Wednesday, 4 January 2017

AGIZO LA RAIS MAGUFULI LAWAKUMBA WATUMISHI WATATU KAGERA



SERIKALI mkoani Kagera imetekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli la kuwachukulia hatua watumishi wa manispaa waliohusika katika ukarabati wa majengo ya shule ya sekondari ya Omumwani, ambayo yameonekana kutoendana na thamani ya fedha iliyotumika.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo juzi, wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani hapa, ambapo alitembelea shule hiyo na kukagua majengo yanayokarabatiwa na serikali kwa ajili ya kuwahifadhi wanafunzi waliotoka katika shule mbili zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi, lililotokea Septemba 10, mwaka jana.

Akiwa shuleni hapo, Rais Dk. Magufuli alisema hakuridhishwa na ukarabati huo kwa kuwa haulingani na fedha iliyotumika.

“Nimetembelea majengo haya, sijaridhika na ukarabati uliofanyika, nimekaa katika kitengo cha ujenzi muda mrefu, najua viwango vya ujenzi vilivyofanyika hapa haviendani na fedha iliyotumika.

"Pia, katika taarifa yenu, mmenieleza kuwa zimeshatumika shilingi  milioni 119, wakati katika uchunguzi wangu, nimegundua zimetumika shilingi milioni 172, hivyo naagiza Kamati ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, kufuatilia kila senti iliyotumika hapa ilifanya nini na nipate majibu haraka,”aliagiza Rais Magufuli.

Agizo hilo limetekelezwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Diwani Athumani, baada ya kufanya ukaguzi wa majengo hayo, ikiwemo miundombinu ya maji, ambayo ilikarabatiwa kwa ajili ya kuwapa hifadhi ya muda wanafunzi wa shule za Ihungo na Nyakato, zilizoathiriwa na tetemeko hilo.

Athumani, baada ya ukaguzi huo, alimtaka Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Chibunu Lukiko, kumtajia majina ya watumishi waliohusika moja kwa moja katika usimamizi wa kila siku wa shughuli hiyo.

Alisema ametazama kwa macho na kugundua kuwa kazi hiyo iko chini ya kiwango na kwamba, haiendani na thamani ya sh. milioni 119, zilizotolewa na serikali.

“Kwa nini wakurugenzi hampendi kufuatilia kwa karibu miradi iliyoko katika maeneo yenu ili kujiridhisha na kujua kinachoendelea. Kama mgefuatilia mapema, mngegundua hali hii kabla na kuirekebisha.

"Naagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, uwasimamishe watumishi waliohusika, ambao ni Mhandisi Kitengo cha Ujenzi Manispaa ya Bukoba, Andondile Mwakitalu, Mhandisi Msaidizi, Costane Felix na Fundi, Charles Kafumu ili wapishe uchunguzi, ambao utafanyika kwa ajili ya kulinganisha kazi iliyofanywa na kiasi cha fedha iliyotumika kama vinaendana,”alisema.

Alisema tatizo lingine aliloliona ni usimamizi wa mradi huo kutoka kwa watumishi wa manispaa, ambao haukuwa mzuri.

Kwa mujibu wa Katibu Tawala huyo, uchunguzi utafanyika kwa uwazi na ukweli na hawatamuonea yeyote.

Diwani aliwamwagiza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Chibunu Lukiko, kuhakisha anachagua watu wengine wa kuendelea na kazi ya kusimamia mradi huo na kuukamilisha kwa muda uliopangwa.

Kwa upande wake, Mhandisi Mwakitalu, alisema majengo hayo yalikuwa katika hali mbaya kwa kuwa yalijengwa miaka mingi iliyopita.

Alisema majengo hayo yalijengwa tangu mwaka 1955, hivyo kuyakarabati na kurudi katika hali ya upya ilikuwa kazi ngumu.

Mwakitali alisema fedha zilizotolewa na serikali alizitumia kufanya ukarabati kwenye maeneo yaliyoonekana kuwa ni muhimu.

"Kila kazi tunayofanya ikikamilika, tunaomba fedha katika kamati ya maafa tunalipa, zinaisha na hazipitii mikononi mwetu, bali zinapitia katika akaunti ya manispaa,”alisema Mwakitalu.

No comments:

Post a Comment