwa na kitendo cha CHADEMA kusimamisha wagombea wake kinyume na makubaliano.

Mketo alisema hadi sasa bado kuna mvutano kati ya vyama hivyo, ambapo awali walikubaliana kuachiana kata za kugombea kwenye uchaguzi huo mdogo.

“Awali, makubaliano hayo yaliitaka CUF kusimamisha wagombea katika kata nne, ambazo ni Kijichi, Nkome, Kimani na Malta zilizoko Mwanza, lakini cha kushangaza ni kuona CHADEMA imesimamisha kila kata kinyume na makubaliano,”alifafanua Mketo.

Aliongeza kuwa, makubaliano yalikuwa kuachiana kwenye kata, ambazo chama husika kina ushawishi wa kushinda na kwamba, CHADEMA imesimamisha wagombea wake kwenye kata 21.

Kwa upande wake, Msemaji wa CUF, Mbarala Maharagande, alisema kuchelewa kufanya kampeni katika uchaguzi huo mdogo kunatokana na ukata wa fedha na mvutano huo.

“Ni kweli bado hatujaanza kufanya kampeni, ila tupo kwenye maandalizi na tunatarajia kuzindua Januari 8, mwaka huu, katika jimbo la Dimani na kwenye maeneo mengine,”alisema msemaji huyo. 

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alizuia ruzuku ya CUF ya zaidi ya sh. milioni 460, tangu Agosti, mwaka jana hadi watakapomaliza mgogoro wa ndani ya chama hicho.

Katika hatua nyingine, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Saalam, Dk. Benson Bana, amesema kitendo cha CUF kutoshiriki kwenye Sherehe za Mapinduzi, hakitaathiri  hali ya kisiasa Zanzibar.

Dk. Bana alisema jana kuwa, CUF kutoshiriki kwenye sherehe hizo hakutapunguza wala kuongeza kitu na kwamba, historia ya kumbukumbu ya mapinduzi hayo inabaki palepale.

“Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad, anapinga na kudai kuwa haitambui serikali ya Rais Dk. Mohammed Shein wala sherehe hizo, huku akitumia na kula fedha za serikali,”alisema Dk. Bana.

Mwenyekiti Taifa wa UPDP, Fahmi Dovutwa, alisema  kitendo hicho sio kigeni kwa CUF na kwamba, hata msimamo wa chama hicho ni kupinga mapinduzi.

Dovutwa alisema kitendo hicho hakitaathiri chochote na kwamba, mwaka 1995, CUF waliingia na vitambaa vyeusi wakimaanisha ni msiba.

“Kutohudhuria kwa CUF, hakutaathiri kitu chochote kutokana na kuwa serikali iliyopo sasa iko kisheria na kikatiba na kama alivyotangaza Dk. Shein, hali ya kisiasa iko shwari,”alisema.

Januari 4, mwaka huu, CUF ilitangaza msimamo wa kususia sherehe hizo huku wakidai kutomtambua Dk. Shein kuwa Rais.

Kilele cha Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar, ni  Januari 12, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Amaan, Unguja.

No comments:

Post a Comment