Wednesday, 4 January 2017

KUBENEA AOMBA KUFUTIWA MASHITAKA



MBUNGE wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea (CHADEMA), anayedaiwa kutangaza habari za uongo kupitia gazeti la MwanaHalisi, ameiomba mahakama kuitupilia mbali hati ya mashitaka na kumwachia huru kwa kuwa hati ya mashitaka ina upungufu kisheria.

Kubenea, aliwasilisha maombi hayo jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kupitia kwa mawakili wake waliokuwa wakiwasilisha hoja za awali kupinga hati ya mashitaka.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbroad Mashauri, mawakili wa Kubenea wakiongozwa na Jeremiah Ntobesya, waliiomba mahakama hiyo itupilie mbali hati ya mashitaka kwa kuwa ina upungufu kisheria.

Akiwasilisha hoja hizo, Wakili Ntobesya alidai hati hiyo ya mashitaka inakinzana na matakwa ya sheria kifungu cha 36 (1) cha Sheria ya Magazeti na kifungu cha  132 cha  Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Alidai hati hiyo imewekwa maneno, ambayo hayapo katika kifungu, ambacho mshitakiwa anadaiwa kukiuka na maelezo ya kosa hayajitoshelezi kumwezesha mshitakiwa kuelewa aina ya kosa linalomkabili.

“Kutokana na hati ya mashitaka kuwa na upungufu, tunaiomba mahakama iitupilie mbali kutoka katika kumbukumbu zake na mshitakiwa aachiwe huru ili aendelee na shughuli zake za kujenga taifa,” waliomba.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali, Dereck  Mkabatunzi, aliiomba mahakama kutupilia mbali mapingamizi hayo kwa kuwa hayana mashiko kisheria.

Dereck alidai hakuna maneno mapya yaliyoingizwa katika hati ya mashitaka kwa kuwa maneno yaliyoko kwenye kifungu cha 36 (1) cha Sheria ya Magazeti, ndiyo yaliyotumiwa katika hati hiyo.

Pia, alidai maelezo ya kosa yaliyoko katika hati ya mashitaka, yanajitosheleza kwa mshitakiwa kuweza kutambua kosa analoshitakiwa nalo na hata watu wengine kuelewa kile mshitakiwa anachoshitakiwa.

“Mashitaka yanakidhi matakwa ya kisheria, tunaona hoja za upande wa utetezi hazina mashiko, hivyo tunaomba zitupiliwe mbali,” aliomba.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Mashauri aliahirisha shauri hilo hadi Januari 25, mwaka huu, litakapokuja kwa uamuzi na kusema dhamana ya mshitakiwa inaendelea.

Kubenea anadaiwa kusambaza habari ya uongo yenye kichwa cha habari 'Yuko wapi atakayeiyokoa Zanzibar'.

Anadaiwa kutenda kosa hilo, Julai 25,mwaka jana,  katika Mtaa wa Kasaba, Wilaya ya Kinondoni, ambapo alisambaza habari ya uongo kwenye gazeti la MwanaHalisi  la kati ya Julai 25-31,2016,  toleo namba 349, ISSN 1821-5432, lenye kichwa hicho cha habari.

Inadaiwa habari ama makala hiyo ingeweza kusababisha  hofu kwa jamii ama kuharibu hali ya amani.

No comments:

Post a Comment