Wednesday, 4 January 2017
DC ILALA AAGIZA WANAOKATAA KUFANYA USAFI WAKAMATWE
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, amewaagiza viongozi wa serikali za mitaa na polisi, kuwakamata wale wote wanaokataa kushiriki usafi au kulipa fedha za uzoaji taka katika maeneo yao.
Aidha, amesema watatumia nguvu kuwafanyisha usafi wale wote, ambao wanasita kushiriki katika kazi ya usafi na kuwatia mbaroni watakaoshawishi wenzao kugoma kufanya hivyo.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa agizo hilo juzi, wakati alipoongoza wananchi wa kata ya Vingunguti, kufanya usafi katika mtaa wa Kombo, wilayani humo.
Alisema mwaka 2017, hautakuwa wa lelemama katika suala zima la usafi, hivyo aliwaonya wananchi wenye tabia za kukaidi, kutegea, kupuuza na kushawishi wenzao kutoshiriki, waache mara moja.
“Katika wilaya yangu, sikubali kutokea mlipuko wa kipindupindu. Nataka kila mmoja ashiriki kufanya usafi. Wale ambao watakaidi, tutawalazimisha kufanya usafi,” alisema Sophia.
Aliongeza: “ Na kwa wale ambao hawataki kufanya hivyo, tutalala nao. Watakumbana na mkono wa sheria.”
Aliwataka wananchi kulipa fedha za kuzolea taka na kusafisha maeneo yao kwa faida yao binafsi na jamii kwa ujumla.
Katika kudhihirisha kwamba hakuwa na mzaha katika jambo hilo, Sophia aliwaita polisi katika eneo hilo na kuwaagiza kuwakamata wananchi, ambao hawakujitokeza kushirikiana naye katika usafi.
Kufuatia hali hiyo, wananchi walianza kujitokeza kwa wingi kushiriki kufanya usafi kwa kuhofia kutiwa mbaroni.
Diwani wa kata hiyo, Omari Kumbilamoto, alisema bado mwamko ni mdogo kwa wananchi kushiriki katika masuala ya usafi.
“Nampongeza mkuu wa wilaya kwa kufika na kutoa maagizo hayo ili wananchi waweze kutambua wajibu wao katika suala zima la kushiriki katika kufanya usafi,”alisema Kumbilamoto.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kombo, Juma Mpate, alisema katika kutii agizo hilo la mkuu wa wilaya, kuanzia Jumamosi ijayo, ataomba jeshi la polisi kufika katika mtaa huo ili kusimamia wananchi kufanya usafi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment