Thursday 6 October 2016

CUF YAZIDI KUCHAFUKA


NA JACQUELINE MASSANO

MWASISI wa chama cha CUF, James Mapalala, amemshukia Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharrif Hamad, kuwa ni mroho wa madaraka, mgomvi na anapenda fedha kuliko wananchi anaowaongoza.

Mapalala, ambaye ndiye aliyeasisi chama hicho upande wa Tanzania Bara, amesema Maalim Seif hafai kuwa kiongozi kwa sababu ni mgonjwa na ndiyo maana anatukana watu hovyo.

Aidha, amewazodoa viongozi wote wa upinzani wanaokwamisha juhudi za Rais John Magufuli kwamba, kamwe lengo lao hilo haliwezi kufanikiwa.

Mapalala alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akizungumza na Uhuru, nyumbani kwake, Oysterbay, Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha CHAUSTA, alisema Maalim Seif anapenda madaraka na fedha, ndio maana hata yeye (Mapalala) alimfukuza  kwenye nafasi ya mwenyekiti.

Alisema yeye ndiye alikuwa mwanzilishi wa CUF na kukipigania hadi kilipojulikana nchi nzima.

“Nilipokuwa mwenyekiti wa CUF, Maalim Seif akiwa Katibu Mkuu, alidai mimi nimeiba fedha, napiga wanachama na kuwa nimeenda kuwasha Mwenge na CCM. Nilishangaa sana  maana nilikuwa Ruvuma kwa ajili ya ziara za chama.

“Kwa kweli iliniuma sana, niliamua kurudi Dar es Salaam na kuitisha kikao, lakini wajumbe kutoka Zanzibar walikataa kuja kwa madai kuwa hawana fedha, kumbe walikuwa na ajenda yao,”alisema.

Mapalala alisema cha kushangaza baada ya siku nne, Maalim Seif aliitisha kikao kilichofanyika Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wajumbe wote, wakiwemo waliodai hawana fedha.

“Niliandikiwa barua ya kujulishwa kuwa kuna mkutano wa dharura. Nilipopata barua hiyo, nikashangaa sana, maana kazi ya kuitisha mkutano ni ya mwenyekiti na si katibu. Kwa nini sasa ameitisha yeye? Nikagundua kuwa walikuwa na yao,”alisema.

Alisema baada ya kupokea barua hiyo, alikutana na wenzake, ambao waliamua kwa pamoja kwenda kwenye mkutano huo kwa ajili ya kusikiliza walichoitiwa.

Mapalala alisema kikao hicho kiliendeshwa na Maaalim Seif, aliyekuwa amekalia kiti cha mwenyekiti.

Aliongeza kuwa akiwa mwenyekiti wa chama hicho, alishangaa alipoingia ndani ya ukumbi wa mkutano, kumkuta Maalim Seif akiwa amekalia kiti chake na kukataa katakata kumpisha.

"Nilisomewa mashitaka yangu kuwa, nimeiba fedha, nimempiga mwanachama pamoja na kwenda kuwasha Mwenge na CCM.
Nilipowauliza ni lini nimeiba fedha, hakuna aliyejibu, ni wapi nimempiga mtu, hata yule aliyetajwa kupigwa nami alikanusha.
Kuhusu Mwenge, wote walikaa kimya.

“Hali ile iliwakasirisha sana wajumbe kutoka Bara, walipoona hivyo walishikwa na hasira, wakaanza kupigana na Wazanzibar na Wazanzibar walipoona hivyo, wakakimbia,”alisema.

Alisema baada ya kutokea vurugu hizo, mkutano ulivunjika na Maalim Seif aliamua kuondoka na watu wake, ambapo baadaye waliamua kuitisha mkutano mwingine wa kumfukuza Mapalala, ambao ulifanyika Tanga.

“Ule mkutano ulikuwa na Wazanzibar tu, lakini baadae waliamua kuzunguka mikoa mbalimbali na kuwahonga fedha wajumbe ili waweze kushiriki katika mkutano huo,”alisema.

Alisema akidi ya mkutano huo ilitimia na kupitisha ajenda ya kumfukuza, naye hakuwa na la kufanya zaidi ya kukubaliana na uamuzi huo.

UROHO WA MAALIM SEIF

Alisema Maalim Seif siku zote huwa anapenda watu wawe chini yake na ndiyo maana mara kwa mara kunakuwa na kutoelewana ndani ya CUF.

“Kutokana na mambo yaliyonikuta, imani yangu kwa Maalim Seif ilikwisha kabisa kwa sababu si binadamu wa kawaida,”alisema.

Alisema Maalim Seif amekuwa king’ang’anizi wa madaraka, ndiyo maana anagombana na mwenyekiti wa sasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

“Sioni ajabu kuona Maalim Seif anatukanana na watu hadharani. Seif hali yake kiafya sio nzuri, lakini cha ajabu anang’ang’ania sana madaraka,”alisema.

Alisema Maalim Seif hafai kuwa kiongozi kwa sababu anajitafutia madaraka, pia ni mgomvi na mtu asiye na staha mbele ya Rais.

“Labda ugonjwa alionao umezidi ndiyo maana amekuwa mgomvi. Sasa na ugonjwa ule atapigana na nani?” Alihoji.

KUHUSU  UKAWA

Akizungumzia UKAWA, Mapalala alisema umoja huo una malengo mazuri kisiasa, lakini unatumia njia mbaya za kisiasa.

“Mnaweza kuishinda CCM kwa kutumia akili na wala sio kwa kutumia fujo,” alisema.

Aliviomba vyama vya siasa vinavyounda UKAWA, kutotumia nguvu kwa sababu vitasababisha vurugu na madhara makubwa, ikiwemo vifo ambapo na wao pia hawatapona.

Hata hivyo, alisema kwa sasa wamechelewa kwa sababu hawawezi kumshinda Rais Dk. John Magufuli, kutokana na mambo makubwa anayoyafanya.

AMPONGEZA RAIS MAGUFULI

Mapalala alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya, ambapo alisema chini yake, serikali imefanya mambo makubwa ambayo hayajawahi kutokea.

“Nampongeza sana Rais Magufuli, pamoja na kwamba nilikuwa mpinzani, lakini sikuwahi kugombana na CCM hata siku moja,” alisema.

Alisema anashangaa kuona watu wanamkosoa Rais Magufuli wakati  hawana lolote walilofanya.

“Wengine ni watu wa CCM, ambao wanataka kumuangusha Rais Magufuli, hawatamuweza kwa sababu anafanya kweli, tena ile kweli ya Mungu,”alisema.

USHAURI KWA CUF

Mwanasiasa huyo mkongwe alisema ili CUF iendelee, ni lazima Profesa Lipumba na Maalim Seif waondoke kwenye nafasi zao.

“Hawa wote ni lazima waondoke, yaani wakitaka CUF iendelee ni lazima waondoke, hakuna kingine hapo,”alisema.

Aliwataka wanachama wa CUF, kuhakikisha wanachagua viongozi wengine, ambao wataweza kukiendesha chama hicho ili kuepusha migogoro isiyo na lazima.

Wakati huo huo, aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Jesse Mashime, alisema aliamua kujiuzulu nafasi hiyo mwaka 1993, baada ya kuona viongozi wanafanya kazi kwa maslahi ya matumbo yao.

Akizungumza na Uhuru jana, Mashime alisema aliamua kuachana na siasa baada ya kuona hakuna kiongozi mwenye mlengo ya kuwasaidia wananchi na taifa kwa ujumla. 

“Wanasiasa wengi ni wanafiki. Ni wanasiasa wachache sana, ambao wanafanya kazi kwa maslahi ya nchi, lakini wengine ni kwa maslahi yao,”alisema na kuongeza:

“Nimeamua kuwa Mhubiri katika Kanisa la Kristo la Buguruni, siasa siiwezi ni bora nihubiri tu, siamini kabisa katika siasa za Afrika.”

No comments:

Post a Comment