Sunday 25 June 2017

WAKUU WA MIKOA 11 WATOA TAMKO LA KUMPONGEZA RAIS MAGUFULI


Wakuu wa Mikoa 11 wametoa tamko la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kutokana na kazi ya kizalendo ya kutetea na kulinda rasilimali za Watanzania kwa maslahi ya taifa zima.

Tamko hilo limetolewa jana jioni wakati wakuu hao wakihitimisha mkutano wa kawaida wa ujirani mwema baina ya mikoa hiyo ambao umefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa mkutano huo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanry wakuu wa mikoa ya Singida, Rukwa, Katavi, Kagera, Dodoma, Manyara, Geita, Shinyanga, Mwanza na Kigoma wamesema wanamuunga mkono Rais na wataendelea kuzingatia maelekezo yake katika utendaji wao.

“Sisi wasaidizi wake (rais Magufuli) tutaendelea kutekeleza   na kuzingatia maelekezo katika utendaji wetu wa kila siku. Aidha, wakati wote tutakuwa pamoja na wananchi na kuwatumikia kwa kutimiza wajibu wetu kwa uaminifu, uadilifu na tutahakikisha maslahi ya wananchi na taifa yanapewa kipaumbele cha kwanza”, sehemu ya nukuu ya tamko hilo.

Katika tamko hilo pia wametoa wito kwa wananchi na wawekezaji wote halali wa ndani na nje ya nchi kumuunga mkono rais Magufuli kwa kazi nzuri ya kulinda rasilimali za taifa na wakati wote wazingatie sheria za nchi.

“Tutumie fursa nyingi zinazoendelea kutengenezwa kwa hatua hizo za kizalendo anazochukua mheshimiwa mpendwa wetu rais Dkt. Magufuli Kwa mafanikio, maendeleo na tija kuelekea Tanzania ya uchumi wa kati na uchumi wa viwanda”, sehemu nyingine ya tamko hilo.

Katika Mkutano huo Mwenyekiti Mwanry amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida kwa kuandaa mkutano huo na kupendekeza mikutano ya ujirani mwema ya mikoa ifanyike kikanda ili kuimarisha ulinzi na usalama wa taifa pamoja na kubadilishana uzoefu na kupeana taarifa mbalimbali za kimaendeleo.

“Tumekutana hapa kwa mapenzi ya nchi yetu na ya rais wetu Magufuli. Tuliokutana leo hii changamoto za mikoa yetu zinafanana. Changamoto hizi ni pamoja na uharibifu wa mazingira, uhaba wa mvua, kilimo cha kuhama hama na uhamiaji haramu”, amesema Mwanry na kuongeza;

“Kwa hiyo tukiacha kila Mkoa utatue changamoto hizi kivyake hatutafanikiwa kizitatua. Tumekubaliana kukutana mara kwa mara ili changamoto zinazotukabili sote tuzipatie ufumbuzi wa kudumu kwa pamoja”.

Aidha, mwenyekiti huyo amesema wamekubaliana kusimamia matumizi bora ya ardhi pia kusimamia ulinzi na usalama hasa kwa Mikoa ile iliyopo mipakani na nchi jirani.

Kwa upande wake Mwenyeji wa Mkutano huo Dkt Rehema Nchimbi amesema mkutano huo umekua wa manufaa makubwa kwa mikoa iliyohudhuria pamoja taifa kwakuwa wameweza kubadilishana mawazo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wote.

No comments:

Post a Comment