Wednesday, 4 January 2017
WALIOPORA MIL. 25/- DAR WATIWA MBARONI
POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inawashikilia watu waliohusika na tukio la ujambazi wa sh. milioni 25, lilitokea juzi eneo la TAZARA, Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa jana na Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, ilisema watu hao walikamatwa na wapo kituoni kwa ajili ya kuhojiwa.
“Tumefanikiwa kuwakamata baadhi ya watu waliojihusisha na tukio la ujambazi maeneo ya TAZARA na wako kituoni, ambapo polisi wako nao kwa ajili ya kuwahoji ili kujua lengo la wizi huo,” alisema.
Sirro alisema wizi huo ulifanyika eneo hilo bila mlio wowote wa bunduki, jambo lililosababisha polisi kushindwa kutambua tukio hilo mapema.
Alisema watu hao walivunja kioo cha gari la mmiliki wa kampuni inayotengeneza mabati ya Sun Shine na kufanikiwa kuiba fedha hizo.
Sirro alisema upelelezi bado unaendelea ili kuwabaini watu wengine waliohusika na uporaji wa fedha hizo na ukikamilika, watawafikisha mahakamani.
Wizi huo ulitokea juzi, saa nne asubuhi, wakati gari hilo likiwa kwenye foleni ya magari eneo la TAZARA.
Majambazi hao walipora fedha hizo wakiwa katika eneo hilo huku askari waliokuwa doria wakiwa wametanda wakikamata pikipiki zilizokuwa zikitoka eneo la Buguruni.
Ilielezwa kuwa watu waliokuwa kwenye gari walikuwa wakipeleka fedha hizo benki pasipokuwa na ulinzi wa polisi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment