Thursday 6 October 2016

MKUU WA MAGEREZA DODOMA KITANZINI, ADAIWA KUTENGENEZA MADAWATI KWA WATU BINAFSI


NA MWANDISHI WETU, DODOMA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, kuchunguza ni kwa nini Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma, Antonino Kilumbi, amekwenda kutengeneza madawati kwa watu binafsi, badala ya karakana ya Magereza kama ilivyokusudiwa na serikali.

Magereza mkoa wa Dodoma, ilipewa sh. milioni 24 na serikali ili kutengeneza madawati 480 na kila moja lilitakiwa kugharimu sh. 50,000. Lakini uongozi wa gereza hilo ulitengeneza madawati hayo kwa watu binafsi, ambapo dawati moja liligharimu sh. 70,000.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana, wakati alipotembelea Gereza la Isanga, mkoani Dodoma, akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo yanayotoa huduma za kijamii mjini hapa.

Alisema kama gereza hilo halikuwa na uwezo wa kutengeneza madawati hayo, kwa nini kazi hiyo wasingeipeleka kwenye taasisi nyingine ya umma, hivyo amemtaka Rugimbana, kufuatilia ziada ya sh. 20,000, kwenye utengenezaji wa kila dawati inatoka wapi na inakwenda kwa nani.

“Nimesikia kwamba mnawachangisha askari kiasi kilichoongezeka kwenye utengenezaji wa madawati haya. Ni marufuku askari kutoa fedha mifukoni mwake kulipia shughuli za serikali.

"Serikali imeandaa utaratibu wa kuwezesha taasisi zake zikiwemo za kijeshi kwa kuzipa kazi ya kutengeneza bidhaa na miundombinu mbalimbali, ikiwemo madawati ili kuyaongezea tija,"alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma, Kilumbi alisema waliamua kupeleka kazi hiyo kwa watu binafsi kwa sababu hawana vifaa.

Aidha, Waziri Mkuu alimtaka mkuu huyo wa magereza mkoa kuimarisha kitengo cha ufundi seremala na kuhakikisha anatumia vizuri nguvu kazi aliyonayo katika kuzalisha bidhaa mbalimbali.

Kuhusu changamoto ya makazi kwa askari, Waziri Mkuu alisema serikali inatambua na imeweka mkakati wa ujenzi na kwa upande wa askari magereza, wataanzia na mkoa wa Dodoma.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alitembelea maduka ya kuuzia bidhaa mbalimbali, zikiwemo nguo katika maeneo ya Soko la Sabasaba na Majengo.

No comments:

Post a Comment