Thursday, 19 November 2015

DK. TULIA ACKSON ACHAGULIWA KUWA NAIBU SPIKA WA BUNGE, ASEMA HATAILINDA SERIKALI, BALI ATAISIMAMIA



MBUNGE wa kuteuliwa, Dk. Tulia Ackson, amechaguliwa  kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 Dk. Tulia ameibuka mshindi baada ya kupata kura 250, sawa na asilimia 71.2 na kumshinda Magdalena Sakaya wa CUF, aliyepata kura 101, sawa na asilimia 28.8.
Mapema jana,  Dk. Tulia Ackson, alisema kazi ya Bunge sio kuibeba serikali bali ni kuisimamia na kwamba, hilo ndio litakuwa jukumu lake.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge, juzi, Dk. Tulia alisema zinapotokea hoja kwamba mtu mwingine ataibeba serikali, si za kweli.
“Mimi sitaweza kuibeba serikali, nitaibebaje? Kazi ya Bunge ni kuisimamia serikali kutokana na kupokea mapendekezo na si vinginevyo,” alisisitiza.
Aidha, alisema serikali italeta mapendekezo yake, ikiwemo ya miswada ya sheria mbalimbali na Bunge kama kawaida yake itayajadili.
Dk. Tulia alieleza kuwa kuteuliwa kwake na Rais Dk. John Magufuli, haimanishi kuwa anamuwakilisha bungeni, bali ni mbunge kama wengine.
Alisema atawasimamia wabunge kuisimamia serikali na sio kuibeba serikali.
Aliongeza kuwa ana vigezo vya kutosha kukalia kiti hicho na kuwa amefanya kazi kubwa katika Bunge la Katiba, hivyo hana shaka na hilo.
Alisema bunge hilo ni la vijana, hivyo kuna changamoto nyingi ambazo wabunge wamekutana nazo wakati wakipita kwa wananchi kuomba kura, hivyo watazileta zote bungeni na zitafanyiwa kazi.

No comments:

Post a Comment