Sunday, 29 October 2017

JPM ATEUA WAKUU WAPYA SITA WA MIKOA


RAIS Dk. John Magufuli, amefanya uteuzi wa wakuu wapya wa mikoa, makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu.

Katika uteuzi huo, uliotangazwa kwa vyombo vya habari jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Rais Magufuli amewateua wakuu wapya wa mikoa sita huku akiwapandisha wakuu wa wilaya watatu.

Akitangaza uteuzi huo, Balozi Kijazi aliwataja wakuu wa wilaya waliopanda cheo, mikoa yao ikiwa kwenye mabano kuwa ni Alexander Mnyeti (Manyara), Joackim Wangabi (Rukwa) na Robert Gabriel (Geita).

Kabla ya uteuzi huo, Mnyeti alikuwa mkuu wa wilaya ya Arumeru, Gabriel alikuwa mkuu wa wilaya ya Korogwe wakati Wangabi alikuwa mkuu wa wilaya ya Nanyumbu.

Wakuu wengine wapya walioteuliwa ni Adam Malima, anayekwenda mkoa wa Mara, Christina Mndeme, aliyeteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Dodoma na Gasper Nyakemwa, aliyeteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Mtwara.

Aidha, Rais Magufuli amewateua IGP wa zamani, Ernest Mangu na Katibu Mkuu wa zamani, Azizi Mlima kuwa mabalozi wapya. Vituo vyao watapangiwa baadaye.

Katika uteuzi huo, Rais Magufuli pia amewapandisha manaibu katibu wakuu saba kuwa makatibu kamili wa wizara, amewahamisha makatibu wakuu wanne na naibu katibu mkuu mmoja kwenda wizara nyingine.

Ofisi ya Rais Ikulu, Katibu Mkuu anaendelea kuwa, Alphayo Kidata; Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Katibu Mkuu anakuwa Laurian Ndumbaro na Naibu wake ni Doroth Mwaluko,

TAMISEMI: Katibu Mkuu anaendelea kuwa Injinia Mussa Iyombe, akisaidiwa na Zainabu Chande (Afya) na Dickson Nzunda (Elimu).

Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira: Katibu Mkuu ni Injinia Joseph Malongo, naibu wake ni Butamo Phillipo.

Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu: Katibu Mkuu ni Erick Shitindi, akisaidiwa na manaibu Maimuna Tarishi na Faustine Kamuzora.

Wizara ya Kilimo: Katibu Mkuu ni Mathew Ntigumwa akisaidiwa na Dk. Thomas Kashillilah.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi: Katibu Mkuu ni Maria Mashingo (Mifugo) na Yohana Budeba (Uvuvi).

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano: Katibu Mkuu ni Leonard Chamuliko, Injinia Joseph Nyamuhega, Maria Sasabwe na Anjelina Madete.

Wizara ya Fedha: Katibu Mkuu ni Dotto Mgisha, akisaidiwa na Susan Mkapa, Amina Shabani na Dk. Khatib Kazungu.

Wizara ya Nishati: Katibu Mkuu ni Khamisi Mwinyimvua

Wizara ya Madini: Katibu Mkuu ni Simon Mpanjira.

Wizara ya Katiba na Sheria: Katibu Mkuu ni Sifuni Mchome, akisaidiwa na Amon Mpanju.

Wizara ya Ulinzi: Katibu Mkuu ni Dk. Florence Turuka, akisaidiwa na Immaculata Ngwala.

Wizara ya Mambo ya Ndani: Katibu Mkuu ni Meja Jenerali Projes Rwegasira, akisaidiwa na Balozi Hassan Simbayahaya.

Wizara ya Maliasili na Utalii: Katibu Mkuu ni Meja Jenerali Gaudence Milanzi, akisaidiwa na Dk. Aloyce Nzuki.

Wizara ya Ardhi: Katibu Mkuu ni Doroth Mwanyika, akisaidiwa na Dl. Moses Kasiluka.

Wizara ya Viwanda na Biashara: Katibu Mkuu ni Profesa Elisante Ole Gabriel, akisaidiwa na Ludovick Mhiye na Profesa Joseph Mushashwaya.

Wizara ya Elimu: Katibu Mkuu ni Leonard Akwilapo, akisaidiwa na Profesa Hapifan Mdoe na Avemaria Semakafu.

Wizara ya Afya: Katibu Mkuu ni Mpoki Olusibisya, akisaidiwa na Sihaba Mkinga.

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo: Katibu Mkuu ni Susan Mlawi, akisaidiwa na Nicholaus William.

Wizara ya Maji: Katibu Mkuu ni Dk. Kitilya Mkumbo, akisaidiwa na Injinia Emmanuel Kalobelo.

Wizara ya Mambo ya Nje: Katibu Mkuu anakuwa Dk. Adolph Nkenda, akisaidiwa na Balozi Ramadhani Mwinyi.

Kwa mujibu wa Balozi Kijazi, wateule hao wapya wanatarajiwa kuapishwa leo, katika hafla itakayofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

UMEME WAMTOKEA PUANI KIGOGO TANESCO


WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani ameagiza kuhamishwa kwa Meneja wa kituo cha kuzalisha umeme cha Kidatu, Manfred Ndyalu kwa kushindwa kutoa taarifa mapema, baada ya kuchomoka kwa waya na kusababisha mitambo iliyobaki kuzidiwa.
Pia, amemtaka Meneja Mkuu wa Usimamizi na Uzalishaji Umeme, Abdallah Ikwassa, kuhakikisha kuwa mashine zote  zinafanyakazi, vinginevyo aachie ngazi kutokana na kutokufanya majukumu yake ipasavyo.
Vilevile, amemuagiza Naibu Mkurugenzi wa Usafirishaji, Kahitwa Bishaija, kuhakikisha mfumo wa kusambaza umeme wa Ubungo, unaanza kufanyakazi mara moja, vinginevyo ajitafakari na kuchukua hatua mara moja.
Kauli hiyo aliitoa jana, alipotembelea mitambo ya Umeme ya Ubungo na ule wa Kinyerezi 1, baada ya kutokea kwa hitilafu ya umeme, iliyosababisha kukatika kwa umeme nchi nzima.
Dk. Kalemani alisema, wanamuhamisha meneja wa kituo hicho, kutokana na uzembe alioufanya wa kushindwa kutoa taarifa mapema ya kuchomoka kwa waya na kusababisha hitilafu kwenye gridi ya taifa.
"Tumemuelekeza mkuu wake amuondoe kwenye kituo hicho mara moja ili hali hiyo isijirudie tena na ili tuwe na wafanyakazi wachache wenye uweledi," alisema.
Kuhusu Naibu Mkurugenzi wa Usafirishaji, alisema anatakiwa kujitathmini mwenyewe kutokana na kushindwa kusimamia  mfumo wa Ubungo, kuhakikisha unafanyakazi.
Pia, alisema Meneja wa Usimamizi na Uzalishaji Umeme, anatakiwa ajitafakari mwenyewe kutokana na mitambo mingi ya umeme kutofanyakazi.
"Kutokana na hali hiyo, mitambo mingi ya kuzalisha umeme na vyanzo vingi vimeshindwa kufanyakazi, lakini nashukuru Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), walitoa taarifa ya kuwaomba radhi wananchi," alisema.
Hata hivyo, alisema wanaendelea kufuatilia chanzo cha tatizo hilo ili kuweza kulitatua mara moja.
"Tumefuatilia maeneo yote ambayo tumehisi yana tatizo, tumeenda kwenye mfumo wenyewe Ubungo ili kuweza kugundua chanzo cha tatizo, lakini tumekuta mfumo bado unafanyiwa marekebisho ya kuongezewa nguvu, taratibu zinaendelea.
"Pia, tukaenda Kinyerezi 1, ambako sasa kuna mashine haifanyikazi, nayo itafanyiwa matengenezo, lakini kubwa ni valvu moja, ambayo imesababisha mtambo wa Kinyerezi ushindwe kufanyakazi, jitihada zinaendelea," alisema.
Alisema marekebisho yanaendelea na kwa sasa umeme unapatikana nchi nzima, baada ya gridi ya taifa kurejea, ambayo imerudi tangu usiku.
"Lakini hata hivyo, yapo maeneo machache ambayo hayapati umeme wa kutosha kwa sababu mtambo mmoja wa Ubungo 11, wenye uwezo wa kuzalisha umeme megawati 129, haujaanza kufanyakazi.
"Nimewaelekeza wataalamu wafanyekazi usiku na mchana leo (jana), mpaka mtambo wa Ubungo wenye megawati 129, nao uweze kufanyakazi. Wamenihakikishia kwamba, mpaka leo saa nne asubuhi, mtambo wa Ubungo 11 nao utakuwa unafanya kazi," alisema.
Kutokana na hali hiyo, alisema Wizara na TANESCO watahakikisha leo, saa 5 asubuhi, maeneo yote yaliyobaki yanapata umeme wa uhakika.
"Yale matengenezo yaliyokuwa yanaendelea ya kurekebisha mashine, nazo zitaendelea na utaratibu wake kama kawaida. Tunawaomba radhi wananchi kwa matatizo yalitokea," alisema.

MVUA YALETA KIZAAZAA DAR, MMOJA AFA





MVUA kubwa iliyonyesha jijini Dar es Salaam, jana, ilisababisha mafuriko makubwa na kuua mtu mmoja, huku miundombinu nayo ikiharibika.
Maeneo yaliyoathirika zaidi ni Bonde la Mto Msimbazi, maeneo ya Jangwani na Mto Kenge, Tabata wilayani Ilala, ambako maiti ya mtu mmoja mwanaume iliopolewa.
Katika maeneo ya Tegeta, Basihaya na  Mbezi Beach,  maji yamezingira makazi ya watu na kufanya  wananchi kuzikimbia nyumba zao.
Maeneo mengi yaliyokumbwa na mafuriko hayo, nyumba zimezama kabisa na zingine maji yamefikia usawa wa paa.
Mvua hizo, zilisababisha wanafunzi 12 wa Shule ya Msingi Atlas Kampasi ya Madale, Dar es Salaam kuokolewa baada ya basi walilokuwa wamepanda kuzama katika Mto Tegeta, ulioko Goba Mtaa wa Muungano.
Hali  hiyo, imesababisha adha kubwa kwa usafiri kutokana na barabara nyingi kutopitika, ambapo Kampuni  ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART ), ililazimika  kusimamisha huduma baada ya maji kupita juu ya barabara eneo la Jangwani na mawasiliano kukatika kati ya Magomeni na Kariakoo.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, ambaye alikagua maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo, alithibitisha mvua hiyo kuleta madhara na kutoa tahadhari kwa wananchi waishio mabondeni na maeneo hatarishi kuondoka mara moja.
“Hali sio nzuri. Serikali imekuwa ikitahadharisha wananchi kuondoka maeneo ya mabondeni mara kwa mara, lakini wananchi wamekuwa wazito kutii.
“Natoa agizo wote waondoke kwa sababu bado mvua inaendelea kunyesha, huenda kukawa na madhara makubwa,” alisema Mjema akiwa Jangwani.
Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu, alisema mvua hiyo imesababisha uharibifu mkubwa wa mali, nyumba kuzama na miundombinu ya barabara kuharibika.
“Hatua moja tunayofanya ni kuhamasisha watu kuondoka katika maeneo hatarishi. Maji ni mengi na yanaendelea kuongezeka. Chanzo ni madaraja katika mito mingi kujaa uchafu unaozuia maji kupita kwa urahisi. Tumeomba msaada wa kuzibua mifereji na madaraja hayo,”alisema Zungu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Salum Hamduni, alithibitisha mtu mmoja kufa maji.
“Maiti ya kijana wa umri wa miaka kati  ya 25 na 30,  iliopolewa bonde la Mto Kenge Tabata. Umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Amana,” alisema Kamanda Hamduni.
Alisema kuhusu madhara mengine yaliyopatikana, bado  polisi wanaendelea kufuatilia na watatoa taarifa zaidi.
Hata hivyo, alitahadharisha wananchi kutii maagizo ya serikali ya kuondoka katika maeneo hatarishi.
Waathirika wengi  walionekana wakitoa  mali zao katika nyumba zilizojaa maji huku wengine wakiwa wamejikusanya katika nyumba za jirani, ambazo hazikuathirika wakiwa na mizigo yao.
“Hatufahamu hatima yetu. Tumepoteza kila kitu hapa,”alisema Zainabu Omari, mkazi wa Jangwani.
WANAFUNZI WAOKOLEWA
Wanafunzi 12 wa Shule ya Msingi Atlas, Kampasi ya Madale, Dar es Salaam, waliokolewa baada ya basi walilokuwa wamepanda kuzama katika Mto Tegeta, ulioko Goba, Mtaa wa Muungano.
Basi hilo dogo aina ya Hiace, lilizama jana, saa tano asubuhi, baada ya mvua kubwa iliyonyesha maeneo mbalimbali, kusababisha baadhi ya mito, ukiwemo Mto Tegeta, kujaa na kufurika maji.
Wanafunzi hao, walikuwa wakirejeshwa nyumbani kutoka shule na walipofika eneo hilo, basi hilo lilizama kutokana na wingi wa maji katika mto huo.
Kelele za watoto hao kuomba msaada, zilisikika baada ya kukwama katikati ya mto huo huku maji yakiingia ndani ya gari kupitia madirishani.
Mashahidi wa tukio hilo, walisema dereva wa basi hilo, alionekana akiendesha kwa umakini, lakini alipofika eneo hilo, alishindwa kupita kutokana na maji ya mto huo  kukimbia kwa kasi.
“Tulianza kusikia kelele za watoto za kuomba msaada, tulijikusanya na kwenda kuwaokoa, watoto ni wadogo, ambao kwa kukisikia wana umri wa miaka mitatu
“Tunashukuru kwa umoja wetu, tumefanikiwa kuwaokoa ingawa hadi sasa gari lao halijatoka kutokana na maji yaliyojaa katika eneo hilo,”alisema Maimuna Ally.
MABASI YA DART YASIMAMA
Wakati huo huo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), Deus Bugaywa, alitangaza kusitishwa kwa huduma ya usafiri wa mabasi hayo baada ya kufungwa kwa barabara ya Morogoro, kwa sababu ya daraja la Mto Msimbazi kujaa maji.
Hata hivyo, alisema huduma hiyo itarejeshwa baada ya hali hiyo kutengamaa.
“Tunawaomba radhi abiria wetu kwa usumbufu uliojitokeza kwani huduma hiyo ni muhimu kwa jamii na itarudi baada ya hali kukaa sawa,”alisema Bugaywa.
Mvua hizo pia zilisababisha barabara ya Morogoro, eneo la Mbezi Kibanda cha Mkaa, maji yalijaa na kusababisha magari kushindwa kupita.
Baadhi ya magari, likiwemo lori lililobeba mbao, lilionekana katikati ya daraja wakati maji yakiendelea kuongezeka.
Mbali na madhara hayo, mvua hizo pia ziliharibu daraja la Kiluvya, ambalo lilikatika na kusababisha magari yanayotumia barabara ya Morogoro, yakiwemo ya abiria, kusababisha usumbufu mkubwa ambapo baadhi yalilazimika kuzunguuka na kupitia barabara ya Msata-Bagamoyo.
NDEGE YAPATA AJALI SERENGETI
Katika tukio jingine, mvua hizo zilisababisha ndege ndogo ya abiria ya Kampuni ya Coastal Aviation, kupata ajali ilipokuwa ikijaribu kutua katika uwanja wa ndege wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Taarifa ya kampuni hiyo ilisema, ndege hiyo ilipata ajali saa 8.30 mchana, ilipokuwa ikitaka kutua, ambapo kutokana na hali mbaya ya hewa iliyosababishwa na mvua, ilishindwa kufaya hivyo.
Iliongeza kuwa, abiria wawili na rubani ndio waliopata majeraha machache na kulazimika kupelekwa hospitali.
Chanzo cha habari kilisema majeruhi hao walipelekwa Nairobi, Kenya kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Wednesday, 25 October 2017

MKUCHIKA AWAKOROMEA WANAOITISHA TAKUKURU



TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imetakiwa kufanyakazi zake kwa ujasiri bila kuogopa kutishwa na wasikubali kuingiliwa katika utendaji wao na mtu yeyote.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu George Mkuchika, kutokana na taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Valentino Mlowola, kuwa mamlaka hiyo inaingiliwa na wanasiasa.

Akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi wa  TAKUKURU, Mkuchika alisema, chombo hicho kipo kwa mujibu wa sheria, hivyo wasikubali kutishwa au kuingiliwa na mtu yeyote.

"Ni lazima muhakikishe kuwa, utendaji wenu unaakisi matakwa ya kisheria yanayosisitiza haki, weledi na umakini wa hali ya juu ili kuepuka kuonea au kumkomoa mtu," alisema.
Pia, alisema viongozi na watumishi wa taasisi hiyo, ndiyo kioo cha watumishi wengine wa serikali, hivyo inawapasa kuwa mfano bora katika kutumia rasilimaliwatu, vifaa na fedha za umma walizokabidhiwa katika kutekeleza majukumu yao.

Waziri huyo alisema, watumishi wanaokiuka maadili ya kazi, wachukuliwe hatua mara moja. "Hatuwezi kuvumilia watumishi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na utovu wa nidhamu,"alisisitiza.

Aliongeza: "Natoa onyo kwenu na watumishi mnaowasimamia kwamba, serikali hii haina mzaha katika kuwashughulikia wavivu na wabadhirifu. Taasisi yenu ni kati ya taasisi chache za serikali, ambazo zina vijana wengi na wasomi, hivyo matokeo ya kazi zenu yanatarajiwa kuwa kwa wakati na weledi wa hali ya juu."

Vilevile, aliitaka TAKUKURU kutoa elimu kwa wananchi, shuleni, katika vyuo na kutoa machapisho mbalimbali yanayotoa elimu kuhusu rushwa.

"Kwa ofisi nyingi za serikali, wakala na ofisi za umma, mwitikio wa kutoa mafunzo kwa watumishi wake dhidi ya vitendo vya rushwa haujawa mzuri sana," alisema.
Kutokana na hali hiyo, alitoa wito kwa viongozi wote wa ofisi za serikali, kuwashirikisha viongozi wa TAKUKURU katika mikusanyiko yao ili waweze kutoa mafunzo kuhusu rushwa.

Akizungumzia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, kifungu 145(c), alisema ni kuimarisha Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) ili iweze  kufanyakazi zake kwa ufanisi.

"Pia kuanzisha Mahakama maalumu ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, kwa lengo la kuharakisha uchunguzi na utoaji hukumu kwa makosa hayo," alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Valentino Mlowola, alisema taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali za wanasiasa, kutumia vibaya chombo hicho kukuza umaarufu wao.

"Wapo baadhi ya wanasiasa ambao siku za hivi karibuni, wamekuwa wakitumia jina la TAKUKURU kujikuza kisiasa. Jambo hili halikubaliki kwani taasisi hii ni huru na inafanyakazi zake kwa weledi bila kuingiliwa na mtu yeyote," alisema.
Kutokana na hali hiyo, alitoa rai kwa wanasiasa, kuacha kuitumia TAKUKURU kwa maslahi yao kwa sababu hawatasita kuwachukulia hatua kali za kisheria, ikiwemo kuwafikisha mahakamani.

"Nikuombe waziri, ulichukue hili na ukawaelimishe wabunge na wasiasa wengine, hasa utakapokuwa bungeni, waache mara moja kuitumia TAKUKURU kwa maslahi yao," alisema.

Alisema taasisi hiyo ina upungufu mkubwa wa watumishi, hasa kwenye ofisi zao za wilaya, ambapo hawajafanikiwa kufungua ofisi kwenye wilaya mpya zilizoanzishwa na serikali.

Kuhusu bajeti ya taasisi hiyo, alisema toka mwaka 2014, imeendelea kupungua mwaka hadi mwaka, hali inayoathiri utendaji kazi wa taasisi hiyo kutoka sh. bilioni 24, kwa mwaka hadi sh. bilioni 12.

UFAHARI WAMTOKEA PUANI KIGOGO TRA




TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imempandisha kizimbani Ofisa Forodha Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jennifer Mushi, akituhumiwa kumiliki magari 19, yenye thamani ya sh. milioni 197.
Pia, Jennifer anatuhumiwa kuishi kifahari, maisha ambayo hayalingani na kipato chake halali.
Jennifer, alipandishwa kizimbani jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambako alisomewa mashitaka mawili ya kumiliki magari hayo, ambayo hayaendani na kipato chake na kuishi maisha ya kifahari yenye thamani ya sh. 333,255,556.24, ambayo nayo hayalingani na kipato chake.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter, alimsomea mshitakiwa huyo mashitaka hayo aliyoshitakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ambayo aliyakana.
Peter, alidai tarehe tofauti kati ya Machi 21 na Juni 30, 2016, maeneo ya mkoa na jiji la Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa  mtumishi wa umma, aliyeajiriwa na TRA kama ofisa forodha msaidizi, alikutwa akimiliki magari 19, yenye thamani ya sh. 197,601,207, ambayo hayaendani na kipato chake halisi.
Mshitakiwa huyo anadaiwa alikutwa akimiliki magari aina ya Toyota Rav 4 mawili, Toyota Dyna Truck, Toyota Viz, Suzuki Carry mawili, Toyota Ipsum, Toyota Wish mawili, Toyota Mark II, Toyota Mark X, Toyota Regiusage, Toyota Estima mawili, Toyota Alex, Toyota Noah, Toyota Crown, Toyota Hiace, Toyota Passo.
Pia, mshitakiwa huyo anadaiwa  kati ya Machi 21, 2012 na Machi 30, 2016, katika jiji na mkoa wa Dar es Salaam, akiwa mwajiriwa wa TRA na cheo chake hicho, aliishi maisha ya juu ya sh. 333,255,556.24, ambayo hayaendani na  kipato chake.
Mshitakiwa huyo, ambaye anatetewa na Wakili Elisalia Mosha, alikana mashitaka hayo, ambapo upande wa jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuomba kupangiwa tarehe ya kuanza kwa usikilizwaji wa awali.
Kwa upande wa Wakili Mosha, aliiomba mahakama kumpatia dhamana mteja wake kwa kuwa mashitaka yanayomkabili yanadhaminika kwa mujibu wa sheria.
Hakimu Shaidi alitoa masharti ya dhamana, yaliyomtaka mshitakiwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho, ambaye atatia saini dhamana ya sh. milioni 20.
Mshitakiwa alifanikiwa kutimiza masharti hayo ya dhamana na kuachiwa huru hadi Novemba 7, mwaka huu, shauri hilo litakapopelekwa kwa usikilizwaji wa awali.

Tuesday, 24 October 2017

JPM: WAPUUZENI WANAOPOTOSHA TAKWIMU ZA SERIKALI




RAIS Dk. John Magufuli, amewataka watanzania kuendelea kuwapuuza wapotoshaji wa takwimu rasmi za serikali, wanaodai mapato ya serikali yanashuka, tofauti na inavyoelezwa na mamlaka husika.

Amesema lengo la watu hao ni kuliondoa taifa kwenye mwelekeo wa kujenga uchumi kwa kuwachonganisha wananchi na serikali yao, inayofanya jitihada kubwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadaye.

Rais alisema vyombo vya ulinzi na usalama, vinapaswa kuwaangalia watu hao na kwamba ana kumbukumbu juu ya uwepo wa sheria ya kudhibiti wapotosha takwimu, ambayo inapaswa kutekelezwa, ikiwezekana wahusika wafikishwe mahakamani kujieleza.

Alitoa kauli hizo Ikulu jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza kwenye hafla ya kuwatunuku vyeti wajumbe wa kamati zilizofanya uchunguzi wa kiwango, aina na thamani ya madini katika makinikia na baadae kufanya mazungumzo na Barrick Gold Mine kwa mafanikio makubwa.

Dk. Magufuli alisema, kuhusu makubaliano ya biashara ya madini, mpaka sasa kazi kubwa, ya hatari imefanywa na watu wenye uzalendo na waliotoa maisha yao kwa ajili ya taifa, hivyo ni jambo la ajabu kwa mtu kusema taifa limeliwa, kwa sababu ya manufaa binafsi.

"Unaweza kuhoji uzalendo wao, watu wamejitoa maisha kwa ajili ya rasilimali za taifa hili, halafu watu fulani wanakuja na kusema eti tunaliwa kwa sababu tu wamepewa kitu chochote kwa ajili ya matumbo yao, hii haikubaliki, nawaomba tutangulize uzalendo," alisema.

Rais Magufuli alifafanua kuwa mtu hawezi kusema serikali inapindisha uhalisia kuhusu takwimu za mapato, wakati kuna miradi na mikataba lukuki imetekelezwa na mingine naendelea kutekelezwa na serikali hiyo hiyo kwenye sekta, maeneo mbalimbali nchini.

Aliitaja baadhi ya miradi hiyo na mikataba kuwa ni ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge, Ununuzi wa ndege sita kwa mpigo, ongezeko la fedha kwenye bajeti ya afya, ujenzi wa barabara za lami na usambazaji wa umeme vijijini (REA); na kuhoji kama kweli kusingekuwa na ongezeko la mapato, serikali ingewezaje kuyafanya yote hayo.

"Kwa mfano kwenye mradi wa Stingler Gorge ambao tangu enzi za Hayati Baba wa taifa ulifikiriwa, zimejitokeza kampuni zaidi ya 79 kwa ajili ya kuomba zabuni ya ujenzi, haya yote tunayafanya kwa sababu mapato yapo, kwa hiyo inashangaza watu wakipotosha," alisema Rais Magufuli.

Alisema kwa mafanikio yaliyopatikana, Watanzania wamethibitisha kuwa ni taifa linalopaswa kutoa misaada na si kuomba misaada hivyo kuna ulazima wa kushirikiana ili manufaa yanayopatikana kwenye sekta ya madini yawe kwa usawa tofauti na ilivyokuwa awali.

Pia, alitumia fursa hiyo kuwashukuru wajumbe wote wa kamati wakiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na kuwaita watanzania kweli, wazalendo wenye mapenzi mema na nchi yao licha ya kuweka maisha yao hatarini.

Alisema, kazi waliyoifanya ni kubwa, ya kutisha ambayo bila Mungu wasingeikamilisha na kwamba hata yeye rais, mtikisiko alioupata muda wote wa mazungumzo baina na serikali na kampuni za madini zilizohusika na makinikia, ulikuwa si wa kawaida lakini alikuwa tayari kukabiliana nao kwa kuwa amejitolea maisha yake kwa ajili ya wapigakura wa Tanzania.

"Hii kazi ni kazi mbaya, hawa walijitolea maisha yao kwa sababu hata mimi mtikisiko nilioupata naujua mwenyewe lakini nilijipa moyo kwamba lolote ninalopitia, sijali ili tu matokeo mazuri yawe kwa ajili ya watanzania walionipigia kura niwe rais wao," alifafanua.

Alizitaja faida za makubaliano ya Barrick na Serikali ambayo yametajwa kuwa ya karne kibiashara kwamba pamoja na zingine, ajira kwa watanzania migodini zitaongezeka, kutakuwa na ulipaji wa kodi na ushirikiano kwenye usimamizi wa migodi kwenye ngazi za utawala utakuwa wa ubia.

Rais Magufuli aliongeza kwa kuwashukuru wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kukubali kulifanyia kazi vizuri suala la Hati ya Dharura, iliyohusu kupitisha mapendekezo ya serikali kwenye sheria za madini, ambayo baadhi ya wabunge waliona haina umuhimu lakini matokeo yake ndio yameipa Tanzania heshima kwenye ulinzi wa rasilimali zake.

"Ninawashukuru sana wabunge, mmeonyesha uzalendo mkubwa kwenye kupitisha sheria hii ya madini lakini pia wananchi tunawashukuru kwa uvumilivu wenu, mmesikia mengi lakini bado mmeendelea kuiunga mkono serikali," alisema rais.

Aliahidi kuendelea kutekeleza yale aliyoyaahidi kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi wakati akiomba ridhaa ya wananchi mwaka 2015 na kwamba siku moja wasiomuelewa leo, watakuja kumwelewa nia yake kwa watanzania.

MAZUNGUMZO TANZANITE, ALMASI
Dk. Magufuli alisema, baada ya mazungumzo ya dhahabu, kamati husika, inapaswa kuanza kushughulika na Tanzanite na Almasi ambapo alimtaka Profesa Kabudi na timu yake kuanza mara moja mazungumzo na wahusika.

Alisema anafurahishwa na dalili za mafanikio zilizoanza kujitokeza baada ya kampuni ya Tanzanite One inayohusika na biashara ya Tanzanite, kusema ipo tayari kwa mazungumzo pale itakapohitajiwa kufanya hivyo na serikali.

"Mwenyekiti naomba kazi ianze na tayari Tanzanite One wamesema wapo tayari kwa mazungumzo," alisema Rais Magufuli.

AWAITA WAFANYABIASHARA
Kwa kuonyesha kuwajali wafanyabishara wa ndani, Rais Magufuli alisema, huu ndiyo wakati wa kufanya biashara kwenye sekta zote nchini kuanzia nishati, madini na viwanda.

Alisema serikali yake inawapenda wafanyabiashara na inaamini wana uwezo wa kumiliki hata migodi mbalimbali hivyo milango iko wazi kwa wao kuchangamkia fursa hiyo ya kulijenga taifa lao kupitia sekta ya biashara.

Rais Magufuli, aliutambua uwepo wa Dk. Reginald Mengi na Godfrey Simbeye wa TPSF ambao aliwataka kuufanyia kazi ujumbe wake huku akiwataka wananchi na Kituo cha Uwekezaji (TIC), kuitangaza Tanzania na fursa zake za uwekezaji kokote duniani.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye hafla hiyo, baadhi ya waliyohudhuria  wakiwemo viongozi wa dini, wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wa vyama vya upinzani walisema serikali inastahili pongezi kwenye jitihada ambazo tayari zimefanyika kulinda rasilimali za taifa na ambazo bado zinaendelea kufanywa.

Mussa Azzan Zungu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Almasi alisema, wameridhishwa na kazi iliyofanywa na kwamba, Rais Magufuli ni kiongozi ambaye watanzania wanapaswa kujivunia kwa kumuunga mkono kwenye kila jitihada anayoifanya kulijenga taifa la Tanzania.

Naye Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Ally, alisema viongozi wa dini hawana cha kumlipa rais zaidi ya kumuombea afya njema ili andelee kuwatumikia watanzania kwenye masuala mbalimbali.

Alisema Dk. Magufuli hatakiwi kusikiliza maneno ya mitaani, kwa sababu kwa yeyote anayefanya wema kwenye masuala yenye maslahi, hakosi kulaumiwa na wengi ambao kwa namna moja au nyingine walikuwa wakinufaika kwayo.

"Wewe rais wetu ni mwema kama ambavyo vitabu vya dini vimesema kuwa taifa linalohitaji matengenezo, linahitaji mtu mwema hivyo sisi tunaamini tutakuwa wema pia kwa sababu yako, usiwasikilize wanaokulaumu... kalaumiwa Mwenyezi Mungu, Mitume na watu wema zaidi," alisema.

Profesa Ibrahim Lipumba kwa niaba ya viongozi wa vyama vya siasa, alisema upinzani ulipiga kelele suala la mikataba mibovu ya usiri kwenye sekta ya madini na kwamba ni ajabu kama watu hao hao wataanza kupinga yanayofanywa na serikali kwa sasa.

Alitahadharisha watanzania watakaopata fursa ya kuiwakilisha Tanzania kwenye ubia na kampuni za kigeni za madini kuwa watangulize uzalendo ili kipande cha faida kinachostahili kwa serikali kitolewe kwa weledi na si kwa dhuluma.

"Unaweza kushangaa mgawo wa faida unaambiwa ni asilimia 0, sasa sifuri ikigawanywa 50 kwa 50 unaweza kuona tutapata 0 wakati labda kuna faida kubwa tu ilipatikana ikafichwa kutokana na ukosefu wa weledi wa watu wetu," alisema.

Alisema utanzania kwenye masuala ya maendeleo daima unapaswa kuwa mbele kwanza halafu vyama baadaye hivyo Rais Magufuli anatakiwa kuendelea kushikilia hapo hapo kwa mashali ya taifa.

Waziri wa Madini, Angella Kairuki, kwa nafasi yake alisema, ataendelea kufanya kazi kwa ukaribu na kamati za madini zilizotunukiwa vyeti jana na rais, ili kudhibiti upungufu uliopo ikiwemo utoroshwaji wa madini ili sekta ya madini iendelee kutoa mchango mkubwa kwenye pato la taifa.

"Tunakupongeza sana mheshimiwa rais kwa kazi nzuri ambayo imefanyika, sisi kama wizara mpya tunaahidi kuendelea kupambana na ulinzi wa rasilimali zetu za madini kwa kuziba mianya yote ya utoroshwaji wa madini kwenye maeneo yote," alisema.

Wajumbe waliotunukiwa vyeti na rais jana ni Mwenyekiti Profesa Palamagamba Kabudi, Spika Job Ndugai aliyewakilishwa na mke wake Fatma Ndugai, Profesa Abdulkarim Mruma, James Mgosha, Dk. Yamungu, Geofrey Mwambe, Adolph Ndunguru, Profesa Andrew Luoga, Kasmir Kisaki na Andrew Massawe.

Wengine ni Lusajo Asubisye, Tedy Luasha, Ardegen Mwaipopo, Moses Moses, Royal Lienga, Andrew Mwangakala, Michael Kambi, Profesa Longinus Lutasitara na Dk. Oswald Mashindano.

Pia, Gabriel Malaba, Utano Kisaka, Profesa Rwanura Ikinwa, Profesa Buchweshaiga, Dk. Athuman Ngenya, Dk. Joseph Philip, Dk. Ambrose Matolo, Mohammed Makongoro na Henry Gombera nao walipewa vyeti.

OMAN KUWEKEZA SEKTA YA VIWANDA VYA NYAMA


WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, amekutana na Waziri wa Uwekezaji wa Oman, Salim Al Ismail na kujadili uwekezaji wa viwanda katika sekta ya mifugo na uvuvi.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Jijini Dar es Salaam, Mpina alimueleza Salim kuwa, Tanzania imekuwa ikizalisha nyama tani 36, kwa siku na inafanya  biashara hiyo kwa nyama ambazo hazijakatwa katika nchi za Falme za Kiarabu, ikiwemo Oman.

Alisema wakati umefika kwa nchi hizo mbili kushirikiana katika sekta ya mifugo na uvuvi, ili kuwekeza katika viwanda vya ndani vya nyama kwa kuendeleza vilivyopo na kujenga vipya.

“Ni wakati wa nchi hizi kuona namna ya uwekezaji tunaoweza kuufanya.
Tunatambua ujenzi wa kiwanda cha nyama cha Ruvu, ambao umefikia asilimia 51 kukamilika, lakini ipo haja ya kufungua fursa nyingine za uwekezaji,”alisema.

Alisema ni muhimu viwanda vyote vya nyama vya ndani, vikidhi mahitaji na kuweza kuuza nyama nje ya nchi.

Kwa upande wake,  Waziri wa Oman, Al Ismail alipoelezwa kuhusu viwango na madaraja mbalimbali ya nyama nchini na mtaalamu kutoka wizara hiyo, alisema kuwa ameridhishwa na hatua zilizopo.

Waziri huyo alisema wapo tayari kuwekeza katika sekta ya viwanda vya nyama na kuisaidia Tanzania kutafuta soko nchini Marekani kupitia Oman.

Alisema wanacho cheti  na kibali kilichothibitishwa na Mamlaka ya Dawa Marekani, hivyo ni vizuri kushirikiana katika kutumia fursa hiyo.

“Tunaweza kuchukua nyama kutoka Tanzania na kuingiza Marekani bila kulipa ushuru. Tunapaswa kuwa na vyeti halali ili kupata soko katika nchi nyingine,”alisema.

Waziri huyo alisema, kampuni binafsi kutoka Oman, zipo tayari kufanya biashara katika eneo hilo, hivyo ni wakati wa Tanzania kuonyesha utayari.

“Hizi bidhaa za nyama ni lazima zitoke kwenu kwa sababu sisi hatuna maji wala majani ya kulisha mifugo kama ng’ombe, mbuzi na kondoo, ambao huchinjwa kwa wingi baada ya Hijja,”alisema.

Akizungumzia sekta ya uvuvi, waziri huyo alisema wamenunua teknolojia ya kisasa ya uwekezaji katika fukwe ya Bahari kutoka Texas, Marekani, inayojulikana kitaalamu kama ‘Shrim farming’, inayoruhusu uzalishaji wa chakula cha samaki wavuliwao katika maji marefu bila kuharibu mazingira.

Waziri huyo alisema teknolojia hiyo inaweza kutumika katika uwekezaji wa fukwe ya bahari ya Hindi nchini, ikiwemo eneo la Bagamoyo, kwa kuzingatia tathmini ya athari ya mazingira na ujenzi wa miundombinu ya barabara ili kuwasaidia wavuvi wadogo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Yohana Budeba, alisema hii ni fursa pekee kwa wafanyabiashara wa Oman, kuwekeza au kushirikiana na wafugaji na wavuvi wa ndani, kwa kuwa kuna samaki wengi wa kutosha kumudu viwanda vya kuchakata  na kuwezesha biashara kubwa ya samaki ndani na nje ya nchi.