NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imetoa siku 30 kwa wawekezaji waliowekeza
kwenye viwanda na mashamba yaliyokuwa yakimilikiwa na serikali, kuwasilisha
taarifa za utekelezaji wa mauzo baada ya baadhi yao kushindwa kuviendeleza.
Imesema endapo wawekezaji hao watashindwa kutoa taarifa
hizo za utekelezaji wa mikataba, viwanda na mashamba hayo yatarejeshwa
serikalini.
Hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa kuvirejesha viwanda na
mashamba ambayo wawekezaji wake kushindwa kutekeleza mpango wa uwekezaji kwa
kuvibadilishia matumizi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Msajili wa
Hazina, Lawrence Mafuru, alisema ofisi hiyo inapitia mikataba yote ya
ubinafsishwaji wa viwanda na mashamba.
Alisema wapo baadhi ya wawekezaji wamekiuka masharti ya
mikataba hiyo, ambapo baadhi wamechukua mashine kwenye viwanda na mashamba bila
kuzirejesha mashine mbadala.
Alibainisha kuwa masharti mengine yaliyokiukwa ni baadhi
ya viwanda na mashamba kubadilishiwa matumizi kinyume na mikataba na
kutokukamilisha malipo ya ununuzi.
Msajili huyo wa hazina aliwataka wawekezaji walionunua
mali hizo zilizokuwa zikimilikiwa na serikali, kuwasilisha taarifa zao za
utekelezaji wa mikataba ya mauzo serikalini ndani ya siku 30.
Endapo wawekezaji hao watashindwa kutekeleza maagizo
hayo ya serikali, Mafuru alisema hatua stahiki zitachukuliwa, ikiwemo kurejesha
viwanda na mashamba hayo kwenye miliki ya serikali.
Maamuzi hayo ya serikali ni muendelezo wa utekelezaji wa
ahadi za Rais Dk. John Magufuli, ya kurejesha viwanda na mashamba yaliyokuwa yakimilikiwa na
serikali ambayo wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza.
Alipokuwa akiwahutubia wananchi
kwenye mikutano ya kampeni kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais, Dk.Magufuli alisema mara
atakapopata ridhaa ya Watanzania, atarejesha serikalini viwanda vyote
vilivyobinafsishwa bila kuendelezwa.
Alisema hatua hiyo itakwenda
sambamba na ufufuaji wa viwanda na kujenga viwanda vingine ili kuondoa tatizo
la ajira kwa vijana.
No comments:
Post a Comment